Kwa wale wazee wenzangu nadhani kama bado wanakumbuka vile vijarida vya Sauti ya TANU, vilikuwa vinatuhabarisha mengi siku zile.
Kwa mfano Sauti ya TANU na. 18 ya Desemba 16, 1957 ibara ile ya 5 Mwalimu Nyerere alisema wazi wazi kwa nini alijiuzulu nafasi yake ya kuteuliwa katika lile Baraza la Kutunga Sheria (Legico).
Dai lake lilikuwa Baraza likubali kubadili Kanuni za Uchaguzi wa Mseto (by removing this irritation which it was a public secret government was only a few months ago willing to remove), lakini serikali ya mkoloni iligoma katu katu kurekebisha bila sababu yoyote, bali ni kiburi tu cha serikali kukandamiza upinzani kwa nia ya kubomoa au kuua upinzani. Basi, hakuwa na njia; isipokuwa kujiengua kutoka katika Baraza lile.
Historia hiyo inatuelimisha hata sasa kuwa upinzani daima wanaonewa. Kama hivyo ndivyo, je, ni busara kwa wapinzani kuvimbishiana misuli na Serikali? Kuna manufaa kwa wananchi katika hali namna hiyo?
Baba wa Taifa ametuonesha wazi kuwa ili kuwanufaisha wanyonge wanaotetewa na upinzani HEKIMA na BUSARA vinahitajika kuleta uamuzi shirikishi ili wananchi wavune wanachokitarajia kutoka kwa wajumbe wao bungeni.
Nafasi pekee na nzuri za kupeleka vilio vya wanyonge ni kushiriki mijadala ya Bunge hasa la Bajeti. Kuachia Serikali peke yao watapitisha madudu ambayo kama wapinzani wangekuwapo wangeonesha na Serikali ingegutuka ikabadili mwelekeo.
Hofu ile aliyokuwa nayo Mwalimu pale Tabora kuwa kama TANU itasusa, vyama vingine vitapata nafasi ya kuingia katika Legico na hapo lengo letu (TANU) halitapata wasaa wa kuingia katika Serikali na kuongoza nchi – kumbe kwa busara ile ya kiongozi Nyerere kushawishi chama kiingie kwenye kupiga kura za mseto, TANU ndipo ikafanikiwa kukumba viti vyote na leo hii nchi yetu iko HURU (Taz. Mwito wa Uhuru by Saadan Abdu Kandoro uk. 105).
Nadhani kama CUF kule Visiwani wangekuwa na mtazamo namna ile si ajabu wangeibuka tena na ushindi kulazimisha CCM kukubali kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Lakini kwa kususa, ehee, CCM imejipatia Serikali kiulaini kabisa kabisa.
Huku Bara, kama upinzani kwa kutumia vijana wake wasomi na talented kama kina Tindu Lissu, Ester Bulaya, Halima Mdee, Zitto Kabwe, John Mnyika na Kiongozi wao Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe ni dhahiri kungepatikana mabadiliko mengi katika BAJETI ya mwaka huu. Kamwe Serikali isingepitisha kiulaini. Now it is a one sided show!
Kumbe demokrasia safi lazima pawepo na mkosoaji hapa na pale. Nafasi nzuri sana ya kutoa mapendekezo au kilio cha wanyonge ndiyo imepotea kwa huo utamaduni wa kususia vikao. Sasa kwa nini mlikwenda Dodoma? Kuona au kushiriki? Kila mtu anaruhusiwa kuona, lakini si kila mtu anapata fursa ya kuchangia mawazo bungeni – ni wawakilishi waliochaguliwa tu wana fursa hiyo.
Tunahitaji kuwa na mtazamo hasi wa vikao vya Bunge na siyo kuingia kuchungulia kisha kusimama kundi lote kuchopokea nje. Huko si kuwatendea haki wapiga kura wenu. Huko ni kuwanyima haki zao za uwakilishi. Ni kubinya demokrasia ya Kitanzania. Upinzani tangu enzi za ukolonii ulilenga kufikisha vilio vya wanyonge kwa Serikali tawala.
Wazee katika makabila yote ya Kibantu wanakuwa na vikao vya kujadiliana mambo yao ya ukoo. Mzee akisutwa na akaamua kuondoka penye kikao, Wangoni wana msemo huu, “UKA DUVAYI TE TIKIMALI MIHALU YITU YOHA KWALI WAMWENE” ndio kusema UKISUSA KIKAO CHETU CHA MAJADILIANO, SISI TUTAENDELEA NA KUFIKIA UAMUZI TU. Shauri lako mwenyewe utakayekosa kujua tulichoamua.
Yaani hakuna atakayekufuata na kukueleza tumeamuaje, hivyo hasara ni yako kwa ubinafsi wako. Kule Musoma Wazanaki wanakutana chini ya mti kumaliza mashauri yao. Walikubaliana hapo chini ya mti wao kuwa ndipo mahali pa kuongelea mambo yao ya kimila… Katika vikao namna ile chini ya mti, mtu mmoja asipokubaliana na wenzake huwa anasusa kikao na kuondoka hapo. Basi, huwa analalamika kilugha – “amang’ana gasarikiri” akimaanisha mambo yameharibika, lakini wenzake hawamfuati kumbembeleza – ndiyo demokrasia ya Waafrika. Wanaendelea na kikao. Kususa ni ubinafsi na kutokufikiria matakwa ya wengine.
Basi, Watanzania hatutaki demokrasia yetu iharibiwe na wachache kwa tabia au mtindo huo wa kususa vikao halali. Tuikuze na kukubaliana bila ushawishi wa Wazungu waliotutawala. Tuwe na demokrsaria asilia ya Wabantu. Wazungu wanatafuta kila njia kutuvuruga ili warudi tena kwa mlango wa nyuma, watutawale kiuchumi. Hamuoni hilo? Chama gani cha siasa kimewahi kualikwa kwenda kushuhudia uchaguizi kule Ulaya au Marekani?
Kwa nini sisi tunawakaribisha kuja kuangalia uchaguzi wetu? Shauri la visenti vyao hakuna kigezo kingine zaidi ya hicho cha kuwaomba misaada! Tutaendelea kutawaliwa kweli kiuchumi.
Haya nimeyaandika kutokana na kumbukumbu zangu za historia katika nchi yetu. Vijana wote waliozaliwa miaka ya 1960 baada ya Uhuru hawajui baadhi ya niliyoyaandika katika makala hii. Lakini bila ya kura ile ya mseto ya mwaka 1958/1959 na ‘retold’ historia hii vizazi vipya vitakwenda na maji kwa mkumbo wa ustaarabu wa Magharibi.
Hivi sasa utamaduni wa Kitanzania unafifia na utamaduni wa Magharibi hasa katika nyanja za nyimbo, mavazi, miondoko na hata siasa unaenea kwa kasi sana nchini mwetu. Dharau inaanza kuonekana. Heshima kwa wazee inatoweka. Ni hatari kwa Taifa.
Tudumishe mila na utamaduni wetu. Kitu ‘zomea zomea’ ni “western culture” na kuna hata kutupiana mayai viza! Je, tufike huko? HAPANA!
Tusikubali kufikia hali namna hiyo hapa Tanzania. Wazee kweli tumesahau historia yetu hii. Mapokeo yanadai tuwakabidhi vizazi vipya historia ya ukombozi wetu ili nao wawe wazalendo kweli kweli.
Kule Uyahudi na Palestina, watoto wanapakazwa uzalendo na kufundishwa maadui wa uhuru wao ni akina nani. Vipi sisi tunashabikia sana maono na maelekezo kutoka nje? Ni uzalendo gani tunaujenga katika fikra za kizazi kipya?
Tuwe Watanzania na hasa wazalendo. Tuache zomea zomea, tusisusie vikao ila tuwe Watanzania halisi. It can be done, play your part (Nyerere: Bunge Karimjee tarehe 12 Mei, 1964).