Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia afya njema na amani kila kukicha. Kusema kweli hatuna budi sisi wanadamu kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa mema mengi anayotutendea ikiwa ni pamoja na uhai, ambao tumejaaliwa kuwa nao kutokana na neema na upendo wake kwetu. 

Kwa upande mwingine hata tukisema kwamba tunaishi katika dunia yenye teknolojia za kisasa na ving’amuzi vya kila aina na mitandao ya kijamii kiasi cha ‘kujidai kuwa sasa dunia tunayo viganjani mwetu’, tukumbuke kuwa uhai wetu – tutake au tusitake –  umo mikononi mwa Mwenyezi Mungu aliyetuumba.

Vilevile, hata masuala hayo ya maendeleo – kiteknolojia, kiuchumi, kisiasa na kijamii – anayetuwezesha kuyamudu ni yeye Mungu ambaye ndiye asili ya yote. Kwa hiyo, ni vema na haki sisi binadamu kumshukuru na kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa kila jambo.

Baada ya kusema hayo, nirudi kwenye mada kwa kusema kuwa iko haja kubwa kwa Serikali na wadau wengine kuweka mazingira mazuri na mikakati madhubuti kuwasaidia wazee. Vilevile, kuna haja ya kuchukua hatua za haraka kuwasaidia. Kiini cha kuyasema haya ni kutokana na taarifa iliyotangazwa kupitia Radio Tumaini. 

Wakati nikisikiliza kipindi cha “Hapa na Pale-Magazetini na Dukuduku” asubuhi ya Ijumaa Mei 28, 2016 ndipo nikasikia Mtangazaji (Bwana Remidius Mavere) akimhoji mtangazaji mwenzake (Ms. Valeria Mwalongo) kuhusu taarifa aliyoitoa kuhusu wazee wanaoishi kwa shida hadi mmoja wao kula “udongo” katika Mtaa wa Ngobedi, Kata ya Zingiziwa, Manispaa ya Ilala.

Kulingana na maelezo ya Valeria, yeye kama mwandishi wa habari na mtangazaji, aliwahi kupata tetesi kuwa kuna changamoto zinazohusu matumizi ya ardhi katika Kata ya Zingiziwa iliyopo Manispaa ya Ilala, kilometa chache kutoka Chanika.

Mtangazaji huyo alipozuru Kata ya Zingiziwa na kudadisi juu ya changamoto za matumizi ya ardhi, ndipo akabaini kuwapo wazee katika Mtaa wa Ngobadi wanaoishi kwa tabu kiasi cha “kula udongo”. Taarifa hiyo ilimshtua mno na ndipo akaona ni vema kuifuatilia.

Alifanya hivyo baada ya kuona suala la wazee limemgusa na alitaka apate undani.

Kutokana na juhudi ya Valeria, Radio Tumaini ikaweza kurusha hewani taarifa juu ya wazee wanavyoishi kwa shida mno katika Mtaa wa Ngobadi, Kata Zingiziwa katika Manispaa ya Ilala. Taarifa hiyo ilitolewa kupitia kipindi cha Jamii Tuzungumze, kipindi ambacho pia kinaandaliwa na kutangazwa kupitia Radio Tumaini. 

Naamini kuwa kupitia kipindi hicho, taarifa hiyo ya kuhuzunisha ikamfikia Bwana Mavere ambaye aliona ni vema kumhoji mtayarishaji na mtoa taarifa kwa faida ya watu wengi zaidi.

Mimi sikujaaliwa kusikiliza taarifa hiyo kupitia kipindi cha Jamii Tuzungumze, lakini kutokana na Bwana Mavere kumtaka Valeria atoe maelezo kupitia mahojiano yaliyofanyika Mei 28, 2016 wakati wa Hapa na Pale/Dukuduku; nikaweza kupata ufahamu wa changamoto zinazowakabili wazee wa Mtaa wa Ngobedi. 

Kazi aliyoifanya mwandishi ya kuibua changamoto kama hizo ni mfano wa kuigwa na waandishi wengine. Ingawa nimekuwa nikisikia masuala mengi yakijitokeza kupitia waandishi/watangazaji wengi hasa kupitia kipindi cha ‘Jirani’ cha Radio Tumaini kinachotangazwa nyakati za jioni, lakini pia kupitia sehemu ya Dukuduku wakati wa asubuhi; taarifa kuhusu wazee wa Mtaa wa Ngobadi ilinifanya nijisikie vibaya mno hasa baada ya maelezo kuwa mmoja wa wazee hao anaishi kwa kula udongo.

Nimejiuliza maswali mengi bila majibu. Mathalani, inakuwaje binadamu aishi kwa kula udongo? Je, majirani hawana huruma kidogo angalau wakamsaida chakula?

Binadamu chakula chetu kinatokana na mazao au matunda. Lakini pia tunaunganisha na nyama (mifugo) au samaki na mboga za majani (green vegetables). Mwenyezi Mungu alituumba na kuweka vyote kwa faida ya binadamu. Mimea/miti hustawi kutokana na ardhi/udongo na kupitia udongo hasa ulio na rutuba na hatimaye kutoa mazao kama mahindi, mtama au mpunga. 

Mimea mingine hutengeneza mazao chini ya archi kama viazi, magimbi, mihogo, karoti na kadhalika. Vilevile, kutokana na miti tunapata matunda kama machungwa, maembe, mapapai, ndizi, maparachichi, mafenesi, ukwaju na kadhalika. Mazao na matunda ndicho chakula kinachostahili kuliwa na binadamu; na si udongo. Kutoka kwa wanyama tunapata nyama ambayo inapatikana kwa wanyama kula nyasi na mimea – rasilimali ambazo zinastawi kutokana na udongo. 

Hata wanyama wenyewe hawaishi kwa kutegemea udongo moja kwa moja; iweje binadamu aishi kwa kula udongo?

Haingii akilini kusikia binadamu anaishi kwa kula udongo na kama hivyo ndivyo, inaashiria hali ya hatari sana. Ukienda kwenye baadhi ya masoko kuna wafanyabiashara ambao huuza aina fulani ya udongo eti unapendwa na baadhi ya wajawazito. 

Hata hao wajawazito wa aina hiyo hawatumii udongo huo kama chakula, bali ni hali ya msukumo usio wa kawaida wanaokuwa nao kipindi hicho cha ujauzito. Wakishajifungua hamu ya kupenda kitu kama hicho inakwisha mara moja. 

Kwa hali hiyo, hatuwezi kusema udongo ni chakula cha binadamu. Hivyo, kwa mzee wa Mtaa wa Ngobadi kutegemea udongo kama chakula chake ni aibu kwetu kama jamii na Taifa. Naamini huyo mzee hakufanya hivyo kwa kupenda, bali ni dhiki na makali ya njaa ndipo akaona hakuna jinsi bora ale udongo ili aishi. Hivi kweli mpaka afikie hali kama hiyo jamii inayomzunguka imeshindwa kabisa kumsaidia angalau mlo mmoja kwa siku?

Changamoto za maisha kwa wazee katika Mtaa wa Ngobadi, Kata ya Zingiziwa, Manispaa ya Ilala ziwe fundisho kwetu. Haiwezekani tukaachia hali kama hiyo kwa binadamu kuishi eti kwa kula udongo halafu tukasema tunaishi katika Taifa lenye Watanzania wanaopendana. 

Naelewa kuwa yapo maeneo mengi nchini hasa vijijini ambako hali za maisha ni ngumu mno, lakini sijawahi kusikia eti mahali fulani watu wanaishi kwa kula udongo. Sehemu kadhaa huwa zinakumbwa na ukame au mafuriko na kusababisha mavuno kuwa haba. Mara nyingi Serikali hutoa misaada. Vilevile, wanajamii huwa tunasaidiana ili kunusuru maisha ya wenzetu wanaopatwa na majanga kama hayo. Tunafanya hivyo kwa kutambua kuwa nguvu ya Serikali pekee haitoshi. 

Nashidwa kuelewa imekuwaje kwa wazee wa Mtaa wa Ngobadi wakose msamaria hata mmoja hadi waanze kutumia udongo kama chakula chao? Je, viongozi wa mtaa walichukua hatua gani? Je, Manispaa ya Ilala haikuwa na taarifa juu ya hali kama hiyo?

Sasa hali ndiyo hiyo. Yaliyopita si ndwele, tugange yaliyopo na yajao. Jitihada zifanyike ili tunusuru wazee wa Mtaa wa Ngobadi. Turudi katika mwelekeo wa ‘mpende jirani yako kama nafsi yako’. 

Natambua kuwa si rahisi kutimiza azma hiyo maana kwa hali ya kawaida ya kibinadamu ni vigumu mno kuweza kutimiza, lakini tujitahidi aliye na vipande viwili vya mkate amhurumie anayekula udongo kwa kumgawia kimoja. 

Hii ina maana kwamba Serikali itimize wajibu wake kwa kuwahudumia wazee ipasavyo na jamii pia tusaidiane kadiri ya uwezo wetu. Tuhurumiane na kusaidiana bila kuchoka. Wote tunahitaji kuishi. Kuishi bila chakula haiwezekani labda iwe ni kwa miujiza ya Mwenyezi Mungu.

Kutokana na hali ambayo imejitokeza katika Mtaa wa Ngobadi, Kata ya Zingiziwa nashauri yafuatayo:

(i)Serikali kupitia Manispaa ya Ilala itenge fungu maalumu kuwasaidia wazee wa eneo hilo na maeneo mengineyo. Juhudi zifanyike katika kata zote kuorodhesha wazee wenye umri mkubwa hasa zaidi ya miaka 70 na kati ya hao waorodheshwe wanaohitaji kusaidiwa kwa kukosa ndugu, vipato au kama wanao ndugu, lakini uwezo wao wa kutunza wazee ni mdogo. Kupitia huduma inayotolewa kwa jamii na TASAF, basi wazee wenye shida kupitia viongozi wao wa mitaa watambuliwe na wasaidiwe bila ubaguzi au upendeleo wowote;

(ii) Jamii kupitia sekta binafsi, mashirika ya kidini, na makundi mbalimbali kama umoja wa wanawake, wanaume, vijana, wanamichezo, wanamuziki, wasanii na wengine waweze kutoa chochote kuwasaidia wazee katika jamii tuishimo. Waswahili husema ‘kutoa ni moyo, usambe ni utajiri’. Kilichotokea Mtaa wa Ngobadi kwa wazee wanaoishi hapo kituguse nafsi zetu na kama jamii yenye kupendana tuchukue hatua za haraka ili kunusuru maisha ya wazee hao kwa kuwapatia chakula na mahitaji mengine. Niombe Tumaini Media itusaidie kuratibu suala hili kwa faida yetu sote;

(iii)  Kuanzia sasa niombe Watanzania tusiwe watazamaji au wasikilizaji tu kwa suala la kuwasaidia wazee. Tuwe watendaji na kuchukua hatua pale inapobidi kufanya hivyo. Viongozi wote na kwa ngazi zote watimize wajibu wao ipasavyo na jamii itimize wajibu wake wa kuishi kama ndugu na kuweza kusaidiana ipasavyo. 

Kumwacha binadamu aishi kwa kula udongo itakuwa ni ishara kwa jamii kukosa upendo na kutothaminiana kama binadamu tulioumbwa kwa mfano wa Mungu. Tusikubali hali hiyo itokee tena: Dhamira yetu iwe moja, yaani kuona kila mmoja wetu hasa wazee ambao hawana nguvu za kufanya kazi wanapata chakula na kuishi mahali pazuri. 

Hakuna lisilowezekana iwapo tutadhamiria kweli kutimiza wajibu wetu wa kuwatunza wazee. Mwenyezi Mungu anisaidie; pia akusaidie nawe ili kwa pamoja tuweze kuutambua na kuutimiza wajibu huu muhimu. Tumtangulize Mwenyezi Mungu na kwa msingi wa upendo na huruma tuwasaidie wazee nchini Tanzania. INAWEZEKANA, TIMIZA WAJIBU WA KUSAIDIA WAZEE KATIKA ENEO UNALOISHI.