Katika dunia yetu ya leo ya utandawazi, suala la nchi yoyote duniani kubaki kama kisiwa halipo kabisa. Maendeleo katika  teknologia ya mawasiliano yameifanya dunia yetu igeuke kuwa kijiji kimoja.

Tofauti zilizopo kati ya nchi moja na nyingine zitabaki zile za kihistoria ya nchi hiyo — siasa yake, uchumi wake na  masuala  mengine ya kijamii, ambayo hayahusu mfumo wa mawasiliano ya teknolojia ya kisasa unaotoa fursa watu kupata taarifa, elimu na hata kufanya biashara pasi na kuonana ana kwa ana baina ya mnunuzi na muuzaji.

 

Mataifa ya Ulaya chini ya Umoja wao wa Jumuiya ya Nchi za Ulaya, yamekuwa yakipigania kuulinda Umoja huo kwa udi na uvumba. Jumuiya hiyo ambayo imeendelea kudumu kwa muda mrefu sasa, ina wanachama wasiopungua ishirini na nane.

Kwa kupitia Umoja huo, nchi hizo za Ulaya zimeshirikiana katika masuala ya kiuchumi na kijamii, japo kuna matatizo ya hapa na pale.

Wamekuwa wakijitahidi kupambana nayo yakiwamo masuala ya ajira, uhamiaji haramu, kupukutika kwa maliasili zao, uharibifu wa mazingira, ongezeko la hali joto duniani na kuibuka kwa China kama nchi tishio katika soko la dunia.

 

Katika makala yangu ya leo nataka kujikita katika suala linaloendelea katika ukanda wa Afrika Mashariki. Suala la dalili za kumeguka kwa Jumuiya hiyo linaanza kuchomoza.

Sina haja ya kurejea historia, madhumuni na malengo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) iliyovunjika mwaka 1977 na iliyokuwa imezijumuisha nchi za Tanzania, Kenya na Uganda, Rwanda na Burundi na muda si mrefu Sudan Kusini pengine itatambuliwa rasmi zimejiunga hivi karibuni.

Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na taarifa kwamba Uganda, Kenya na Rwanda zimekuwa  zikiendesha vikao na kufikia uamuzi  bila  kuzishirikisha Tanzania na Burundi,  kitu ambacho kimetafsiriwa  ni dalili za  kutaka  kuwatenga wenzao — Tanzania  na Burundi.

 

Je, kitendo cha nchi tatu kuwa na vikao ambavyo sielewi kama ni rasmi  na havikubaliki kutokana na kanuni  zinazoendesha na Jumuiya hiyo, kitavuruga ndoto za pamoja za EAC?

Je, kwanini Kenya, Uganda na Rwanda wamefikia hatua hiyo? Je, Tanzania na Burundi zimekiuka taratibu zipi ambazo  wenzao  wameona  kuwa ni vyema waanzishe  sasa EAC ‘C’?

 

Waziri wa Afrika  Mashariki, Samuel Sitta, aliwaeleza wabunge  kuwa Tanzania  inazungumza  na Burundi  na Jumhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) juu ya uwezekano  wa kuanzisha  ushirikiano  mpya wa kiuchumi.

 

“Mazungumzo na Burundi yanaendelea; mazungumuzo (DRC) yanaendelea kwa maana ya kushirikiana,” amesema Sitta.

 

Amesema kuwa uchumi mkubwa upo DRC na si Rwanda na Burundi. Ninatambua wazi, Sitta kama waziri mwenye dhamana, sidhani kama ana ndoto za kuona

 

Tanzania ikijiengua kutoka katika EAC — sitarajii hilo kabisa. Lakini  kwa nini kuwepo na mazungumuzo  ya kuzihusisha  Kongo na Burundi kabla ya kutafuta ukweli na sababu za Kenya, Uganda na Rwanda kuwa na vikao nje ya vile vinavyotambulika Jumuiya hiyo?

 

Je, Tanzania haioni kuwa kuanzisha mazungumzo  na Kongo na Burundi badala ya kuwaita wenzao na kuwahoji kulikoni ni kufungua mlango na kuiaga rasmi EAC?

 

Sasa kwanini tufike huko? Tusiingilie utajiri  na ukubwa wa Kongo  na  kuanza kufikiria kufunga nao ndoa ya mkeka.

 

Tutajuta baadaye kama Taifa. Nchi zote za Afirika  Mashariki  bado zinahitaji mshikamano ndiyo sababu  hakuna nchi inayotaka kusimama yenyewe kama nilivyotangulia kusema awali.

 

Kila nchi inategemea nchi nyingine katika kukuza uchumi wake; Serikali ya Tanzania na Rwanda zinashirikiana katika ujenzi wa daraja, lengo ni kutaka kusaidiana kukuza uchumi wa pande zote mbili.

 

Miundombinu ya  barabara kati ya Tanzania na Kenya imekuwa ikitumika kuinua kiuchumi  wa nchi hizo kwa kipindi kirefu tu.

 

Uganda, Rwanda na Burundi ni nchi ambazo hazina bahari (land locked countries), hivyo ukuaji wa uchumi wao unategemea Kenya au Tanzania. Sasa nje ya Jumuiya ushirikiano wa kibiashara miongoni mwa nchi hizi utazorota.

 

Hivi karibuni Rais Jakaya Kikwete amewataka viongozi wa Mkoa wa Njombe, kuwapatia fursa wakulima wa mahindi kuuza mazao yao nje ya nchi ili waweze kuingiza pato lao.

 

Sasa nje ya Jumuiya sidhani kama wakulima hawa pamoja na wafanyabiashara wengine wa ndani wataweza kunufaika endapo hakutakuwa na fursa ya kuuza nje bidhaa zao kwa uhuru na kwa maslahi mazuri.

 

Ni lazima kutakuwapo na vikwazo ambavyo ndani ya Jumuiya huenda visiwepo. Vita baridi ina madhara makubwa kiuchumi na kijamii.

 

Tanzania na Burundi ni vyema, kwa kutumia diplomasia na si jazba za kisiasa, ziwaite wanachama wenzao hata kwa vikao vya dharura ili waweze kuwasilisha dukuduku lao badala ya kuanza kuzungumza pembeni, kwa sababu kauli hizi zinazotolewa na viongozi wetu, zinawafikia walengwa kwa njia isiyo rasmi.

 

Kila nchi iliyomo kwenye EAC ina mwakilishi wake – balozi wake — hivyo mijadala hii inawafikia walengwa na hatuwezi kujua majirani zetu tunaowatuhumu wanazitafsiri vipi kauli za viongozi wetu.

 

Sasa sidhani kama hii ndiyo dawa ya kuzungumza nje ya vikao vya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Ni kweli Bunge pamoja na wananchi wanapaswa kuelewa kinachoendelea, lakini wananchi pamoja na viongozi wengine, wangependa kujua kauli kutoka kwa wale wanaoonesha dalili za kutaka kujitenga, kwa sababu makubaliano yote yanayopitishwa huwekwa saini na pande zote husika.

 

Hivyo kama kweli wenzetu wanataka kutuacha, basi ni lazima tupate ukweli kupitia vikao vya EAC.

Lakini kwa nini wenzetu wanataka kutuacha, Je, ni kelele za Rwanda na Kongo kuhusu ucheleweshaji wa mizigo yao bandarini? Je, ni lawama zilizokuwa zikitolewa na nchi hizo kuhusu upotevu wa mali zao katika bandari yetu?

 

Kwa sababu kinachofanywa na hawa wenzetu Kenya, Uganda na Rwanda ni kutaka kutumia Bandari ya Mombasa. Je, Bandari ya Mombasa inakidhi matakwa ya Rwanda na Uganda kuliko ilivyo kwa bandari yetu ya Dar es Salaam? Na kama ni kweli kwa nini iwe hivyo?

 

Pamoja na jitihada zote zitakazofanywa viongozi wetu ni lazima wahakikishe kuwa siasa haitumiki katika kujadili suala la kujitoa. Siasa itumike katika kuimarisha uhusiano wetu katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo.

Uchumi wetu bado unahitaji kukua. Ukuaji wa uchumi wetu bado utahitaji ushirikishwaji wa wanachama wote wa EAC bila kujali nani anataka kuwa mwiba kwetu.

 

Hivyo, biashara ya pamoja ni jambo lisiloepukika. Tunachozalisha, ziada lazima ipelekwe nje kwa manufaa ya wazalishaji na Taifa kwa ujumla. Ukiachilia mbali suala la uchumi kuna suala zima la ulinzi na usalama. Nchi zetu zinahitaji ushirikiano mkubwa kiulinzi ili kuhakikisha usalama unakuwapo. Utengano wetu unaweza kutoa fursa kwa magaidi kuendelea kuwa tishio katika nchi zetu.

Hakuna anayependa kuona kwa jirani yake kunateketea. Uvamizi uliofanywa na Al-shabab jijini Nairobi katika Jengo ya Westgate, si kwamba ulikuwa na athari kwa Kenya peke yake, la hasha. Tumeona baada ya tukio lile, jinsi gani vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vilivyoanza kuchukua tahadhari dhidi ya mashambulio yoyote ya kigaidi dhidi yetu.

 

Ni matarajio yangu kuwa Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki atajitahidi kufanya kila linalowezekana ili kuhakikisha mazungumzo yanafanyika na hatimaye sababu za wenzetu kuanza kujitenga itaeleweka.

Endapo vikao hivyo vinaruhusiwa kikatiba basi wananchi waelimishwe. Inawezekana kuna uwezekano wa kuwapo maafikiano ya mengine ndani ya Jumuiya, ambayo hayawezi kuathiri ushirikiano mkuu ambao ndiyo mhimili wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

 

Kama tumeweza kuwa mfano bora wa kuwa na muungano uliodumu zaidi ya miongo minne, kwanini tushindwe kutafuta suluhisho katika hili linaloendelea kujitokeza?

 

Nitoe changamoto kwa kila muumini na anayeamini kuwa dunia yetu ya leo inahitaji kuwa na ushirikiano wa karibu kuliko nyakati zote zilizopita.

[email protected]

0763 400 283