Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeshauriwa kutafuta wadhamini wenye uwezo wa kujenga vituo vya kukuza vipaji, kuliko kuendelea kuokoteza wachezaji.
JAMHURI limezungumza na wadau wa soka, ambao wamesema mashindano ya vijana chini ya umri wa miaka 17, yanayoendelea nchini Gabon, yameonesha udhaifu kwenye timu ya Serengeti Boys.
Hata kutolewa kwa vijana hao katika mashindano hayo yanayoendelea nchini Gabon, kumetokana na kukosa msingi imara tangu awali, ikilinganishwa na washindani wao.


Ujio wa wadhamini kama Sportpesa unaweza kuleta mabadiliko, kama wadhamini hao wa Serengeti Boys, Simba, Yanga na Singida United, watajikita katika kusisitiza kuwapo kwa programu ya vijana kama sehemu ya masharti ya udhamini.
Mashindano ya AFCON U-17, yameonesha udhaifu wa klabu za Tanzania katika kuwekeza kwenye soka la vijana, maana wachezaji wake wengi wamepatikana nje ya mfumo huo.
Mkurugenzi wa Sportpesa, Abbas Tarimba, amealiambia JAMHURI  kuwa ni wakati wa TFF kushirikiana na wadau wa soka nchini, kuhakikisha uwekezaji kwa vijana unaanza kufanyika tangu ngazi ya chini.
 “Malengo yatafikiwa pale TFF na klabu zitakapoanza kutilia mkazo timu za vijana wenye vipaji, uwepo wa shule za michezo katika mikoa yote nchini,” amesema Tarimba.


Amesema ni zaidi ya miaka 30 imepita tangu Tanzania ing’are katika riadha kupitia wanariadha wa zamani kama Francis Naali, Samson Ramadhan, Gidamis Shahanga, Juma Ikangaa, Suleiman Nyambui na Filbert Bayi, huku akisisitiza uwekezaji ulifanyika.
 “Katika vita hii ya kuirudisha nchi katika ramani ya michezo, TFF haina budi kutafuta udhamini wa kujenga vituo vingi vya soka nchini,” ameshauri Tarimba.
Amesema hata mafanikio yaliyopatikana miaka ya nyuma yalitokana na uwekezaji kwa vijana, hali hiyo iliifanya Tanzania kuwa mshindani na kuogopeka lilipokuja suala la michezo ndani na nje ya nchi.
Tarimba, ambaye amewahi kuwa Rais wa Klabu ya Yanga, amesema TFF haina budi kuja na kanuni kali itakayoweka ulazima wa klabu zote kuwa timu za watoto watakaokuja kuwa tegemeo kwa Taifa katika mashindano mbalimbali.
Akizungumza na JAMHURI, Mkurugenzi wa Ufundi, TFF, Salum Madadi, amesema kwa sasa nchi inao makocha wa ngazi za awali wa kutosha na wana uwezo wa kulisaidia Taifa katika kuanzisha vituo vya soka.
“Siku zote TFF imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha klabu zinakuwa na timu za watoto wadogo, kwa kiwango fulani kuna mafanikio japo baadhi ya timu zinakabiliwa na ukata na hivyo kushindwa kumudu kuwa na timu hizo,” amesema Madadi.
 Amesema timu ya Serengeti Boys, iliyoshiriki michuano ya AFCON iliundwa kutokana na vijana walioonesha vipaji kwenye mashindano ya shule za sekondari, Copa Coca-Cola na Airtel Rising Stars miaka miwili iliyopita.
“Lengo letu ni kuendelea kuilea Serengeti Boys ili iwakilishe nchi kwenye mashindano ya Olympic ya mwaka 2020 kwa wachezaji wenye umri chini ya miaka 23,” amesema Madadi.


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, amesema Serikali wanaikaribisha Sportpesa, si kuendeleza michezo tu lakini kuanzisha miradi ambayo itachangia ajira.
Dk. Mwakyembe amesema wadhamini hao wamekuja wakati mwafaka, Serikali kwa kushirikiana na TFF itahakikisha michezo inachezwa kuanzia ngazi ya chini hadi ngazi ya Taifa kwa kushirikiana na wadau wote.
Amesema tayari wizara imekamilisha maandalizi ya rasimu ya Sera ya Maendeleo ya Michezo, ikiwa ni hatua ya mapitio ya Sera ya Maendeleo ya Michezo ya mwaka 1995.
Amesema rasimu hiyo tayari imejadiliwa kuanzia ngazi za awali na kutolewa maoni mbalimbali yanayohitaji kuzingatiwa ambayo wizara inaendelea kuyafanyia kazi.


Kukamilika kwa mapitio ya sera ya maendeleo ya michezo ya mwaka 1995, kutawezesha, pamoja na mambo mengine, kuifanyia marekebisho Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa Na. 12 ya mwaka 1967 na marekebisho yake Na 6 ya 1971 ili iendane na mahitaji ya sasa.
“Ni lazima tuanze kubadilika kuanzia Serikali, BMT, TFF pamoja na wadau wote wa michezo hapa nchini, lengo letu liwe moja, kuhakikisha michezo inachukua nafasi yake kama ilivyokuwa miaka ya 1970,” amesema Mwakyembe.
Kampuni ya Sportpesa ilianzishwa nchini Kenya mwaka 2014, imeweza kufungua ofisi zake katika majiji ya Liverpool, nchini Uingereza, Nairobi, Kenya na Dar es Salaam.