Mhariri,

 

Wakati umefika kwa Watanzania kuzungumza na kupongeza viongozi wachapakazi wachache tulionao nchini. Hii tabia itafanya viongozi wengine wengi wawaige viongozi wachapakazi.

Nasema hivi kwa sababu mara nyingi Watanzania wamekuwa na tabia ya kulaumu bila kuchambua viongozi wale wanaofanya kazi kwa uadilifu. Siandikii mate ilhali wino upo.

Hivi karibuni nchi yetu imegubikwa na wimbi la viongozi wengi nchini kutokuwa waadilifu, wazalendo na wachapakazi. Hii imeridhishwa na ukaguzi uliofanywa na Mdhibiti na Makaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Kamati mbalimbali za Bunge kukuta ubadhirifu mkubwa wa mali za umma.

 

Dhahiri kwa watu wanaoielewa Tanzania , nchi inayojulikana ulimwenguni kwa amani na utulivu, uozo unatupunguzia hadhi.

 

Ingawaje hali ya ufisadi imedhihirika, lakini bado kuna viongozi wanaochapa kazi, vilevile wakiwa wazalendo wanaopaswa kuigwa nasi. Mithili yao ni ndugu Dk. John Magufuli, Dk. Felix Mwakyembe, Aggrey Mwanri, Profesa Sospeter Muhugo, Philipo Mulugo na Majaliwa Majaliwa. Waheshimiwa hawa wanapaswa kupongezwa kwa dhati kwa vile uchapaji kazi wao umetukuka sana.

 

Mimi binafsi nimekuwa nikifuatilia utendaji kazi wao bungeni au nje ya Bunge. Wanadiriki kukemea maovu na kuchukua hatua kali za kuimarisha kazi, kuwachukulia hatua za kisheria watumishi wabadhirifu.

 

Hakika hii ni mifano mizuri ya viongozi mahiri, weledi na wapenda nchi yao ambao Rais Jakaya Kikwete anapaswa kujivunia.

 

Mwalimu  A.M.N. Wabyaye

0752234702.