Historia duniani inaonyesha jinsi ambavyo mbinu mbalimbali zimetumika kudidimiza kilimo katika nchi zetu ili tugeuke wategemezi.

Hujuma ya kwanza dhidi ya kilimo chetu ilikuwa enzi ya ukoloni. Wakoloni hawakutaka tujitosheleze kwa chakula au tuanzishe viwanda vinavyotumia mazao ya kilimo.

Enzi ya ukoloni tulilazimishwa kulima mazao yanayokidhi mahitaji ya viwanda vya wenzetu. Ikawa piga ua lazima tulimishwe katani, chai, pamba na kahawa. Baadhi ya wakulima wetu ambao walikaidi kulima mazao hayo wakalima ya chakula waliadhibiwa. Wale waliokubali kulima mazao hayo wakawa ndio wanaohudumiwa na kuitwa ‘progressive farmers’.  Mazao ya chakula yakapuuzwa sana chini ya ukoloni.  Reli, barabara na bandari zikajengwa ili kuwezesha mpango wao.

Baada ya ukoloni ikaletwa mbinu mpya – kitu kinaitwa mapinduzi ya kijani (Green Revolution). Tukafurahia ujio wake sana bila kujua hasa malengo ya green revolution yalikuwa nini. Ikawa kila nchi ya Kiafrika imeweka mpango wa mapinduzi ya kijani katika kilimo. Lakini waliokuwa nyuma ya green revolution ni wenye kampuni kubwa za mbegu, mbolea na viatilifu. Kina Bayer, CIBA Geigy, Sygenta, BASF na wenzao.

Hawa nia kuu haikuwa kuongeza uzalishaji wa chakula kama walivyokuwa wakidai. Nia yao kuu ilikuwa kuongeza soko la bidhaa zao. Huu ndio muda zikaanzishwa benki za mbegu. Eneo la Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ikawekwa pale Lusaka. Mbegu za asili zikafungiwa benki. Mbegu za chotara (hybrids) za kina Bayer ndio zikawa zinatamba mashambani. Ni wakati pia vikaanzishwa vituo maalumu vya kuzalisha mbegu chotara kikiwepo kile maarufu kilichopo Las Banos, Ufilipino kilichokuwa kinazalisha mbegu za mpunga (International Rice Research Centre – IRRI).

Nchi zetu zikawa watumwa wa hizi kampuni kwa mwamvuli wa green revolution. Nchini India mbegu ya asili ya aina ya BASMATI ikakaribia kutoweka! Baadaye ikawekewa hati miliki (patent) ikawa mali ya kampuni. Ikawa marufuku mkulima wa mpunga India kuilima bila idhini au kulipia!

Hata baada ya miaka zaidi ya 20 ya green revolution bado njaa duniani haikutoweka! Kilichotoweka ni mbegu zetu za asili na uhuru wetu wa kujiamulia tulime nini!

Baada ya hadaa ya mapinduzi ya kijani  ikaletwa hadaa mpya. GMseeds. Wengi wanaita GMO! Utaalamu wa GMO unatumika kwenye nyanja nyingi – siyo mbegu peke yake. Kwa hiyo kwenye mbegu inaitwa GMseeds. Tukaambiwa suluhisho la usalama wa chakula (food security) utapatikana kwa kuhimiza kilimo cha GM seeds. Mabingwa wakiwa kampuni ya Monsato ya Marekani.

Ni kweli utaalamu wa GM seeds unaweza kuzalisha chakula kwa wingi kwa kutumia GM seeds au GM tissues. Hakika GM tissues inaweza kuzalisha chakula cha kutosha mkoa mzima kwenye chumba chenye ukubwa wa sebule. Lakini pia GM seeds zina uwezo wa kuzaa kwa wingi mashambani. Hu ni ukweli usiopingika. Lakini kama ilivyokuwa kwa Green Revolution nia siyo Food Security. Nia ni ile ile ya kutufanya watumwa wa mbegu na viatilifu vyao.

Niwape mifano michache ili mjue GMseeds ni utumwa mamboleo:

Mosi, mbegu iliyokuwa genetically modified (GMseed) inaweza kuwa trait-specific. Yaani inakarabatiwa kuwa na sifa maalumu ya kiasili. Mfano, ili iweze kuzaa itahitaji kiatilifu (kimakosa wengi wanaita dawa) maalumu. Mfano ni mbegu ya mahindi au maharage kutoka kampuni ya Monsanto. Ili iweze kuzaa inakulazimu unyunyuze sumu ya glyphosate (inapatikana ndani ya ROUNDUP).

Ukijidanganya ukapalilia na jembe la mkono au na sumu nyingine mahindi au maharage yako hayatazaa. Ni kwamba ‘kizazi’ cha mahindi au maharage kimetolewa na kuwekwa ndani ya ROUNDUP! Unaponyunyuzia ROUNDUP inafanya kazi mbili: kuua magugu na kubebesha mimba maharage au mahindi yako. Utaalamu huu unaitwa TRAIT SPECIFIC TECHNOLOGY. Maana yake ni kuwa mkulima akishanunua mbegu hii atalazimika kurudi dukani palepale kununua ROUNDUP! Hana ujanja! Huu ndio utumwa mamboleo!

Pili, kuna utaalamu unaitwa TERMINATOR TECHNOLOGY. Mbegu inakarabatiwa inabaki na kizazi kimoja tu (F1 generation).  Wengi wanajua hii kupitia mbegu chotara. Ukinunua mbegu chotara itazaa kwa msimu mmoja tu. Msimu wa pili inakulazimu kwenda kununua mbegu tena hata kama umevuna magunia elfu!  Utaalamu huu unatumika sana kuzalisha GM seeds.

Tatu, utalamu wa GENETIC MODIFICATION unaweza kutumika kuamua mbegu itakaa muda gani baada ya kuvunwa bila kuharibika au itunzwe kwa njia gani au sumu gani! Yaani ukivuna huna uhuru wa kuiweka muda mrefu hadi bei ipande! Unatakiwa uuze halafu uwahi kununua mbegu kwa msimu ujao. Huna uhuru wa kuihifadhi kwa kutumia majivu au moshi au kwenye kihenge ulichosiriba mavi na mkojo wa ng’ombe! Uamuzi huo unakuwa mikononi mwa kina Monsanto, siyo mkulima! Mahindi yako, lakini wanakuamulia uuze lini na uhifadhi kwa muda gani?  Utumwa mamboleo.

Tanzania lazima iwe makini sana na hii teknolojia hasa kwenye MBEGU. Ama sivyo kilimo chetu kitakuwa mfukoni mwa kina Monsanto.

Hadaa hii ya GMseeds iliambatanishwa na tafsiri potofu ya usalama wa chakula (food security). Kwa mujibu wa Umoja wa Matiafa [UN] (kumbuka kampuni hizi zina nguvu sana) usalama wa chakula ni KUJITOSHELEZA KWA CHAKULA. Pia ili eti nchi ijitosheleze kwa chakula lazima iboreshe kilimo kupitia GM seeds na pia chakula cha misaada (food aid).

Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) likapewa kazi ya kupigia debe GM seeds na Shirika la Mpango wa Chakula (WFP) chakula cha misaada. Dhana hii ni potofu mno. Baadhi yetu tulioshiriki katika UN High Level Task Force on Food Security tulitoa mawazo yetu kwa nini hii ni dhana potofu.

Kwa mfano sisi tulisema kuwa suala si Food Security, bali Food Sovereignty. Lazima wakulima wawe na sovereignty katika kuzalisha chakula. Wamiliki ardhi, mbegu, soko, pembejeo na kadhalika. Kinyume cha hapo ni FOOD COLONIZATION. Pia tulipinga dhana ya kuleta food security kupitia chakula cha misada. Chakula cha misaada kina madhara yake mengi kwa nchi. Kinaua kilimo cha nchi, kinachochea uvivu, kinatumika kutupa vyakula visivyofaa kwa afya ya binadamu kwenye nchi changa, kinatumika kuingiza GM seeds kinyemela kwenye nchi changa, n.k.

Kuna nchi chakula cha misaada kimetumika kuhujumu imani za watu. Kuna nchi chakula cha misaada kimetumika kuingiza kwa makusudi GM seeds. Lazima wakulima wetu wawe na food sovereignty ndio tutafanikiwa. Bahati mbaya nchi nyingi za Kiafrika ikiwemo Tanzania ziliingia mkenge hadi zikaanzisha wizara za AGRICULTURE AND FOOD SECURITY! Wangeanzisha ‹MINISTRY OF AGRICULTURE AND FOOD SOVEREIGNTY» ndiyo lingekuwa jibu sahihi kwa hawa wahuni wa kimataifa.

Hujuma iliyofuata ikawa kilimo cha mkataba (Contract Farming). Hii ndio mbinu iliyotumika kuwaingiza hawa wanunuzi wa mazao yetu ikiwemo korosho. Kilimo hiki kilianzishwa India na Pakistan haswa kwa wakulima wa pamba. Zao la pamba lilianza kupungua sana duniani ikabidi watumiaji wakubwa wa pamba watunge mbinu ya kujihakikishia udhibiti wa soko la pamba.

Ikaonekana wakulima waingizwe kwenye utaratibu wa mikataba. Anakuja mtu anaingia mkataba na mkulima ambao mkulima analazimika kumuuzia mtu huyo zao lake. Kwa kuwa elimu ya wakulima ni ndogo, mikataba hii ikawa kiama chao. Mwisho wa msimu mkulima analazimika kumuuzia mtu kwa bei ya kutupa! Akijaribu kumuuzia mwingine mkataba unamzuia hata kama huyo mwingine ana bei nzuri zaidi. Hili ndio linawakuta wakulima wengi nchini mwetu. Anadanganyiwa uhakika wa soko kumbe analiwa!

Tukitaka kuepuka huu mtego ni kurejesha utaratibu wa mkulima kuuzia serikali kupitia chama cha ushirika. Ushirika ulikuwa kinga ya mkulima. Tatizo lilikuwa ushirika kutowajibika kwa wakulima. Tatizo lilikuwa kutowajibishana! Hii haifanyi ushirika usiwe na maana. Turudishe ushirika, tuwape mamlaka wakulima kuwawajibisha watumishi wa ushirika wanapokosea. Tutaachana na hawa walanguzi walioletwa kupitia hadaa ya contract farming.

Ni vyema waliokabidhiwa dhamana ya kusimamia na kuendesha kilimo chetu wakatambua mambo haya ili wasijetumika bila wao kujua kuwaumiza wakulima wetu. Nawasilisha.