Serikali imesema inawasiliana kwa mara ya mwisho na serikali za Afrika Kusini na Malawi ziruhusu mazao ya Tanzania yaingie katika nchi hizo.
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kupitia akaunti yake katika mtandao wa kijamii wa X ameeleza wamepokea taarifa kuwa Malawi imezuia mazao kuingia nchini kwao.
Bashe alisema uamuzi huo umesababisha wafanyabiashara wa Tanzania wakwame kuingiza mizigo katika nchi hiyo. Alitaja mazao hayo ni unga, mchele, tangawizi na ndizi.
Advertisement
“Vilevile wamezuia mahindi kutoka Tanzania kuingia kwao,” alieleza jana. Aidha, Bashe alieleza kuwa kwa miaka mitano serikali imekuwa ikifanya jitihada kufungua soko la ndizi Afrika Kusini bila mafanikio.
“Inatukumbusha jinsi pia, tulivyohangaika kwa miaka 10 kufungua soko la zao la parachichi mpaka pale tulipoamua kutaka kuzuia mazao yao kuingia kwetu tunaona mwelekeo ni uleule,” alieleza Bashe.
Alieleza kuwa hadi kufikia Jumatano ijayo kama nchi hizo zitakuwa hazijaruhusu mazao ya wafanyabiashara wa Tanzania yaingie huko Wizara ya Kilimo itazuia mazao yote ya kilimo na bidhaa zote za kilimo kutoka Afrika Kusini na Malawi.
“Aidha, hatutaruhusu zao lolote kutoka nchi hizi mbili kupita ndani ya nchi yetu iwe kwenda Bandari ya Dar es Salaam au nchi nyingine yoyote kama tulivyofanya mwaka jana hadi wakatufungulia”.
Aliongeza: “Na pia kwakua tumekua tukiwauzia mbolea, tutazuia mbolea kwenda Malawi, kwa hiyo natoa notisi hii kama kuna wafanyabiashara wa Kitanzania wana mizigo ya kwenda Malawi kuanzia wiki ijayo kama watakua hawajabadilisha msimamo wasipakie chochote”.
Bashe alieleza kuwa notisi hiyo itaanza kutekelezwa kuanzia Jumatano wiki ijayo kama serikali isipopata mrejesho kutoka kwao.
“Ifahamike kwamba kama, Waziri mwenye dhamana nimefanya jitihada zote za kuwasiliana na Waziri wa Kilimo wa Malawi bila kupata majibu yoyote,” alisema.
