Wiki tatu zimepita sasa tangu tuchapishe habari ya askari wastaafu wa Jeshi la Polisi kudai mafao yao na kugomea kambini. 

Nimefarijika baada ya habari hii Rais John Magufuli amemwagiza Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene, afuatilie mafao ya askari Magereza kwa Waziri wa Fedha na Katibu Mkuu wa Hazina.

Rais Magufuli amesema ameambiwa zinadaiwa Sh milioni 546.1, ambazo ni mafao ya kusafirisha mizigo kwa askari Magereza (nadhani). 

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Brigedia Jenerali Suleiman Mzee, amemwambia Rais Magufuli jijini Dodoma wiki iliyopita kuwa kwa sasa wanatumia fedha za ndani kuwalipa askari wanaostaafu, ila kuna watu waliostaafu miaka ya nyuma hawajalipwa. Najiuliza, huu ndiyo utaratibu wa kisheria?

Sitanii, mimi ndiye niliyeandika habari hii kwenye toleo No. 486 la Gazeti la JAMHURI wiki tatu zilizopita. 

Mwanzo niliambiwa kuwa askari Polisi 2,000 hadi 3,000 wamestaafu na hawajalipwa nauli. Baada ya kuandika habari hii, simu yangu sasa imegeuka kuwa call center ya polisi wastaafu. 

Huwezi kuamini, askari anakupigia simu anasema yeye anadai Sh milioni 1.7 tu za kusafirisha mizigo kutoka Mbeya kwenda Singida, lakini hadi leo hajalipwa.

Mwingine anakwambia anadai Sh milioni 4.5 tangu mwaka 2011, hadi leo hajalipwa. Mwingine anasema amefiwa na mke wake, akalazimika kuomba msaada wa magari ya Polisi kusafirisha mwili kwenda kuzika Bukoba kutokea Mbeya, wakati angekuwa amelipwa kwa miaka zaidi ya mitano aliyostaafu, asingekuwapo Mbeya na serikali isingeingia gharama za kusafirisha mwili wa mkewe.

Mwingine anasema aliacha mizigo yake Moshi, akarejea kwao Songea. “Ni miaka minane sasa tangu nimestaafu. Niliacha kijana wa kazi kwenye nyumba niliyokuwa ninakaa kama ofisa na mizigo nikaifungia ndani. Kwa kweli tatizo ni kubwa kuliko maelezo. Tumefanya kazi kwa uadilifu, serikali muda wote inasisitiza fedha inazo, tunaomba itulipe fedha zetu za nauli ya mizigo turejee nyumbani kwetu,” anasema.

Mwingine amesema kiwango cha unyanyasaji kwa askari wenzao walioko kazini kimevuka mipaka. “Unajua katika mambo ya majeshi haya, huwa tunalazimika kufanya uamuzi kwa njia ya amri. Sasa kama binadamu, unakuta wakati mwigine mtu anakuwa anakuchekea akiwa msaidizi wako, ukistaafu akashika yeye nafasi ile, anakulipizia kimyakimya amri ulizokuwa unampa.

“Leo tunatolewa kambini kama wahalifu kwa hapa Mbeya, tunaambiwa askari waliopo kazini wanataka nyumba, hivyo sisi tuziachie, unajiuliza, sijalipwa mizigo yangu ninatoka niipeleke wapi? Tena wengine wametugeuza kama wahalifu. Tunaripoti mara moja kila wiki kuulizia malipo yetu yamefikia wapi, jibu pekee tunalopewa ni kwamba ‘yanashughulikiwa’. Tunaomba Mhe. Rais atusaidie katika hili,” anasema.

Sitanii, mwingine akasema: “Niliposoma Gazeti la JAMHURI na nikaona Mhe. Waziri Simbachawene anakiri uwapo wa tatizo hili, nimefarijika sana. Nimejua anakwenda kulifanyia kazi. Lakini pia niwashukuru nyinyi Gazeti la JAMHURI. Najua baadhi ya waandishi hawawezi kuandika habari zetu, wanakumbuka mambo ya zamani… mmoja aliniambia kutesa ni kwa zamu eti nilimkamata hapo Central Dar, na kwamba sasa nalipia hiyo dhambi… nikawaambia nilikuwa kazini kama wewe ulivyo kazini kaka. Hakunielewa akakataa kuandika habari zetu.

“Tena nikamwambia nilimkamata kwa ajili ya usalama wake, wala si kwa nia ya kumtesa, lakini amenitolea maneno yameniuma kaka, niliporudi nyumbani nikabaki kulia tu. Nikasema hawa tuliokuwa tunawatumikia hawatujali tena, tunaowakimbilia wanasema tuliwahi kuwaumizi hivyo nao wamepata fursa… mimi naomba upendo uwepo. Tuthaminiane muda wote sawa na tunapokuwa kazini,” anasema.

Sitanii, meseji na simu ni nyingi kiasi kwamba ujumbe wa askari wote walionipigia hata gazeti unaweza kulijaza. Naamini kwa watu hawa waliostaafu mwaka 2011 na kuendelea ambao wanadai kati ya Sh milioni 1.7 hadi milioni 6, kulingana na umbali wa nyumbani kwa askari husika serikali inao uwezo wa kuwalipa mafao yao.

Ombi langu la kiungwana kabisa ni moja, serikali iwalipe askari hawa wanaoteseka. Pili, askari nao wajifunze kuwa ipo siku watastaafu. Wahudumie kwa staha wateja wao wa ndani (askari wenzao) na raia. 

Hivi kwani askari akikuamkia kama unamzidi umri akasema shikamoo, uaskari wake unakwisha? Hivi kwani ni lazima askari watumie ubabe unaowafuata hata wanapokuwa wamestaafu?

Hatuoni nchi za wenzetu hata Urusi, mtuhumiwa akikamatwa anaruhusiwa ambusu mpenzi wake kwanza, kisha anakaribishwa kuingia kwenye gari la polisi? 

Kwani sisi hatuwezi kufikia kiwango hiki cha huduma kwa wateja? Serikali iwalipe askari hawa, ila nao wajifunze kuishi na watu.