Wiki hii nafahamu kuwa kuna tukio la aina yake nchini. Ni kwa mantiki hiyo, nashindwa kuendelea na mada yangu ya gesi. Naomba niisogeze mbele kwa wiki moja. Yanayotokea ni ya mpito, ila Tanzania itabaki.
Leo ni siku ambayo Bunge Maalum la Katiba linakutana tena. Linakutana kujadili kwa siku 60 kama fursa ya mwisho juu ya hatima ya Katiba Mpya.
Nafahamu walikwishatumia siku 70 za awali, hawakuweza kujadili hata sura moja, leo wanazo siku 60 kujadili sura 17. Hakika kuna upungufu mkubwa mwingi kiasi kwamba rasimu hii hata ikipitishwa ilivyo, haitekelezeki. Niwie radhi msomaji angalau kwa aya chache niiguse Rasimu ya Katiba.
Sitanii, niseme mapema tu kuwa CCM hawana haki ya kupenyeza wayatakayo ndiyo yageuzwe maoni ya wananchi, na wala Chadema au Ukawa hawana haki ya kulazimisha Taifa hili kupitisha Katiba mbovu. Iitishwe kura ya maoni, wananchi waulizwe maswali mawili. Moja, Muungano mnautaka au hamuutaki? La pili, kama mnautaka uwe wa Serikali ngapi?
Swali langu la pili nimeliacha wazi kwa maana ni la kitakwimu zaidi, lakini lenye mantiki ndani yake. Tukienda na swali lenye kuohoji serikali moja, mbili au tatu, tutawakosesha fursa wenye hamu ya kuona Serikali nne ikiwamo ya Pemba, au tano na zaidi ikiwamo ya visiwa kama Ukerewe au Musira.
Kwa ufupi tu nisema ibara ya kwanza ya Rasimu ya Katiba ni tatizo. Inasema, “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Nchi na Shirikisho lenye mamlaka kamili ambalo limetokana na Muungano wa nchi mbili za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, ambazo kabla ya Hati ya Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964, zilikuwa nchi huru.”
Hapo peke yake kuna mgogoro. Nchi ni eneo la ardhi yenye mipaka inayotambulika, watu wanaoishi muda wote, serikali yenye jeshi na uwezo wa kusaini mikataba ya kimataifa. Hii ni kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Sheria za kimataifa pia zinatambua Shirikisho kama muungano wa mataifa au nchi kuanzia mbili na kuendelea. Kwa mfano, Marekani ina shirikisho lenye mataifa/majimbo 50.
Sitanii, Tanganyika inaweza kupewa haki ya kuwa taifa, Zanzibar ikapewa haki ya kuwa taifa na Tanzania ikabaki kama nchi kwa kuamua kisheria tu kuwa Tanzania ndiye mmiliki wa ardhi, watu (uraia), serikali yenye jeshi na uwezo wa kusaini mikataba ya kimataifa, hivyo kuifanya nchi ya Tanzania kuendelea kuwapo.
Haiwezekani kamwe, Taifa letu likawa nchi na wakati huo huo likawa shirikisho. Ibara hii ni mgogoro. Ni sawa na kusema ‘sina na nina mimba’ kwa wakati mmoja. Jibu sahihi ni ama una mimba au huna mimba. Kwa maana hiyo nchi ni nchi na shirikisho ni shirikisho, huwezi kuwa navyo vyote kwa wakati mmoja.
Tatizo hapa ni hofu. Baada ya tamko la Mizengo Pinda bungeni kuwa Zanzibar si nchi, hata Tume ya Marekabisho ya Katiba imeingia kwenye mkondo wa siasa kuwaridhisha Wazanzibari waliovunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2010 kutokana na uzembe wa walioapa kuilinda, sasa tunataka kuhalalisha uzembe huo kwa kuwaridhisha tukiwaita nchi washirika. Nasema hapana.
Ukitaka kujua rasimu hii ni kizungumkuti, ibara ya kwanza hiyo hiyo sehemu ndogo ya pili inapingana na sehemu ndogo ya kwanza. Sehemu hii inasema hivi: “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Shirikisho la kidemokrasia linalofuata mfumo wa vyama vingi vya siasa, usawa wa binadamu, kujitegemea, utawala wa sheria, kuheshimu haki za binadamu na lisilofungamana na dini.”
Ibara ya 1 (1) imesema “Tanzania ni Nchi na Shirikisho”. Ibara 1 (2) rasimu inasahau ilichokisema kwenye sehemu ya kwanza, inasema “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Shirikisho…” kwa maana nyingine walioandika rasimu hii wamesahau kuwa walisema kwenye ibara ndogo ya kwanza kuwa ni Nchi na Shirikisho, sasa ibara ya pili wanasema ni Shirikisho.
Sitanii, rasimu hii inampa mzigo Rais wa Tanzania asioweza kuubeba. Sura ya 2, Ibara ya 12 (2) inaitaka Serikali ya Tanzania kutoa taarifa bungeni juu ya shughuli za maendeleo ya nchi, wakati katika mambo ya Muungano, hakuna hata moja linalohusiana na maendeleo ya nchi kama elimu, afya, maji, rasilimali za nchi na mengine. Najiuliza, itatoleaje taarifa mambo yasiyo chini yake?
Ibara ya 65 (2) na (3) ya rasimu inasema: “(2) Bila ya kuathiri mipaka iliyowekwa na Katiba hii, kila Nchi Mshirika wa Muungano itakuwa na uwezo na uhuru wa kuanzisha mahusiano au ushirikiano na mambo yaliyo chini ya mamlaka yake kwa mujibu wa Katiba ya Nchi Mshirika wa Muungano.
“(3) Nchi Mshirika wa Muungano inaweza, wakati wa kutekeleza majukumu yake chini ya ibara ndogo ya (2), kuomba mashirikiano kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya kufanikisha mahusiano na jumuiya au taasisi ya kimataifa au kikanda, na Serikali ya Jamhuri ya Muungano inaweza kutoa ushirikiano kwa Nchi Mshirika wa Muungano kwa namna itakavyohijika.”
Sitanii, wala mimi sioni sababu ya kutumia njia ndefu kueleza jinsi ya kuvunja Muungano. Ibara hii ndiyo nguzo ya kuvunja Muungano. Neno ‘inaweza’ lililotumika wala haliibani nchi husika kulazimika kuishirikisha Serikali ya Muungano. Maana yake ni kwamba wawili hawa watatenda na mambo yatajulikana mbele ya safari.
Mfano, Tanzania ilijitoa COMESA, Tanganyika inaweza kuamua kuingia COMESA hakutakuwa na kizuizi, na hata isipoamua kushauriana na Tanzania wala halitakuwa kosa kikatiba. Hii ina maana kuwa Tanganyika na Zanzibar zinaweza kuomba uanachama wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika bila kizuizi ikiwapendeza kufanya hivyo.
Nasema kwa kuwa nchi hizi zitakuwa hazibanwi kisheria kuomba ridhaa ya Tanzania kabla ya kuingia uhusiano na jamii ya kimataifa, tutapata mgogoro usiopimika. Miaka miwili tu baada ya rasimu hii kupita, Tanganyika itaomba uanachama wa UN na AU bila kuishirikisha Tanzania, vivyo hivyo kwa Zanzibar.
Narudia, ikiwa tuna nia ya kuvunja Muungano wala hatupaswi kutumia njia ndefu. Twende kwa wananchi tuulize maswali mawili niliyosema hapo juu, ikiwa wenye matumaini kuwa Muungano utavunjika watashinda, basi itakuwa hivyo na ikiwa watashindwa, basi tutaendelea na Muungano.
Ibara ya 109 ya Rasimu inapendekeza kuanzishwa kwa Tume ya Ushirikiano. Inapendekezwa Mwenyekiti wa Tume hii awe Makamu wa Rais, ambayo wajumbe wake ni pamoja na Rais wa Tanganyika na Rais wa Zanzibar, lakini haizungumzi chochote juu ya Rais wa Muungano.
Kwa maana nyingine, rasimu hakuna mahala popote inapowalazimisha Rais wa Tanganyika na Rais wa Zanzibar kuwajibika kwa Rais wa Muungano wa Tanzania. Hii ina maana kuwa marais wa nchi hizi wakiamua kumkaidi Rais wa Muungano (Tanzania) hatakuwa na nguvu yoyote kikatiba kuwazuia wasifanye hivyo.
Upungufu upo mwingi katika rasimu hii, ila kwa kuwa nafasi inazidi kupungua nigusie suala la ardhi. Ardhi si moja kati ya mambo ya Muungano. Kwa mshangao, uraia linapendekezwa kuwa suala la Muungano wakati mtu hawezi kuwa raia wa nchi isiyo na ardhi.
Mwishoni mwa wiki nimesikiliza midahalo. Nimemsikiliza Tundu Lissu, na nimemsikiliza Profesa Patrick Otieno Lumumba kutoka Kenya. Wote walikuwa na hoja za msingi, ila Profesa Lumumba ameonya kuwa tuweke kando Ukawa, tuweke kando Tanzania Kwanza, tuifikirie Tanzania.
Profesa huyu amesema heshima ya Tanzania isiyo na ukabila, Tanzania isiyo na umajimbo wala migawanyiko ni kubwa. Ameeleza jambo lililonigusa akisema ikiwa mkondo wa kupigana vita unaoonekana kupigiwa chapuo unaweza kuepukwa, kwa nini twende huko?
Ametumia maneno kuwa hata tukiamua kuingia vitani sawa na zilivyofanya nchi nyingi za Afrika, bado tutarejea kwenye meza ya mazungumzo kwa nia ya kupata mwafaka na maridhiano. Ameshauri tuuepuke mkondo huu. Nasema, naungana na Profesa Lumumba.
Sitanii, Profesa Lumumba ameshauri Ukawa warejee bungeni, ila mimi nasema kurejea au kutorejea kwa Ukawa katika uhalisia wa mambo hakutasaidia. Tuchukue maneno ya Tundu Lissu kuwa mambo yameishaharibika. Tusitishe mchakato wa Katiba, turudi kwenye michoro tuondoe upungufu uliopo kisha tuandike Katiba mpya.
Hatuna sababu ya kuharakisha Katiba mpya, tukaishia kupata Katiba ‘feki’.
Ninachoamini tunaweza kudhani kuwa hili ni bao la kisigino kisiasa, lakini tukiipitisha rasimu ilivyo, itaivunja Tanzania na CCM wakifanya mambo yao wakaikarabati watakavyo, matokeo yake haitakuwa Katiba ya Tanzania bali ya CCM sawa na ilivyokuwa mwaka 1977.
Sitanii, tunachoweza kufanya sasa ni mambo mawili. Moja, kufanya marekebisho ya 15 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tukarekebisha yanayolalamikiwa kwa sasa. Pili tufanye uamuzi mgumu. Tusitishe mchakato wa Katiba, twende kwa wananchi tuwaulize iwapo Muungano wanautaka au hawautaki, na kama wanautaka wanataka Serikali ngapi?
Wiki ijayo, nitarejea kwenye mada yangu ya gesi, naomba usikose nakala yako ya JAMHURI.