Na Deodatus Balile

Mwaka 2021 unaomalizika umekuwa na matukio makubwa yasiyosahaulika katika historia ya taifa la Tanzania, jumuiya mbalimbali na familia kwa ujumla. 

Sitatenda haki nisipowataja watu wanne ambao wamefariki dunia bila kutarajiwa. Katika ngazi ya kitaifa, ni Rais John Magufuli. Hakuna aliyetarajia kuwa mwangwi wa sauti yake ungezimika ghafla kivile. Mungu amlaze mahala pema peponi.

Sitanii, sauti ya Magufuli ilifika mahala ikafahamika hata kwa watoto, bila kumwangalia kwenye TV. Ndiyo, pamoja na machache nitakayoyagusia, lakini angalau nianze na mazuri. 

Eneo la ujenzi, katika uongozi wake amelitendea haki. Atabaki katika historia kuwa ndiye aliyefanya uamuzi wa kuanza ujenzi wa Reli ya Kisasa (Standard Gauge).

Yeye amejenga reli yenye kasi ya kilomita 160 kwa saa, lakini kwa tuliopata fursa ya kusafiri nje ya nchi, tunafahamu kuwa China kwa sasa wanatumia teknolojia ya ‘magneto’ kuendesha treni za umeme, ambazo baadhi zinatembea kasi ya kilomita 650 kwa saa. 

Nyingi zenye teknolojia kama hii tunayoijenga, zinatembea wastani wa kilomita 480 kwa saa. Sisimuliwi, bali nimeipanda treni ya mwendo huu kutoka Guangzhou kwenda Beijing kilomita 2,409 mwaka 2018 tulitumia saa 6, hivyo kasi hii nimeishuhudia. Tuelekeee huko.

Kwa ukanda wetu, treni ya umeme ni mgodi unaotembea. Tumalizie ujenzi, tuunganishe nchi zote zilizotuzunguka. 

Tulenge kasi ya kilomita 480 kwa saa. Hata tukichukua mkopo mkubwa kiasi gani, treni hii ikikamilika itaimarisha usalama. Italiingizia taifa letu mapato makubwa ajabu kwa mizigo ya ‘transit’ kwenda kwa jirani. 

Itazinusuru barabara zetu zinazomalizwa na malori ya mizigo. Itapunguza ajali. Itapunguza gharama za usafiri kwa wananchi wa kawaida. Mama Samia malizia hii reli, maisha yabadilike kwa kasi ya 5G nchini.

Sitanii, miradi kama ununuzi wa ndege, ambao Rais Samia Suluhu Hassan naona ameamua kuuendeleza naye kwa kununua ndege mpya nyingine tano, umelifutia aibu taifa letu. 

Kwamba nchi yetu inatoka katika kumiliki ndege mbovu moja, na sasa inamiliki ndege mpya 11, huku Rais Samia akiagiza nyingine tano, kwa maana zifike 16, ni suala la msingi mno.

Ujenzi wa Bwawa la Nyerere (Stiegler’s Gorge) kuzalisha umeme megawati 2,115, nao ni historia ya Magufuli isiyofutika. 

Ujenzi wa hospitali za wilaya 67 na vituo vya afya takriban 200. Ukamilishaji wa Hospitali ya Mwalimu Nyerere mkoani Mara na mengine mengi. Hayatasahaulika. Siwezi kutaja yote aliyoyafanya hapa yakatosha. Tumuenzi, tuyaige na kuyaendeleza haya mazuri kwa taifa letu.

Hata hivyo, kuna upande wake wa pili wa Rais Magufuli. Huu si wengi wanaopenda utajwe. Wanasiasa wa upinzani kufunguliwa kesi sawa na enzi za mkoloni, hili ni moja ya mambo mabaya kabisa yaliyotendwa na uongozi wake. 

Kitendo cha Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, kupigwa risasa 16, Rais aliyeko madarakani akashindwa angalau kutoa pole kwa Lissu mwenyewe, hadi kesho kitaendelea kunishangaza. 

Hili si la kurudiwa. Si hulka na vinasaba vya Tanzania. Namshukuru Mama Samia, alikwenda hospitalini Nairobi, akampa pole Lissu. Na sasa Lissu amefutiwa kesi zote chini ya uongozi wa Rais Samia.

Tumehitimisha uongozi wa Rais Magufuli mwaka 2021, hivyo ni haki kabisa kujadili kipindi cha uongozi wake kwa ujumla. Mikopo ya kibiashara iliyochukua Serikali ya Magufuli, ni suala ambalo kama nchi tuliepuke miaka ijayo. 

Vitendo vya watu kupotea kama akina Azori Gwanda na Ben Saanane, kamwe visijirudie. Kuibuka kwa msamiati wa “Watu Wasiojulikana.” Kuteua wakuu wa wilaya wanaofanya ujambazi kama Lengai ole Sabaya ilivyothibitishwa na mahakama, kamwe isitokee tena. 

Uchaguzi kufanyika wapinzani wote wakaonekana hawajui kusoma au kuandika, kuanzia uchaguzi wa serikali za mitaa 2019 hadi Uchaguzi Mkuu 2020 wakawa wameenguliwa kwa kujaza “vibaya” fomu wakati walisoma darasa moja na wenzao wa chama tawala, kamwe isirudiwe.

Kumfungulia Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kesi ya ugaidi na kuvunja ukumbi wake wa starehe wa Bilcanas. Tena ugaidi wenyewe unadaiwa ni wa Sh 600,000 na sasa tunaona watesi wake wanalazimika kushona kwa uzi kitabu cha RB kufanikisha malengo yao. 

Hapa naomba niseme, Mama Samia chunguza vizuri. Nikiangalia mwelekeo wa hii kesi, kama ningepata nafasi ya kukushauri, ningekushauri uifute. Wanaokwambia mtie adabu, kimsingi wanachafua jina lako ambalo tangu umeingia madarakani umelijenga vizuri.

Sitanii, huyo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai ole Sabaya, ambaye kesi ya Mbowe imejengwa kwake kuwa alitaka kumdhuru, tayari ametiwa hatiani kwa makosa ya ujambazi, unyang’anyi na wizi wa kutumia silaha. 

Haipendezi kulisema hili, ila wale watesi, bado kuna masalia. Wapo watu ndani ya serikali wanaoamini kuwa kutesa watu ndiyo kuidhihirishia dunia kuwa serikali ina nguvu. Hapana. Hii kesi mama angalia jinsi ya kuimaliza. Haina afya huko tuendako kwa masilahi mapana ya taifa letu.

Vitendo vya kukusanya fedha kutoka kwenye akaunti za wafanyabiashara kwa kutumia vikosi kazi. Kunyamazisha waandishi wa habari kwa kuvinyima matangazo vyombo vya habari walivyofanya enzi hizo, na wakati mwingine kutumia kauli kuwa; “Msidhani mko huru kwa kiwango hicho, watch it.” Mama nakuomba usije hata siku moja ukawaza kulirejesha taifa letu huko. Nakuomba uendelee kujenga madaraja kama unavyofanya sasa badala ya kujenga kuta.

Nilimsikiliza Rais Samia wakati anazindua mkutano wa wadau wa siasa jijini Dodoma, Desemba hii. Kauli nzito na ya kihistoria aliyoitoa kuwa: “Amani haitajengwa kwa ncha ya upanga, bali itajengwa kwa ncha ya ulimi.” 

Naomba kama nchi tuiishi. Tumeona Zanzibar wanavyoneemeka, chini ya uongozi wa Rais Hussein Ali Mwinyi, baada ya kuamua kutumia ncha ya ulimi. 

Tuzungumze na Rais Mwinyi atupe siri. Kama imewezekana Zanzibar, huku mikutano ya hadhara inashindikanaje? Tunashindwaje kufuta kesi za ugaidi za Sh laki sita?

Sitanii, mimi ninayo matumaini makubwa na Rais Samia. Kwa miezi tisa aliyokaa madarakani, amerekebisha mengi. 

Kwa sasa wazazi hawatiwi kitanzi cha kujenga madarasa. Ule mkopo wa IMF alisema atajenga madarasa 15,000 ya sekondari na 3,000 ya shule za msingi. 

Wiki iliyopita nimeona tumepata fedha nyingine zinazoonyesha pia tutajenga madarasa 12,000 ya shule za msingi. Hapo unazungumza madarasa 30,000. Hii ni historia ya pekee.

Kiwango cha madarasa yanayojengwa nacho kinatia moyo. Darasa linakuwa na vigae, gypsum, rangi safi, madawati, madirisha ya aluminium… nawaza kuwa viwango hivi vipya ulivyoviweka, ikikupendeza angalia upate ‘kijisenti’ sehemu hata madarasa ya zamani yakarabatiwe yawe na viwango sawa na madarasa mapya yanayojengwa. 

Hiyo ni haki ya binadamu kabisa. Tena nimepewa salamu na wanakijiji wa Kata ya Nyanga, Wilaya ya Bukoba (M) wanamshukuru Rais Samia kwa kusambaza nguzo za umeme nyumba kwa nyumba.

Nimesema wamefariki dunia watu wanne. Najua waliofariki dunia ni wengi, ila baada ya kumtaja Rais Magufuli, basi nipate fursa ya kumtaja Mkurugenzi mwenzetu; Mkinga Babu Mkinga, aliyefariki dunia Juni 24, 2021. 

Huko uliko Mkinga pengo lako halijazibika. Tunakuombea Mungu akupe pumziko la amani. Mbali na Mkinga, wamefariki dunia mke wa baba mdogo, Ma – Rugeni, maarufu kama Mama Joyce mwezi Agosti. Novemba, akafariki mama mdogo pale Katoma, Ma-Anastazia Christopher. Wote hawa walinigusa mno. Mungu azilaze mahala pema peponi roho zao. Bwana alitoa, Bwana ametwaa, Jina la Bwana Lihimidiwe…

Sitanii, kichwa cha makala hii nimesema “Tusiusahau 2021, tujiandae 2022.” Machache niliyoyataja hapo juu yanatufahamisha nchi tuliyomo. Yanatufahamisha tunavyoweza kuitunza amani au kuiharibu. Yanatueleza kuwa nchi yetu inaweza kuwa na amani ya watu kutulia au kutulizwa. Gharama ya kutuliza watu ni kubwa. Rais Samia amesema tutumie ncha ya ulimi kumaliza matatizo yetu, badala ya ncha ya upanga. Twende mkondo huo.

Vyama vya siasa fanyeni siasa. Hapa mtanisamehe nitawasema nyote. Ndani ya chama tawala kuna vurugu za kimyakimya. Wachache wanakuja hadharani na kusema wanataka kufundisha watu shule ya uongozi. Unajiuliza, wakati wanazo nyadhifa walikuwa wapi kutufundisha huo uongozi. Kwa nini mafundisho hayo yaje sasa? Vyeo vinasumbua. Wapo wanaowaza mwaka 2022 ni wa uchaguzi ndani ya CCM. Kwa maana hiyo wanajipanga kuweka watu wao. Wanapiga pasi ndefu ya 2025!

Na hapo ndipo utaona sasa wanafanya kila mbinu kuchafua sura ya kila wanayedhani ni tishio kwao. Watasuka mipango viongozi wa upinzani washitakiwe, wakijua aliyeko madarakani ndiye ataangushiwa jumba bovu na wapigakura wakikumbuka kesi hizo siku ya kupiga kura. 

Watapenda kufungia vyombo vya habari. Katika hili Rais Samia nakushukuru, na naomba kama alivyosema Dk. Ashatu Kijaji, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, basi mwaka mpya tuuanze magazeti ya Mwanahalisi, Tanzania Daima, Mawio na Mseto yakiwa yamerudishiwa leseni, hili nalo tulimalize. Nashukuru hatua yalipofikia mazungumzo, ila itapendeza tukilihitimisha kabla mwaka 2021 haujaondoka.

Sitanii, wakati ndani ya chama tawala kuna hiyo ngoma ya uchaguzi wa chama 2022, nirejee ombi langu, kwamba kesi ya Mbowe kama ulivyosema kusamehe kupo, basi tutumie ncha ya ulimi kupata amani. Ikikupendeza Mbowe naye ale mwaka mpya akiwa na familia yake; yaani – mke na watoto wake, bila kuwasahau wanachama wenzake. Hili limo ndani ya uwezo wako Mhe. Rais Samia, unaweza kulitenda. Mara zote, mama huwa na huruma na hupenda amani itamalaki. Mungu akutangulie katika hili.

Kwa vyama vya upinzani, nanyi mniruhusu niwaseme kidogo. Acheni kusambaratishwa na ruzuku. Nimeshuhudia NCCR-Mageuzi ya mwanzo, TLP, CUF ya Prof. Lipumba, UDP pale mzee John Cheyo alipogombana na Amani Jidulamabambasi, ingawa mzee Cheyo ukimwambia hili anatamani kukuchapa kibao na mimi nimeishapokea moja ya matusi yake hapo Dodoma kwa kulisema hili.

Vyama vya siasa viruhusiwe kufanya mikutano ya hadhara kama sheria inavyotaka, ila vifahamu kuwa sheria inaviruhusu kujijenga kupitia mikutano ya hadhara na kusajili wanachama, si zaidi ya hapo. 

Lugha zinazotumika kwenye mikutano zisiweke ukakasi kwa wanaowasikiliza. Wala haihitajiki kutumia matusi ndipo mtu aonekane ni jasiri. Tanzania tujenge utamaduni wa kutumia lugha zilizosheeni uungwana ndani yake.

Sitanii, naomba nihitimishe na polisi. Uzoefu wangu katika kuripoti mambo ya siasa tangu mwaka 1990, unanionyesha kuwa polisi wanapozuia mikutano ya siasa, wanatumia nguvu na gharama kubwa kuliko wanapoamua kuilinda ifanyike kwa amani. 

Mikutano ambayo polisi wametoa ulinzi badala ya kuzuia mara zote imeisha kwa amani. Sasa niseme kwenu polisi, kauli ya Rais Samia nanyi inawahusu. 

Amani haipatikani wa ncha ya upanga, bali kwa ncha ya ulimi. Sababu mnayotoa kila mara kuwa “taarifa za kiintelijensia mlizonazo” imeishachusha masikioni mwa Watanzania. Ikiwa ipo sababu ya msingi, itajwe na kwa uwazi.

Mwisho, naomba kuwasihi kuwa Tanzania ni nchi yetu sote. Iwe ni chama tawala, vyama vya upinzani au polisi, tunapaswa kujenga Tanzania iliyo bora zaidi leo kuliko ya jana. 

Badala ya kutumia muda wetu katika malumbano ya kisiasa, nashauri tuutumie muda mwingi katika kujenga uchumi wa viwanda. Hakuna nchi iliyopata kuendelea kwa siasa za majukwaani.

Kwa pamoja tujikite katika kuhamasisha sera ya viwanda, vijana wetu wapate ajira, viwanda vilipe kodi, tupate fedha kama nchi, tujenge miundombinu ya kisasa kama reli ya umeme, viwanja vya ndege, meli kubwa na za kisasa, barabara za lami hadi vijijini, umeme kila nyumba, maji ndani ya mita 400 na mengine mengi ya hivi. 

Hizi ni ajenda ambazo tukizihubiri katika mikutano ya kisiasa bila kusahau mapambano dhidi ya rushwa na wakwepa kodi, tutajenga Tanzania imara hadi kila awaye aduwae. Mungu ibariki Tanzania. Nawatakia heri ya mwaka mpya 2022.