Ukisoma Kamusi Kuu ya Kiswahili moja ya maana ya neno HABARI ni jambo, tukio au hali fulani iliyo muhimu na ya aina ambayo ni ngeni kwa walio wengi.
Jamii ya wasomaji wa magazeti, wasikilizaji wa redio na watazamaji wa televisheni inayofaa kutaarifiwa kwao.
Kadhalika kwenye taaluma ya uandishi wa habari neno habari linaainishwa: “Habari ni tukio geni lenye mvuto na ukweli.” Katika lugha ya Kiingereza inaelezwa kwa ufupi: “News is that which is new, interesting, and true.”
Hii ina maana kwamba habari ni tukio ambalo si la kawaida limetokea katika jamii na kusanifiwa kwa usahihi kutoa maelezo ya ukweli. Habari hiyo iwe ya uchumi, siasa, vita, kifo, mchezo, ngoma na kadhalika. Habari ni kiungo muhimu sana katika mawasiliano ya mtu na mtu.
Nimetoa maelezo haya kutaka kuonyesha maana na umuhimu wa habari kati ya vyombo vya habari na jamii yoyote inayohabarishwa mambo au matukio na kuchukua hatua stahili katika utekelezaji wa jambo au tukio hilo.
Katika makala haya suala kuu ni jinsi gani habari inayozungumziwa inamfikia msomaji wa gazeti, msikilizaji wa redio au mtazamaji wa televisheni.
Nazungumzia chanzo cha habari kinasemaje na mpokeaji wa habari anahabarishwaje. Nipo katika mitaa ya chanzo cha habari, uelewa, uandikaji, uhariri na usambazaji wa habari. Umakini unahitajika sana kupita katika mitaa hii.
Katika sakata la utoroshwaji wa dhahabu mkoani Mwanza, Rais Dk. John Magufuli alisoma gazeti moja lililosema wale polisi waliohusika kushika wamewekwa ndani. “Sasa hata watu wa magazeti, jamani mjifunze, muwe mnauliza vizuri information.”
Walioshikwa ni polisi wale waliokuwa wakiwasindikiza watuhumiwa wa utoroshaji wa dhahabu na kudai rushwa ya shilingi bilioni moja.
Kocha wa timu ya Klabu ya JS Saoura, Nabil Neghag, amelaumu magazeti ya Tanzania yameandika timu yao ni dhaifu sana, hawana kocha, hawana chochote. Alichosema sicho kilichoandikwa. Amesema waandishi hawana experience katika kuandika. Ni tabia mbaya, inaondosha sifa ya waandishi.
Kocha huyo amekiri kusema, katika mkutano na waandishi wa habari, alisema timu yao ni ndogo sana, haina uzoefu kama ilivyo timu ya Simba ambayo ni kubwa. Amesikitishwa na kuhuzunishwa na habari zilizoandikwa magazetini.
Habari zote hizi si nzuri kwetu waandishi wa habari kwa sababu zinapoteza sifa yetu ya uandishi. Zimezidisha kutia dosari katika weledi wetu wa habari na zinathibitisha shaka na lawama zilizowahi kutolewa na Rais Benjamin Mkapa na Rais Jakaya Kikwete enzi za uongozi wao.
Rais wa Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Benjamin Mkapa alisema kuwa hatuko makini katika kuandika na kutoa habari. Alisema kuwa tusiandike habari zake, tunazipotosha.
Naye Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, alisema kuwa taasisi ya habari ina ‘makanjanja’. Hawezi kuvumilia kuwa na waandishi wasio na sifa ya uandishi kuandika habari. Tujirekebishe.
Binafsi naomba radhi nikiwa mwandishi wa habari kwa yaliyotokea. Naamini wakati umefika katika vyumba vyetu vya habari kurekebisha makosa na kuwa makini katika kupokea habari. Ukweli lawama kama hizi zinaumiza na zina fedhehesha. Waandishi tuonyeshe weledi wetu wakati wa kuchukua habari.
Kwa wale walioandika habari zilizolalamikiwa ni busara, ustaarabu na uungwana kwao kukiri makosa. Naomba iwe hivyo. Lakini tuelewe leo zimekosewa habari za nidhamu na michezo. Kesho huenda zikakosewa kuandikwa habari za siasa zenye chokochoko na hizo zina hatari. Tujitathmini.
Mwandishi si haramu, mweledi mtaalamu,
Huandika nidhamu, habari zenye tamu,
Michezo na elimu, watu hutabasamu,
Uandishi dhahabu, si moto jahanamu.