Na Dotto Kwilasa,Dodoma.

CHEMBA ya wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC)kwa kushirikiana na Trademark Africa wamefanya mafunzo juu ya ushiriki wa wanawake na makundi maalum katika kada ya manunuzi ya Umma lengo likiwa ni kuongeza upatikanaji wa masoko na huduma za kibiashara.

Mkurugenzi Mtendaji wa TWCC Mwajuma Hamza ameeleza kuwa mafunzo hayo ni utekelezaji wa Serikali inayoelekeza kuwa asilimia 30 ya bajeti za ununuzi kutengwa kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu ili kukabiliana na changamoto za kupata kandarasi kutokana na ukosefu wa ujuzi wa kiufundi, upungufu wa taarifa na ukosefu wa kujiamini.

Akizungumza kwenye mafunzo hayo Jijini Dodoma November 12,2024 Mkurugenzi huyo ametoa shukrani za dhati kwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwaunga mkono wanawake na vijana kupitia juhudi za kuwawezesha kiuchumi na kuwafungulia milango ya fursa ndani na nje ya Tanzania.

Akizungumzia mafunzo hayo amesema yameshatolewa kwa awamu mbili na kuwanufaisha wanawake 70 ikiwa ni pamoja na kuwaunganisha na mifumo mbalimbali ya manunuzi ikiwemo ya Nest na mfumo wa umoja wa mataifa wa manunuzi wa UNGM.

Mkurugenzi huyo mtendaji wa TWCC amesema asilimia 75 ya washiriki hao wamefanikiwa kuingia kwenye mfumo na kuanza kuomba tenda mbalimbali na kupewa msaada wa kitaalam kuhusu biashara.

Aidha amewapongeza washiriki waliochangamkia fursa hiyo na kuwataka kuzingatia elimu waliyopewa ili iweze kuleta manufaa kwao binafsi na kwa taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na makundi Maalum Felister Mdemu ameeleza kuwa Serikali imeendelea kuhimiza Taasisi za umma kutenga asilimia 30 ya bajeti ya manunuzi kwa ajili ya wanawake na makundi maalum.

Amesema Kwa kutenga asilimia hizo kutawawezesha kunufaika na tenda zinazotolewa na Serikali pamoja na Taasisi za umma na kueleza kuwa Wizara hiyo imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali katika kuwezesha wanawake kiuchumi nchini na TWCC ni mdau mmojawapo katika eneo la kiuchumi.

“Sote tunatambua kuwa ushiriki wa wanawake na vijana katika ununuzi wa umma bado unakabiliwa na changamoto kubwa, changamoto hizo mara nyingi hutokana na ukosefu wa utaalamu,taarifa zisizotosha kuhusu michakato ya zabuni,gharama ya upatikanaji wa mitaji pamoja na wajasiriamali wengi wadogo kuendelea kutokuwa na vigezo vya kukopesheka”

“Kwa wajasiriamali wote wanawake na vijana hapa leo ninawahimiza kutumia fursa hii adhimu,kuuliza maswali,kushirikiana na wakufunzi na kushirikiana na wenzao kwa kujenga mtandao wa kufanya kazi kwa umoja,hii ni fursa yao ya kupata zana,ujasiri na msaada wanaouhitaji ili kushiriki kikamilifu na kufanikiwa kupata zabuni,mikataba ya sekta ya umma na ya kibinafsi,maarifa wanayotapata leo si kwa ajili ya biashara zao tu bali kwa jamii nzima na maendeleo ya taifa letu”

Nae Noela Joel mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo amesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa kwani yatawawezesha kupata taarifa ya namna gani ya kufanya manunuzi kwani wengi hawana taarifa za kutosha kwani wafanyabiashara wengi hawajui tenda ni nini na wanafanya vipi manunuzi hivyo elimu ya kutosha inapaswa kutolewa kwa wajasiriamali wadogowadogo.

Aidha ametumia nafasi hiyo kuiomba Serikali iwapatie mikopo na kuangalia namna ya kuwawezesha kwa namna yoyote ile na kueleza kuwa kuna wakati wanapata tenda lakini lakini mtaji ukawa ni mdogo.

Chama Cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania(TWCC) ni chama kikuu kilichoanzishwa mwaka 2005 Kwa lengo kuu la kukuza uwezeshaji wa kiuchumi wa wanawake Tanzania ambapo chama hiki kina zaidi ya wanachama 10,000 kutoka katika matawi 27 ya mikoa yote Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar.