Wiki iliyopita Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilitangaza mkakati mpya wa ukusanyaji mapato. Mkakati huu mpya ulitangazwa mbele ya Wahariri wa vyombo vya habari nchini siku ya Alhamisi. Mkutano huo ulimhusisha Mkurugenzi wa Elimu kwa Walipakodi, Richard Kayombo na Naibu Kamishna (Mapato ya Ndani), Jenerose Bateyunga.
Chini ya mpango huu TRA inaanzisha utaratibu mpya, ambapo kila mfanyabiashara aliyesajiliwa atalazimika kulipa kodi kwa utaratibu mpya. Mwanzoni wafanyabiashara wenye pato la wastani wa Sh milioni 40 kwa mwaka ndio waliokuwa wakisajiliwa kwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
Kundi hili la wafanyabiashara ndilo lililokuwa linatoa risiti kwa kutumia mashine ya kielektroniki (ETR). Utaratibu huu wa kutumia mashine za ETR ulianza mwaka 2010. Katika mwaka wa fedha wa 2010/2011 uliongeza mapato kwa asilimia 9.6. Mwaka 2011/2012 uliongeza mapato kwa asilimia 23.
Tangazo la TRA linasema kuanzia Mei 15mwaka huu wafanyabiashara wote wenye pato la wastani wa Sh milioni 14 kwa mwaka, waliokuwa wakitumia leseni za anwani ya biashara (business names) sasa watapaswa kutoa risiti kwa kutumia ETR badala ya kukadiriwa. Mpango huu utaingiza walipakodi wapya 200,000.
Sisi wa JAMHURI tulikwishaliona hili siku nyingi. Tulifika mahala tukaandaa mradi tunaoamini uko katika hatua za mwisho kwa ushirikiano na Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) kuona jinsi nchi yetu inavyoweza kupanua wigo wa kodi. Katika mradi huu tunapendekeza njia ya kupanua wigo wa kodi na tuko tayari kuwashirikisha TRA.
Tumekuwa tukisema kuwa Serikali yetu haiwezi kuendelea kutegemea wafadhili kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Tumekuwa tukisema kuwa wigo wa kodi ni mdogo na ndio maana kila kukicha Serikali inafikiria kuongeza kodi kwenye bia, soda, maji, sigara, ushuru wa magari na vinywaji vikali.
Zipo fedha nyingi zinazopita kwenye mikono ya watu bila kuandikiwa risiti. Vituo vya mafuta, maduka ya fedha (bureau de change), maduka ya kawaida, masoko (wanaojiita wamachinga) na sehemu mbalimbali wakilipa kodi kwa asilimia tano tu, nchi yetu itakuwa tajiri.
Tumekuwa tukitoa mfano wa baa kuwa mteja mmoja anatumia hadi 100,000 kwa siku lakini hapewi risiti. Matokeo yake wafanyabiashara wanazidi kutajirika huku wakiituhumu Serikali kuwa haitimizi wajibu wake wakati wao ndio wanakwepa kodi, ama kwa kujua, au kwa kutojua.
Sisi wa JAMHURI tunasema nchi zote zilizoendelea zinakusanya kila kodi kwa kila mauzo yanayofanyika. Tunasema tuko tayari kushirikiana na TRA na kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kulipa kodi kwa manufaa ya maendeleo ya taifa letu. Hongera TRA, hakikisha mnatumia kila mbinu Watanzania wachukue risiti kwa kila bidhaa wanayonunua, na kwa njia hiyo kodi zitaongezeka, taifa letu lipate maendeleo ya kasi.