Ninachukizwa sana na matamshi ya mara kwa mara kutoka kwa viongozi wakuu wa mataifa ya Magharibi. Hivi karibuni mkuu wa Marekani ametamka kuwa anaunga mkono ndoa za jinsi moja.
Sijui tu imekuwaje huku kwetu, jirani yetu huku Malawi, Mkuu wa nchi naye katamka kuunga mkono ndoa za jinsi moja. Katika historia ya mwanadamu tangu enzi za Adam na Hawa, muda wote wa kabla ya kuzaliwa Yesu Kristo na hata baada ya kuzaliwa kwake, haijapata kusikika ati kuna mahali au wakati fulani wanadamu wa jinsi moja wameoana.
Mapokeo yote ulimwenguni kwa karne na karne hakuna ndoa ya za watu wa jinsi moja kutokea wala kusikika. Wayahudi au Wazungu tangu kale wamekuwa na mapokeo ya maadili ya ndoa kwa maana ya muungano wa mtu mume na mtu mke ili kujenga au kuanzisha familia mpya ulimwenguni.
Waingereza ambao hawana Katiba iliyoandikwa rasmi, bali wanatumia ‘Mapokeo’ tu kutoka kizazi hadi kizazi, wametafsiri ndoa kama hivi, na nukuu “Marriage is a legally, socially sanctioned union between one (or more) husband (husbands) and one (or more) wife (wives) that accords status to their offspring and is regulated by laws, rules, customer, beliefs and attitudes that prescribe the rights and duties of partners” (taz. Encyclopedia Britannica vol. 14 uk. 926).
Maneno haya yangeweza kutafsiriwa kuwa “Ndoa ni muungano uliokubalika kisheria na kijamii kati ya mume (au wanaume) na mke (au wanawake) wenye dhamira ya kujenga familia (kuzaa watoto), na muungamo huo umewekwa kwa mujibu wa sheria, kanuni, mila na desturi, imani na hali mbalimbali na unaainisha haki, wajibu na majukumu ya kila mmoja katika muungano huo!”
Basi, kule Uingereza wanasema hivi nanukuu, “Marriage as understood in the Christian World means the lifelong union of one manand one woman to the exclusion of all others, such union being preceded by some form of ceremonial recognized by the law of the particular country in which it takes place” (Encyclopedia Britannica Vol. 14 uk. 931 – Law of Marriage).
Ndiyo kusema ndoa inavyoeleweka katika ulimwenguni wa Wakristu maana yake ni muungano wa maisha kati ya mume na mke bila kuhusisha watu wengine, na kwa kawaida inafanywa kwa sherehe mahususi zinazotambulika kisheria katika nchi husika.
Waingereza hao hao wanadai kuwa mapokeo yao ni ya muda mrefu tangu zamani za kale enzi za Wagiriki, Warumi, Wayahudi na mapokeo ya Ukristo ndipo ulimwengu wa sasa unaendeleza kuyaboresha kulingana na nyakati za sasa. Wanasema, nanukuu tena; “In the industrialized, urban culture of the contemporary Western World the type of organization most commonly established by marriage is the small nuclear family, consisting of a married couple and their children” (Encyclopedia Britannica vol. 14 uk. 928).
Hapa Wazungu wanakiri wazi wazi kuwa katika nchi zao za Magharibi kwenye viwanda na maisha ya mijini jumuiya ndogo kabisa ni mume na mke waliooana – pamoja na watoto wao – kwa maneno mengine tunasema jumuiya ndogo kabisa ni familia moja yenye baba, mama na watoto au tuite ni kaya moja.
Nimejikita sana kuelezea mtazamo wa ndoa kwa Uingereza kwa David Cameron, lakini je, huko Marekani kwa Barrack Obama, ndoa inaonekanaje?
Marekani kwa ujumla wao wameshika mapokeo yote ya Uingereza, tofauti ni kwamba Marekani kila jimbo lina sheria na kanuni zake (state civil marriages) kwa ujumla wao wanasema na nukuu; “The fundamental principle is simply that a man and a woman, each possessed of the requisite capacity may become married by mutual consent”
(Encyclopedia Britannica vol. 14 uk. 934).
The legal conception of marriage is the same as that described under English law.” Kimsingi, Marekani na Uingereza mtazamo wao wa ndoa ni kuwa za jinsi mbili tofauti, yaani mume na mke.
Aidha, nchi zote zinafuata maadili ya Ukristo katika suala la ndoa na katika nchi zote za Magharibi, zinakubali kuwa ndoa ndiyo msingi wa kujenga jumuiya katika dunia hii kwa maana baba, mama na watoto ndiyo chanzo cha kaya/familia/jumuiya ya mwanzo kabisa katika taifa lolote lile.
Kwa vile mapokeo yote waliyonayo Wazungu na Marekani hakuna popote linapoonekana pokeo la ndoa ya jinsi moja ambayo Cameron na Obama wanaibuka siku hizi na kudai kuwa hizo ni haki za binadamu, je, hizo haki za binadamu zinasemaje?
Mimi nikiwa Mwalimu kijana kabisa pale Abbey School Ndanda mwaka 1956, nililetewa kijitabu chenye hizo haki za binadamu kutoka idara ya Serikali iliyoitwa Department of Public Information niwaeleze wanafunzi wa shule kinaganaga juu ya tamko la Baraza la Umoja wa Mataifa juu ya Haki za binadamu wote.
Kijitabu kile kina kichwa cha habari kisomekacho:-
“Universal Declaration of Human Rights”
Final authorized text
United Nations
Department of Public Information
Kimechapisha na The Tanganyika Standard, Dar es Salaam yapo maneno juu ya hilo jalada yanasomeka hivi:-
“On December 10, 1948, the General Assembly of the United Nations adopted and proclaimed the Universal Declaration of Human Rights the full text of which appears in the following pages.
Following this historic act, the Assembly called upon all member countries to publicize the text of the declaration and “to cause it to be disseminated, displayed, read and expounded principally in schools and other educational institutions without distinction based on the political status of countries or territories.”
Kwa maagizo hayo nilipewa jukumu la kupita kwenye middle schools za Jimbo Katoliki la Ndanda (nazo zilikuwa Lukuledi, Nyangao, Mnero na Kitangali bila kusahau shule yangu ya Sekondari ya Abbey Ndanda), kuelezea hizo haki za binadamu zilizotangazwa na Umoja wa Mataifa.
Miongoni mwa haki zile kipo kifungu kinachohusu ‘Ndoa’ na kinasema hivi, nanukuu:-Article 16(1) Men and women of full age, without any limitation due to race, nationality or religion, have the right to marry and to found a family. They are entitled to equal rights as to marriage, during marriage and at its dissolution.
(2) Marriage shall be entered into only with the free and full consent of the intending spouses.
(3) The family is the natural and fundamental group unit of society and is entitled to protection by society and state.
Kwa upande wa ndoa, haki za binadamu zilizotangazwa na Umoja wa Mataifa Desemba 1948 zinatamka hayo.
Sielewi Wazungu wanapotuletea hoja ya ndoa za jinsi moja eti kwa kuheshimu na kutambua haki za binadamu ni vifungu gani hivyo na viliongezwa lini? Wote – Cameron na Obama – zilipokuwa zinatangazwa haki hizi hawakuwapo katika dunia hii (mimi nilikuwapo) na Rais wa Marekani alikuwa Harry Trueman, na Uingereza Waziri Mkuu alikuwa Clement Richard Attlee (Labour), ndiyo walioshiriki kuandaa hizi haki za binadamu.
Huu ushoga na ndoa za jinsi moja wanazotuelezea hawa viongozi vijana wa sasa zina msingi gani katika mapokeo yao? Wote hawa wanaishi nchi za Kikristo (Western Christian countries) wanakofuata Biblia. Vionjo vyao vinategemezwa wapi katika kitabu chetu kitakatifu? Tangu mwanzo wa uumbaji, Mwenyezi Mungu aliumba mtu mume na mtu mke.
Isitoshe Mungu alitoa agizo, “zaeni mkaongezeke mkaijaze nchi na mkaitiishe (Mwa. 2:28)” na Mwenyezi Mungu akatuonya kutunza heshima ya ndoa pale aposema “Usilale na mwanamume mfano wa kulala na mwanamke ni machukizo” (Wal. 18:22). Sasa maongozi yote haya kutoka kwa Mwenyezi Mungu bado binadamu anathubutu kufurahia kutangaza ndoa za jinsi moja kweli?
Kama si kufilisika kimaadili na kuonyesha uozo wa ustaarabu wa Wazungu tutaitaje mambo namna hiyo? Hata kwa akili za kawaida tu si lazima usome Havard au Oxbridge (Oxford au Cambridge) kule Uingereza, mtu uwe na vionjo vya asilia tu kama wanyama wengine ambapo beberu au jogoo aslani hampandi beberu mwenziwe wala jogoo mweziwe, seuze sisi binadamu? Huku ni kuporomoka sana kwa ustaarabu wa Magharibi.
Dini zote zinazungumzia ndoa ya jinsi mbili tofauti. Baiolojia inathibitisha kuendeleza (propagation of any species) uhai wa kiumbe chenye uhai jinsi mbili tofauti, zinahitajika na hata katika madini kupata nguvu ya mvutano wa kukaribiana (attraction) ncha mbili za jinsi tofauti zinahitajika.
Katika zile hesabu za maumbo (geometry) tukilinganisha hivyo tuliweza kumalizia kwa maneno QED (kilatini quod errand demostrandum) kuonyesha urahisi wa kufikia jawabu la kisayansi za kimahesabu. Hawa Wazungu hawalijui hilo?
Watanzania wenzangu, uozo huu wa Wazungu na Marekani ukataliwe katakata katika Taifa hili lenye maadili mazuri sana ya Kibantu. Ndoa ni za jinsi mbili tofauti duniani tangu kuumbwa kwa Adam na Hawa, hadi karne hii ya 21 hapajawahi kutokea au kusikika kuwapo kwa ndoa za jinsi moja katika ulimwengu.
Haya tunayasikia kutoka kwa Wakristo wa mataifa makubwa na tajiri kama Uingereza ambako ninaamini Cameron ni Mkristo na alifunga ndoa yake na mke mmoja anayeishi naye na wana familia – tuyapuuze kabisa na tusiyapokee hapa Taznzania.
Katika nchi yetu tunazo ndoa za aina mbili tu. Nazo ni ndoa ya mke/mume mmoja na ndoa ya mume mmoja na wake zaidi ya mmoja. Ndoa zote hizi zina mlolongo wake wa kuzihitimisha. Ndoa zinafungwa kadiri ya madhehebu ya wahusika.
* Ndoa za Kiislamu zinafungwa mbele ya sheikh/imamu.
* Ndoa za Kikristo zinafungwa mbele ya padri/mchungaji.
* Ndoa za Kiserikali zinafungwa kwa Afisa Utawala Wilaya husika (Bomani) kwa mujibu wa Sheria ya Ndoa ya Tanzania ya mwaka 1971.4.
* Ndoa za kimila/asili/kipagani – kadiri ya mila na desturi za makabila mbalimbali.
Kutokana na aina hizo za ndoa, haingii akilini mwa mtu yeyote wa kawaida kufikiria juu ya ndoa za jinsi moja. Kwa maelezo ya hapa zinaingia wapi? Zinafungwa mbele ya nani? Kwa sheria ipi? Utamaduni huo wa ndoa za jinsi moja katika Taifa hili na katika nchi kama Tanzania, hauwezi kukubalika maana haupo kimila, kidini wala kiserikali.
Tumwombe sana Mwenyezi Mungu aepushe balaa hili la uozo wa ustaarabu wa Wazungu. Tunasema asante kwa kuteletea Dini ya Mungu yenye kutekeleza agizo lake la kuoana mtu mume na mtu mke, na si vinginevyo.
Tanzania tuna maadili yetu mema ya kuamini uhuru wa kuabudu kila mmoja kwa imani yake, lakini ‘ushoga na ndoa za jinsi moja hatukubali asilani’, hatupokei na tusiletewe mila na desturi mbovu za matajiri Wazungu. Tuna utamaduni wetu na tutaishi nao kama walivyotukuta nao.
Mungu ibariki Tanzania, dumisha Uhuru na umoja wetu.
Francis Mbenna ni Brigedia Jenerali mstafuu. Anapatikana kwa simu 0715 806758. Alikuwa pia mwalimu wa shule za sekondari. Ni mwanahistoria na ameandika kitabu cha Historia ya Elimu Tanzania kutoka 1892 hadi sasa (Dar es Salaam University Bookshop.