Na Mwandishi Maalum
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk Hussein Ali Mwinyi ametoa wito kwa Waumini wa Dini ya Kiislamu kuutumia muda vema wakati huu wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa kufanya mambo mema yenye tija kwani kufanya hivyo ni kuuishi Uislamu.
Rais Dk Mwinyi amesema hayo alipozungumza na Waumini wa Dini ya Kiislamu wa Masjid Rahman uliopo Mfenesini alipojumuika katika Mashindano ya Kuhifadhi Quraan.

Ameeleza kuwa utaratibu wa kuhifadhi Quraan kwa vijana ni mzuri kwani unasaidia kuwaandaa Masheikh na Maimamu pamoja na wanazuoni wa baadae jambo linalopaswa kuendelezwa kwa mchango wa kila Muislamu.
Alhaj Dk Mwinyi ametoa rai kwa wafadhili waliopo kuongeza mchango wao na wengine wapya kujitokeza kuunga mkono juhudi za Taasisi za Kiislamu za kuandaa Mashindano ya Kuhifadhi Quraan kila mwaka.

Amefahamisha kuwa utaratibu huo ukidumishwa vijana wengi zaidi watahifadhi Quraan na ni njia bora ya kuwajengea uwezo wa kuishi kiimani.
Alhaj Dk Mwinyi amewasisitiza waumini hao umuhimu wa kuwa wamoja kwa mambo ya maendeleo, amani ya Nchi na mshikamano wa Waislamu.

Kwa upande mwingine, Rais Dk Mwinyi amesema waumini wa Dini ya Kiislamu wana wajibu wa kuzisaidia Taasisi za Kiislamu ili ziweze kutekeleza mambo ya heri kwa manufaa ya Uislamu.