Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, jana aliwasilisha bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo ya mwaka 2012/2013.

Alizungumza mambo mengi ambayo kimsingi yanalenga kuifanya ardhi kuwa mtaji usiomithirika katika suala zima la maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa jumla.

 

Hotuba yake imejaa ufafanuzi na maelekezo mengi ambayo kama watendaji watayazingatia, na wananchi wakapewa elimu ya kutosha kuhusu kanuni na sheria zinazotawala ardhi, ni wazi kwamba migogoro mingi, si tu itapungua, bali itamalizika katika nchi yetu.

 

Waziri Profesa Tibaijuka amewasilisha hotuba yake ya bajeti huku jamii ikiwa katika migogoro mingi ya ardhi inayohatarisha amani na utulivu.

 

Kuna migogoro ya wafugaji na wakulima. Hii inapaliliwa na wanasiasa ambao mara kadhaa wamekwamisha matumizi bora ya ardhi.

 

Katika ukurasa wa 17 wa hotuba hiyo, Profesa Tibaijuka ametoa angalizo zito kwa kusema, “Naziagiza mamlaka za vijiji na halmashauri kufuata sheria, kanuni na taratibu za kugawa ardhi ili kuepusha malalamiko na migogoro isiyo ya lazima.

 

Nasisitiza kuwa ardhi kwa ajili ya wawekezaji hutolewa na Kamishna wa Ardhi kwa mamlaka ambayo yako chini ya Rais. Hakuna tena njia nyingine ya kugawa ardhi nje ya utaratibu huu.

 

“Ukiwa na ardhi yako ukaamua kumpa mtu mwingine huna budi kuirudisha kwa Kamishna ili igawiwe upya kwa mtu mwingine. Tofauti ni kuhamisha miliki yote ya ardhi yako kwa mtu mwingine kwa kumuuzia.

 

Makubaliano yanayofanyika kati ya halmashauri na wawekezaji au wamiliki wengine na wawekezaji nje ya utaratibu huu ni batili, sharti yapate baraka za Kamati ya Kugawa Ardhi ya Taifa kabla hatimiliki mpya hazijatolewa.”

 

Anachokisema hapa Profesa Tibaijuka ni kwamba taifa letu tayari linakabiliwa na hatari ya migogoro ya ardhi kutokana na, ama wananchi kutojua sheria, au kwa makusudi yanayofanywa na baadhi ya viongozi na watendaji.

 

Lililo wazi ni kwamba ardhi ya Tanzania kwa sasa inamezewa mate mno. Watetezi na wapigania umoja katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, pamoja na dhamira zao nyingine nyingi, dhamira yao kuu ni ardhi.

 

Tunatoa rai kwa Serikali, watendaji na wananchi wote kuwa makini katika suala la ardhi. Watu wachache wanaohodhi malefu ya ekari ni lazima wadhibitiwe sasa, vinginevyo siku si nyingi Watanzania watagombana kwa sababu ya uhaba wa ardhi na wengi watakuwa manamba.

 

Mwaka 1958, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alisema,Katika nchi kama yetu, ambayo Waafrikani maskini na wageni ni matajiri, kuna uwezekano mkubwa kwamba Mwafrika akiruhusiwa kuiuza ardhi, katika miaka themanini au miaka ijayo, ardhi yote ya Tanganyika itamilikiwa na matajiri wageni, na wenyeji watakuwa watwana. Lakini hata kama wageni wasingekuwa matajiri, litaibuka tabaka la Watanganyika matajiri wajanja. Tukiruhusu ardhi iuzwe kama kanzu, katika muda mchache, kutakuwa na kundi dogo la Waafrika wakiwa na ardhi na walio wengi watakuwa watwana.”

Tuyatafakari maneno haya.