Mara kadhaa nimepata kumsikia Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli, akisema nchi yetu ni tajiri wakati wananchi wake ni maskini. Nchi hii imetunukiwa maliasili nyingi na Mwenyezi Mungu lakini watu wachache wametuchezea mno katika kupora mali zetu.

Kauli hii inapambwa na maelezo yasemayo: “Mali hizo zingetuwezesha kuwa matajiri kama tusingechezewa na watu fulani wakiwemo ndugu zetu. Watu hawa ndio waliotufikisha hapa tulipo. Ndugu zangu, tumepigwa mno.”

Anaendelea kusema: “Sisi si watu wa kuhangaika kuomba omba misaada kutoka nchi nyingine. Wakati tunaweza kuwa nchi ya kutoa misaada (a donor country) kwa nchi nyingine. Lakini tumefikishwa hapa tulipo na ndugu zetu waliokubali kutusaliti na kuhujumu uchumi wetu.”

Rais Magufuli anasema: “Ndugu zangu huo ndiyo ukweli. Nami sitaacha kusema ukweli, kwani msema ukweli ni mpenzi wa Mungu.” Mwisho wa nukuu. Kauli na mapambo haya na mengineyo, yamepata kurindima masikioni mwa Watanzania mara kwa mara.

Rais anazungumzia mali tulizonazo kama vile ardhi yenye rutuba na mboji, mito, maziwa na bahari. Misitu na mbuga za hifadhi. Anatukumbusha pia kuna viumbe; ndege na wanyama. Hajasahau madini, gesi na mafuta, vyote vinapatikana nchini.

Kwa mfano, tunazo almasi, dhahabu, tanzanite, shaba, fedha, bati na jasi. Mabonde ya Kilombero na Rufiji, maziwa ya Nyanza na Tanganyika. Ndege mbuni na korongo. Wanyamapori: twiga, simba, nyumbu na wengine wengi. Jambo la kujiuliza, vipi tunakuwa maskini ilhali tuna mali kedekede?

Ni wazi zipo kasoro katika maeneo ya kulinda, kutunza na kutumia mali zetu. Inawezekana ulinzi wetu si madhubuti, utunzaji wa mali si murua na matumizi yetu hayana kumbukumbu. Kama hivi ndivyo, mali itapotea bila kujulikana, na tutaendelea kuwa maskini.

Naamini Watanzania tunamwelewa Rais wetu Magufuli. Hoja iliyo mbele yetu, tunafanya nini kuishinda hali hii ya umaskini na kuikamata hali ya utajiri? Tukumbuke wahenga wanasema: “Umaskini umeachwa na utajiri hatua moja.”

“Tumefikishwa hapa ndugu zangu na wenzetu ambao hawana uzalendo.” Ni kauli ya Rais, Dk. John Pombe Magufuli.  Kauli hii bado inagonga vichwa vya Watanzania wengi. Je, tufanye nini na hawa ambao uzalendo ni kama mkuki moyoni? Wenzetu upande wa madini wameanza kuona njia.

Wiki iliyopita wadau, wachimbaji wadogo na wafanyabiashara wa madini walikutana Dar es Salaam na kuzungumzia mafanikio, matatizo na changamoto zilizopo katika sekta ya madini. Mengi yamezungumzwa kuhusu upatikanaji, uchimbaji, utunzaji, usafirishaji na uuzaji wa madini.

Mazungumzo na majibu yaliyotolewa yamethibitisha kilio cha Rais Magufuli ya tumechezewa sana katika mali na maliasili zetu. Mkutano umetoka na maazimio na mapendekezo ya kurekebisha na kuboresha utendaji kazi, na kukusanya mapato zaidi na kuziba mianya ya wizi na utoroshaji wa madini.

Sitarajii tena kusikia maelezo kuhusu kufichwa madini ndani ya tikitimaji, maofisa madini kufanya puuzo katika kuangalia madini. Polisi hawatahifadhi watuhumiwa wa wizi wa madini, Benki Kuu ya Tanzania haitasita kununua na kuhifadhi dhahabu, TRA haitazubaa kuweka ushuru na tozo nafuu kwa wachimbaji na wauzaji wa madini. Wadau kamwe hawatanunua madini kwa magendo.

Hii ni sehemu moja tu kati ya sehemu nyingi zinazohujumu uchumi wetu kukua mithili ya mnazi badala ya mgomba. Wadau wa madini wamethubutu kusema ukweli, kukiri makosa na kuamua kufanya kazi yenye tija na mafanikio. Haya ni mapinduzi chini ya uzalendo. Kumbe inawezekana.

Wadau wa madini wamethubutu na wameweza angalau kututia moyo wa kuondoa umaskini. Je, maeneo ya wanyamapori, misitu, gesi na mafuta na kadhalika mnasemaje? Tunahitaji na nyinyi mthubutu na kufanya kazi kwa weledi. Tukumbuke hatuna ‘wajomba’ nje ya nchi yetu. Uzalendo ni jibu.