Juma lililopita, asasi isiyo ya kiserikali – Afrika Mashariki Fest,
ilikutanisha wana wa Afrika Mashariki jijini Kampala, Uganda na kutambua mchango wa viongozi waliotangulia katika kuanzisha na kujenga umoja wa nchi za Afrika Mashariki – Kenya, Uganda na Tanzania – zilizounda Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Pamoja na Mzee Jomo Kenyatta wa Kenya, na Dk. Milton Obote wa Uganda, Mwalimu Nyerere naye alitunukiwa tuzo ya ‘Uzalendo’ ambayo niliipokea kwa niaba yake.
Historia inatufundisha kuwa siyo uamuzi wote mzuri hufanikiwa. Nia ya kuendeleza Jumuiya iliambatana na matatizo mengi, ikawa ni chanzo cha kutoelewana kati ya wanachama wake, au labda tuseme, kati ya mitazamo tofauti ya baadhi ya viongozi wake katika masuala ya siasa na uchumi.
Na siyo ajabu kuwa moja ya sababu za msingi zilizosababisha
kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ilikuwa viwango tofauti ya maendeleo ya uchumi ambavyo vilikuwa vimefikiwa na nchi wanachama.
Kenya, zaidi ya Uganda na Tanzania, ilikuwa na maendeleo makubwa zaidi ya uchumi na ilikuwa inafaidika kwa kuuza bidhaa zake kwa wanachama wenzake. Na katika nafasi yake hiyo ya nguvu kubwa ya kiuchumi zaidi ya wanachama wenzake, serikali ya Kenya ilikuwa inadai kupewa nafasi nyingi zaidi katika vyombo vya uamuzi vya Jumuiya.
Tofauti za siasa za kibepari za Kenya na za Ujamaa nchini Tanzania, nazo zilikuwa chachu ya kuimarisha tofauti kati ya viongozi na serikali za nchi hizo. Uganda nayo, wakati ule ikiwa chini ya Idi Amin Dada, ilikuwa na malalamiko dhidi ya Tanzania kwa kusaidia waasi waliokuwa wanaipinga serikali ya Uganda, na ambao walikuwa wanaendesha harakati hizo kutoka ardhi ya Tanzania.
Hali ya maendeleo ya uchumi ya Kenya dhidi ya wanachama wengine wa Jumuiya, bado iko vile vile. Ukichukulia, kwa mfano, biashara kati ya wanachama wawili mwaka 2011 Kenya iliiuzia Tanzania bidhaa zenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 488, wakati Tanzania iliiuzia Kenya bidhaa zenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 390.
Uamuzi wa kuunda Jumuiya ya Afrika Mashariki ulileta manufaa mengi. Nchi wanachama ziliweza kushirikiana kugharamia huduma za pamoja, na ujenzi wa miundombinu. Kwa mfano, kabla ya kuvunjika kwa Jumuiya mwaka 1967 nchi wanachama zilikuwa zina mashirika mengi ya pamoja, ikiwa ni pamoja na shirika moja la ndege, East African Airways.
Leo, kila nchi inahangaika kuwekeza kwenye shirika lake la ndege. Kenya inaelekea kuwa imepata mafanikio makubwa zaidi kwenye eneo hilo ingawa Kenya Airways inakumbwa na hasara za uendeshaji. Shirika la Ndege la Tanzania ni kama halipo ingawa jitihada zinafanyika kulihuisha. Shirika la Ndege la Uganda halipo kabisa.
Faida nyingine ni kuwa wakati huo, Jumuiya ilitoa fursa kwa nchi zake wanachama kufikia uamuzi wa pamoja na kutoa kauli ya pamoja na yenye nguvu zaidi ya kisiasa kwenye hadhira mbalimbali za kimataifa.
Faida kubwa kwa wazalishaji ni kuwapo kwa soko kubwa la pamoja. Soko la sasa la nchi wanachama za Jumuiya Afrika Mashariki linakadiriwa kuwa na watu milioni 146. Faida kwa mzalishaji kuwa na soko kubwa ni kupunguza gharama zake kwa sababu ya kuhudumia soko kubwa zaidi, na hivyo kumwezesha kupunguza bei za huduma na bidhaa kwa wateja.
Gharama za msingi za kujenga kiwanda cha vibiriti kwa watu milioni moja ni zile zile kulinganisha na kujenga kiwanda hicho kwa watu milioni 100. Lakini uhakika wa kuuza vibiriti kwa watu milioni 100 unaweka bidhaa kwenye soko na soko kubwa linaongeza fursa ya mauzo na kupunguza uwezekano wa uwekezaji kutozaa matunda.
Mwekezaji anapokuwa na uhakika wa kurudisha pesa yake anakuja hana umuhimu wa kutafuta faida kubwa sana na ukweli huu unaweza kusababisha asitoze bei za juu. Mwishowe inatarajiwa kuwa faida kubwa ya soko kubwa ni bei nafuu kwa wateja.
Uzoefu unatufundisha pia kuwa mjenzi anapogundua ufa kwenye nyumba, haachi ujenzi. Na bila shaka ndiyo ikatokea wanachama wale wale waliokumbwa na matatizo ya kujaribu kujenga umoja wa kiuchumi na kisiasa miaka hiyo ya 1960, wakakutana tena na kuunda upya Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo ipo mpaka leo.
Anayejikwaa huwa kajiandaa vyema kutegemea kuwa penye kila njia vipo vikwazo na anakuwa mwenye uzoefu wa suluhisho la kumwepusha na vikwazo anavyokumbana navyo.
Waandaaji wa mkutano wa Kampala wamejipa pia jukumu la kuwakumbusha wana wa Afrika Mashariki umuhimu wa Jumuiya kwao.
Ni kazi ambayo inapaswa kwenda sambamba na kuwakumbuka na kuwaenzi waasisi wa Jumuiya. Kazi zote mbili zinastahili pongezi.