Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Dar

SHERIA ya habari ya mwaka 2016 ilianza kulalamikiwa kwa kipindi kirefu na wadau wa habari kwa kuwa haikuondoa mitego iliyowekwa na sheria ya mwaka 1979 na kuchangia kudumaa kwa vyombo vya habari nchini.

Hayo yamesemwa leo na Neville Meena ambaye ni mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),Septemba 13, 2022 wakati akizungumza katika Kipindi cha Front Page kinachorushwa na Radio +255 Global jijini Dar es Salaam.

Meena amesema kuwa sheria hiyo ilianza kupigiwa kelele kwa muda mrefu na wadau wa habari ambapo Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan iliona haja ya kukaa meza moja na wadau wa habari ili kuipatia ufumbuzi.

Amesema, hatua za awali alizochukua Rais Samia Suluhu Hassan,ziliongeza ari ya wadau wa habari kushirikiana ili kung’oa vipengele hasi vya sheria ya habari.

‘‘Hatua zilianza kuchukuliwa kwa serikali kuleta mapendekezo ya maeneo ya kurekebisha, lakini na sisi tuliongeza yetu ambayo wao walikuwa hawajaweka kwenye mapendekezo yao kwa kuwa mabadiliko hayo yalianzia kipengele cha 38.

“Sheria ya Habari ya Mwaka 1976, imefanya kazi kwa miaka 40, muda wote huo imetoa mwanya kwa mtu mmoja (waziri) kufungia chombo cha habari anapojisikia kufanya hivyo.

“Hata Sheria ya Habari ya Mwaka 2016 ilipotungwa, imefuata mkondo huo huo wa kutoa mamlaka kwa mtu mmoja kuamua kufungia chombo cha habari ama la ingawa mamlaka hayo amepewa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Malelezo.Katika mabadiliko haya, tumeiomba serikali iondoe kipengele hicho,’’amesema Meena.

Hata hivyo Mei 2,202 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan alielekeza Sheria za Habari ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kubinya uhuru vya vyombo vya habari nchini zirekebishwe.

Rais Samia alitoa maelekezo hayo wakati akiwahutubia Wadau wa Vyombo vya Habari kwenye maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari
ikiongozwa na kauli mbiu ‘Uandishi wa habari na changamoto za kidigiti’katika ukumbi wa Gran Melia Hotel jijini Arusha.

“Nimeelekeza Sheria zirekebishwe, lakini kwa majadiliano pande zote na si tu kwamba sisi tunataka nini. Nimemwelekeza Waziri sheria za habari zirekebishwe kwa kushirikisha wadau wote,”aliagiza Rais Samia

Naye Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye wakati akihojiwa na BBC alisema kuwa,wanaingia hatua ya pili na wadau wa habari ili pale ambapo hawakukubaliana waweze kujadili kupata mwafaka kwa hatua zaidi.

“Nimeletewa ripoti ya majadiliano yale, tunakwenda hatua ya pili sasa kule ambako walishindwa kukubaliana, tunataka tuongeze kikao kingine tukajadili yale tu ambayo hatukukubaliana.

Lakini, niwahakikishie wadau wa habari kwamba, hatutaenda bungeni bila kukubaliana,lazima tukae tukubaliane, tushauriane tufikie mwisho,”.

“Hatutaki kutunga sheria kesho na kesho kutwa tukarudi tena kwenda kurekebisha, na ndiyo maagizo ya Mheshimiwa Rais Samia (Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan) kwamba tukae tuzungumze, tujadiliane mpaka tukubaliane