Kwa muda sisi JAMHURI tumekuwa tukiandika habari zinazohusu wasafishaji na wauza mihadarati; na pia matapeli wa biashara ya madini waliokubuhu. Tulichobaini ni kwamba wahusika wakuu kwenye biashara, hii wanalindwa na baadhi ya viongozi wakubwa katika nchi yetu. Mitandao ya uhalifu katika Tanzania ni mipana na yenye nguvu kuanzia ngazi za chini hadi katika vyombo vya ulinzi na usalama.
Biashara haramu ya mihadarati na utapeli inaungana na utakatishaji fedha haramu zinazoingia nchini kupitia kwa watu mbalimbali. Matokeo ya yote haya ndiyo haya tunayoyaona sasa ya baadhi ya Watanzania na wasio raia wa Tanzania kuwa na ukwasi wa kutisha.
Sisi tunasema kwa kujiamini kabisa kuwa wahusika kadhaa muhimu kwenye biashara hii haramu tunawajua. Miongoni mwao tumediriki kuwataja kwa majina, huku tukitambua hatari zinazotukabili. Kinachosikitisha ni kuona kuwa pamoja na juhudi zote zinazofanywa na vyombo vya habari, JAMHURI tukiwa miongoni mwa vyombo hivyo, hakuna hatua za dhati zinazochukuliwa na Serikali kupunguza na hatimaye kukomesha matukio haya yanayolitia aibu Taifa letu.
Matapeli na wafanyabiashara haramu wanajenga nyumba za kifahari katika maeneo mengi ya nchi hii, husasani mkoani Dar es Salaam. Wahusika wa mahekalu haya hawaulizwi wapi wanakotoa mabilioni yanayowawezesha kuyajenga. Mahekalu yanachipuka kama uyoga, lakini hakuna chombo cha dola kinachowafuata wahusika na kuwauliza kama mapato yao wameweza kuyatumia baada ya kulipa kodi stahiki serikalini.
Kibaya zaidi, mahekalu hayo hayalipi kodi zinazotakiwa. Tunaamini kwa dhati kabisa kuwa kama Serikali itaamua, mapato yanayotokana na kodi za mahekalu haya zinaweza kumaliza tatizo la madawati kwa wanafunzi wa Tanzania. Serikali za Mitaa zimejisahau. Serikali Kuu haioneshi kubana eneo hili ili ziwe chanzo kimojawapo cha mapato yake.
Isitoshe, mahekalu haya yanapangishwa kwa matajiri wanaowalipa wamiliki fedha nyingi mno. Fedha zinalipwa kwa dola. Je, mapato hayo yanakatwa kodi? Haya ndiyo mambo yanayopaswa kuangaliwa na Serikali kama vyanzo vya mapato, badala ya kuwabana wananchi makabwela kulipia kodi ya simu ya Sh 1,000 kila mwezi! Hawa wenye mahekalu na magari ya kifahari ndiyo wanaopaswa kukamuliwa kodi ili fedha zitakazopatikana ziweze kuelekezwa kuboresha maisha ya maskini wengi, wakiwamo watoto wa makabwela wanaokosa mikopo ya kuwawezesha kuendelea na elimu ya juu.
Tunatoa wito kwa vyombo vya dola kufanyia kazi mambo yanayoandikwa na kutangazwa na vyombo vya habari. Kama kunatakiwa ushahidi ili kuiwezesha Serikali kutekeleza wajibu wake, sisi tupo tayari. Tunajua nani wanapata fedha kwa njia haramu.
Tunawatambua baadhi ya waliojenga mahekalu kwa fedha chafu, na mahali mahekalu hayo yalipo. Kinachopaswa kufanywa na Serikali ni utashi tu wa kuamua kukomesha hali hii. Tunayasema haya si kwa sababu tuna wivu, bali ni kutokana na ukweli kwamba huu utajiri wa kutisha wa baadhi ya watu hapa nchini unatia shaka. Haupatikani kihalali. Hata hivyo, vita hii ni ngumu kwa sababu hao wanaopaswa kusimamia sheria, baadhi yao ndiyo wanaoshirikiana na wahalifu hao.
Mungu ibariki Tanzania.