Juma lililopita Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza uamuzi wa serikali yake kuhamisha ubalozi wa nchi hiyo Tel Aviv kwenda Jerusalem. Ni hatua inayotokana na tamko kuwa serikali yake imetambua rasmi kuwa Jerusalem ni makao makuu ya Israel.

Ni hatua inayochochea kudhoofika kwa jitihada za Wapalestina za kutafuta haki wanayoisaka tangu mwaka 1947.

Kwa upande mmoja, unaweza kusema kuwa Rais Trump ni muungwana anayetekeleza tu ahadi ya kampeni zake za kuwania urais ambako aliahidi wapigakura kuwa akichaguliwa atahamisha ubalozi wa Marekani nchini Israel kutoka Tel Aviv kwenda Jerusalem. Matokeo ya uamuzi wake hayana uungwana hata chembe.

Trump ameamua kutekeleza uamuzi wa azimio la Bunge la Marekani lililopitishwa mwaka 1995, wakati huo Bill Clinton akiwa rais wa nchi hiyo. Marais wa Marekani, kuanzia Clinton mwenyewe, George Bush, na Barack Obama wote wamekuwa wakikwepa kutekeleza uamuzi huo wa Bunge kwa mamlaka aliyonayo rais.

Trump amefafanua kuwa maslahi ya Marekani yatalindwa zaidi iwapo ubalozi wa Marekani utahamishiwa Jerusalem.

Na tumpe sifa Trump kwa hili pia; kwamba uamuzi wake kama rais umekuwa ukiongozwa na kuweka mbele maslahi ya nchi yake. Matatizo mengine hayamhusu sana. Amejaribu kuwahimiza viongozi mbalimbali ulimwenguni pia kuongozwa na kanuni hiyo.

Kwa sababu moja ya msingi, uamuzi huo wa kuendekeza kanuni hiyo kwenye uhusiano wa kimataifa ni suala linaloleta hasara zaidi kuliko manufaa kwa sababu linapingana na umuhimu wa kufikia maridhiano kwa pande zote katika masuala ya uhusiano wa kimataifa.

Na msingi wa maridhiano haya ni uamuzi wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 1947 wa kuunda “taifa la Kiarabu” na “taifa la Kiyahudi” katika eneo ambalo sasa hivi ni sehemu kubwa ya Israel kwa kutambua tofauti zilizokuwapo kati ya makundi hayo miwili.

Taifa la Kiyahudi liliundwa, lakini “taifa la Kiarabu” halijaundwa mpaka leo kwa sababu mataifa makubwa yameendelea kupuuza mahitaji ya Wapalestina na kuendelea kuunga mkono matakwa ya Israel.

Tangu enzi hizo mazungumzo ya kutafuta suluhisho la tatizo la Palestina yanakumbana na hatua ambazo hazileti ahueni yoyote kwa Wapalestina, bali kujenga mazingira ya serikali ya Israel kuendelea kukiuka uamuzi wote muhimu wa kimataifa wenye kujaribu kumaliza tatizo hili.

Na tatizo la kuendelea kukosekana kwa taifa la Palestina limezua majanga makubwa. Zaidi ya Wapalestina milioni 7 wametapakaa katika maeneo mbalimbali ya ulimwengu. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, inakadiriwa kuwa Wapalestina zaidi ya milioni 1.26 hawana uhakika wa kupata chakula cha kutosha.

Uamuzi wa Rais Trump kutambua Jerusalem kama makao makuu ya Israel ni uamuzi ambao unagusa suala la msingi kabisa katika mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina.

Pande zote mbili zimekuwa zikidai Jerusalem iwe makao ya pande hizo kinzani, katika kutafuta suluhisho la kuwepo kwa taifa la Palestina. Israel ilifanikiwa kuteka eneo la Jerusalem ya mashariki na kuliweka chini ya mamlaka yake, lakini mamlaka za kimataifa hazitambui uhalali wa Israel kukalia eneo hilo.

Serikali ya Marekani, pamoja na Umoja wa Mataifa, Russia, na Umoja wa Ulaya wamekuwa wasimamizi wakuu wa mazungumzo yanayokusudia kumaliza mgogoro uliopo kati ya Israel na Palestina.

Lakini uamuzi huu wa Rais Trump unapunguza imani yoyote ambayo Wapalestina walikuwa nayo juu ya nia njema ya Marekani ya kusimamia mazungumzo ya kumaliza tatizo la Wapalestina.

Hatua hii ya Trump haina tofauti na hakimu anayesikiliza kesi ya ardhi baina ya watu wawili kupangishwa chumba nyumbani kwa mlalamikiwa wakati kesi ikiendelea. Wapalestina wana kila haki ya kukasirishwa na tukio hili.

Lakini hiyo haitoshi. Ulimwengu mzima ungepaswa kulaani hatua hii ya Marekani ambayo matokeo yake yatakuwa kudhoofisha hatua za kumaliza mgogoro unaowakabili Wapalestina tangu mwaka 1947, na kuzidi kuongeza hatua za Israel za kupuuzia hatua zinazokusudia kufikia muafaka.

Hatua hii ya Rais Trump ingeshutumiwa zaidi katika miaka ya 1960 kuliko sasa. Israel imepiga hatua kubwa ya kujenga uhusiano kidiplomasia na kiuchumi na nchi za Afrika, ikiwa ni pamoja na kutafuta uanachama kwenye Umoja wa Afrika.

Serikali yetu ya Awamu ya Kwanza ilivunja uhusiano wa kidiplomasia na serikali ya Israel baada ya nchi hiyo kuteka maeneo ya Misri, Jordan, na Syria baada ya vita yake dhidi ya nchi hizo ya mwaka 1973. Katika vita kadhaa tangu mwaka 1948 Israel imekuwa ikimega maeneo yaliyokuwa yakikaliwa na Waarabu na kuyaweka chini ya himaya yake, kinyume cha uamuzi wa Umoja wa Mataifa.

Mwalimu Nyerere, akifafanua sera ya nje ya serikali yake mwaka 1973, alisisitiza umuhimu wa kuitambua Israel kama taifa, lakini alisisitiza pia umuhimu wa Israel kutambua kuwa haiwezi kuendelea kukalia kwa mabavu maeneo ambayo iliyateka na kutegemea kuwa waliopokonywa ardhi walazimike kutambua uwepo wa Israel.

Kutokana na msimamo huu Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza ya Bara la Afrika kuruhusu Chama cha Ukombozi cha Palestina kufungua ubalozi mjini Dar es Salaam.

Wanaotazama mgogoro wa Palestina na Israel kwa misingi ya dini wanajizuia kubaini tatizo pana zaidi lililopo. Wapalestina wanatafuta haki ya kurudi kuishi kwenye maeneo waliyopokonywa kwa mabavu. Wanatafuta haki ya kuthaminiwa kama wanadamu. Wanatafuta haki ya kuishi kwa amani.

Tukiyakumbuka haya hatutasahau jitihada ya Wapalestina ya kupata haki na hatutasahau kuunga mkono jitihada hizo.