Tayari Bunge Maalumu la Katiba limepitisha rasimu ya Katiba inayopendekezwa.

Rasimu hiyo iko tayari kwa ajili ya kupelekwa kwa wananchi kupigiwa kura baada ya kupata akidi ya theluthi mbili iliyotakiwa kisheria kwa upande wa Tanzania Bara na Visiwani.

Kabla ya kupitishwa, bunge hilo litakumbukwa kwa kutawaliwa na mikimikiki, kejeli na vijembe ndani na nje ya ukumbi.

Kuna waliotabiri rasimu ya Katiba itakayopendekezwa haitapatikana. Waliueleza na kuuaminisha umma wa Watanzania kuwa theluthi mbili inayotakiwa kisheria haitapatikana.

Hata hivyo hayo yaliyotabiriwa na kuhubiriwa hayakutimia. Rasimu inayopendekezwa imepatikana na iko mezani. Kinachosubiriwa ni kura za maoni kutoka kwa Watanzania ama waikatae au waikubali ili iweze kutumika siku zijazo.

Historia ya Bunge Maalumu la Katiba itaandikwa kuwa baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaojipambanua kwa jina la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kususia vikao vya Bunge kwa kile kinachodaiwa kutokuwa na maridhiano miongoni mwa wajumbe.

Ukiondoa madai hayo, UKAWA amabo wanaoungwa mkono na baadhi ya  viongozi wa dini na wanaharakati  wanadai kuwa Bunge lilikuwa likijadili rasimu tofauti na ile iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Msisitizo wao mkubwa ulikuwa ni kutaka Bunge hilo lisitishwe hadi pale maridhiano yatakapopatikana. Haikueleweka walitaka Bunge hilo lisitishwe hadi lini. Kikubwa kwao ilikuwa ni kusitishwa kwa Bunge.

Hali hiyo ya kususia na kuendesha mijadala ilisababisha Rais Jakaya Kikwete kukutana na UKAWA ili kusawazisha mambo ingawa nalo hilo halikuwezekana.

Madai ya maridhiano katika mchakato wa katiba nayo yalikuwa ni ya msingi. Msingi wake ni katika kuendeleza umoja na mshikamano wa kitaifa.

Ndiyo maana tunasema, Tuwe makini kuelimisha wananchi kabla ya Katiba Mpya kwa sababu ya kuhitajika maridhiano.

Kokote pale duniani iwe kwenye ngazi ya familia ama ya kitaifa maridhiano yanapatikana kwa mazungumzo.

Watanzania wamesikiliza hoja kutoka katika pande zote zilizokuwa zikivutana ndani na nje ya Bunge. Sasa ni wakati wao wa kutoa maamuzi ya mwisho. Maamuzi hayo yatafanyika kupitia kura za maoni wakati utakapofika.

Katiba mpya si ya wanasiasa, wanaharakati na viongozi wa dini pekee bali ni ya watanzania wote. Ni vyema kila mtanzania kutokubali kutumika kwa ajili ya kutimiza matakwa ya baadhi ya watu wanaolenga kuwatumia wengine kupitia migomo, migogoro na maandamano kutimiza malengo yao.

Sisi tunaamini kuwa njia sahihi za kupatikana kwa katiba mpya ni zile za amani na sheria inavyoelekeza tofauti ya hapo ni kuibua migogoro mikubwa isiyokuwa na tija kwa taifa tena awamu hii inaweza kuwa ni zaidi ya ile tuliyoishuhudia wakati wa mchakato.