*Saruji, ngano, vifaa vya ujenzi, alizeti vinahitajika

*Asema majirani zetu wameshaanza kunufaika mno

 

Ushauri umetolewa kwa Tanzania na Watanzania kuamka na kuchangamkia fursa za uwekezaji na biashara zilizojitokeza katika taifa jipya la Sudani Kusini.

 

Ushauri huo umetolewa na Meja Jenerali Wynjones Kisamba, Naibu Kamanda wa Vikosi vya Kulinda Amani katika Jimbo la Darfur (UNAMID), alipokutana na kubadilishana mawazo na maofisa wa Ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, New York.

 

Meja Jenerali Kisamba amezuru Umoja wa Mataifa kwa ziara ya kikazi na mafunzo ya maofisa wa ngazi za juu katika balozi za Umoja wa Mataifa  yaliyoandaliwa na Idara ya Operesheni za Ulinzi wa Amani ya Umoja wa Mataifa (DPKO).

 

“Tanzania tuna kila sababu ya kuwekeza nchini Sudani Kusini, zipo fursa nyingi mno kuanzia upelekaji wa chakula hadi ujenzi. Nikiwa nyumbani (Tanzania) hivi karibuni, nilikutana na viongozi mbalimbali na kuwaelezea juu ya fursa hizi,” amesema Meja Jenerali Kisamba na kuongeza: “Lakini wasiwasi wangu ni kwamba tunachelewa wakati majirani zetu wamekwisha zichangamkia fursa hizo na wako mbali sana sasa, kwa maneno mengine naweza kusema wameishaingia hadi jikoni.”

 

Katika mazungumzo yake na maofisa wa ubalozi, Naibu Kamanda huyo wa vikosi vya UNAMID amebainisha kwamba kama kweli serikali, kwa kushirikiana na sekta za umma na binafsi zikiamua kuingia kibiashara Sudani Kusini, hakuna tutakachopoteza.

 

“Sudani Kusini ndiyo kwanza wanaanza kuijenga nchi yao, wana changamoto nyingi, sisi tunaweza kuwasaidia kwa maana ya kuwekeza na kwa kufanya biashara. Kwa mfano wale wanakula sana chapati, hawana ngano, tunaweza kuwauzia ngano, wanahitaji mafuta ya kupikia tunayo alizeti, wanahitaji vifaa vya ujenzi, tuna viwanda vya saruji na nondo – kwa kweli fursa zipo.

 

“Tunachotakiwa ni kujipanga tu na kuwahamasisha wafanyabiashara wetu. Lakini kubwa na la msingi zaidi ni lazima Watanzania tukubali kuthubutu,” amesisitiza Meja Jenerali Kisamba kwa hisia kali.

 

Kuhusu suala zima la operesheni za kulinda amani katika Darfur, eneo ambalo yeye ni Naibu Kamanda akiongoza bataliani 17 zenye wanajeshi 17,364 wakiwamo polisi 5,511 kutoka nchi 52, Meja Jenerali huyo amesema kuwa kama ilivyo katika fursa za uwekezaji, Tanzania pia bado inayo fursa kubwa ya kujiimarisha zaidi katika eneo la ulinzi wa amani.

 

Akaeleza kwamba wanajeshi kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na askari polisi wanaohudumia katika Jimbo la Darfur, wameonyesha uhodari wa hali ya juu kiasi cha kupigiwa mfano na mataifa mengi makubwa.

 

“Si kama najisifu, lakini watu wetu wameonyesha uhodari na maarifa ya hali ya juu, wanafanya kazi nzuri, wanaheshimika, wana nidhamu, wanaitangaza vema Tanzania.

 

“Tumekuwa tukizungumzwa vizuri sana na baadhi wa washirika wetu kama vile Norway na Sweden. Na hii inatupatia fursa ya kujipanga vizuri zaidi kwa maana ya kuwaandaa na kuongeza idadi ya wanajeshi na askari polisi katika eneo hilo,” amesema.

 

Amesema licha ya mahitaji makubwa ya wanajeshi, kuna mahitaji makubwa ya askari polisi, hasa wanawake. “Tunahitaji kuwekeza katika rasilimali watu kwa maana ya wanajeshi wetu na polisi wetu. Wanajeshi wetu ni wazuri mno, na polisi wetu ni wazuri pia, lakini, na hasa kwa polisi wetu na kwa kuwa ndiyo wameanza karibuni.

 

Hawa wanahitaji mafunzo zaidi katika ngazi ya kimataifa kutokana na ukweli kwamba mafunzo wanayopewa ni yale ya kukidhi mahitaji ya ndani ya nchi. Lakini ni kundi linahohitajika sana hivi sasa katika operesheni za kulinda amani,” amesema.

 

Kwa kulitambua hilo, ameeleza kwamba michakato mbalimbali inafanyika, ambayo pamoja na mambo mengine, inahusisha kuwajengea uwezo na maarifa wanajeshi na polisi ili waweze kukidhi mahitaji na viwango vya kimataifa.

 

Hatua hiyo itarahisisha kuwapo kwa utayari wa rasilimali watu kuhudumu katika operesheni za kulinda amani mara jumuiya ya kimataifa inapowahitaji.


Kuhusu hali katika Jimbo la Darfur na maeneo mengine, Meja Jenerali Kisamba amesema kuwa ingawa wanajeshi wa kulinda amani wanajitahidi kutekeleza majukumu yao, ukweli ni kwamba hadi sasa hakuna amani ya kulinda jimboni Darfur.

 

Amesema wanajeshi na polisi waliopo katika eneo hilo wanaendelea kutekeleza majukumu yao yakiwamo ya kulinda raia, jukumu linalobaki kuwa kati ya majukumu makubwa kabisa ya UNAMID.

 

Kwa upande wake, Tanzania kwa sasa inacho kikosi kimoja cha kijeshi, kombania moja ya wahandisi wa medani, waangalizi wa amani na maofisa wanadhimu na polisi washauri ambao idadi yao wote hadi Mei mwaka huu ilikuwa 1,330.

 

Idadi hiyo inaifanya Tanzania kuwa katika nafasi ya 19 kidunia kati ya nchi 115 zinazotoa walinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa.