Leo gazeti hili la JAMHURI limechapisha taarifa za Jeshi la Polisi kutangaza orodha ya watu 11 wanaotuhumiwa kufanya mauaji huko wilayani Rufiji. Mauaji haya yanafanywa kwa utaratibu wenye kutia shaka. Hawauawi wananchi wa kawaida. Wanauawa viongozi.
Hadi sasa viongozi wapatao 30 tayari wameuawa na watu hawa wasiofahamika. Serikali kila wakati katika taarifa yake inawaita wauaji hawa kuwa ni majambazi. Sisi katika matoleo mawili tofauti tumesema wanaofanya mauaji ni wafuasi wa kundi la al-Shabaab la nchini Somalia.


Tumeeleza jinsi vijana katika wilaya za Rufiji, Kibiti, Mkuranga na maeneo mengine wanavyokusanywa na kusafirishwa kwenda Somalia. Tumeeleza pia kuwa wazazi wao wamekuwa wakinufaika kwa kupata wastani wa dola 3,000 (zaidi ya Sh milioni 6) kwa mwezi, kutokana na watoto wao kuwa Somalia.
Tulichobaini ni kuwa viongozi wa kisiasa na Serikali wanaouawa wanatuhumiwa kutoa siri ya orodha sahihi ya vijana wanaosafirishwa kwenda Somalia, ambao baadaye Serikali inafanya utaratibu wa kuwarejesha nchini. Hata wanaporejeshwa inakuwa hawafurahi.


Kuna matukio kadhaa yenye kuonesha kuwa viongozi wa kisiasa na kiserikali wamekuwa wakiuawa kutokana na kinachodaiwa kuwa wanavujisha ‘siri’ za vijana hao. Tumeona mauaji kadhaa ambayo polisi wameuawa, viongozi wa kisiasa na baadhi ya wananchi kwa kuzuia maslahi ya wanaofanya mauaji hayo.
Tanzania imekuwa nchi ya amani na utulivu kitambo. Matukio ya Rufiji, Mkuranga na Kibiti yanapaswa kutukosesha usingizi. Sisi hatutaki kuamini kuwa wanaofanya mauaji haya ni vichaa. Lakini pia tunasema bayana kuwa kwa sababu yoyote iwayo, hatuungi mkono mauaji haya.


Kwa vyovyote iwavyo, tunaamini tayari nchi yetu imefika hapo ilipo. Suala hapa ni tunatokaje? Tumejiuliza, tumetafakari na kufikia wazo tunaloomba kulifikisha kwa Serikali. Tusisubiri yatukute yaliyowakuta Wakenya kule Westgate. Nchi yetu iandae mazungumzo ya kupata ufumbuzi.
Tutafute wazee, viongozi wa dini, kina mama na watu wenye staha katika jamii kwa maeneo ya Kibiti, Mkuranga na Rufiji tuwape jukumu la kuiepusha nchi yetu na janga. Ikibidi tuunde Kamati au Tume itakayofanya kazi usiku na mchana kujua wanaofanya mauaji wanataka nini.


Sisi tunapenda kusisitiza kuwa tusikimbilie majibu mepesi ambayo yamesambaa maeneo mengi nchini kuwa wanaofanya mauaji wana malengo ya kidini au kisiasa. Tukifanya kosa la kuhukumu bila kuwasikiliza, tutajuta mbele ya safari.
Tunasema wakati umefika sasa kwa Serikali kufanya uchunguzi wa kina na kuja na majibu ya msingi yenye kuimarisha ustawi wa Taifa letu. Majibu haya yatatokana na ushirikishwaji wa jamii husika. Bila hivyo, nchi yetu itayumba na hatupendi tufike huko. Tutafute chanzo cha mauaji Mkuranga, Kibiti na Rufiji, kisha tushirikiane kudhibiti mauaji. Mungu ibariki Tanzania.