Miongoni mwa jamii ya kimataifa, nchi inapojiuliza watu wangu watakula nini leo, basi kwa kiasi kikubwa inapaswa kujibu hilo swali yenyewe na kutafuta suluhisho yenyewe. Yanapotokea majanga yanayoathiri uwezo wa nchi kuzalisha chakula cha kutosha, upo utaratibu wa muda mfupi kutoka nchi nyingine wa kusaidia nchi iliyoathirika kuweza kukabiliana na tatizo hilo. Lakini katika mtazamo wa muda mrefu ni kila mtu na lwake.

Lakini uwezo wa nchi moja na nyingine wa kukabiliana na uzalishaji duni wa sekta ya kilimo unapishana kwa kiwango kikubwa. Lakini katika jitihada hizi za kuhangaika kutafuta njia za uhakika za kuzalisha mazao ya chakula, nchi zilizoendelea zimejifungulia milango wazi kutoka kwa wataalamu wa nchi zilizofanikiwa kukabiliana na tatizo hilo. Athari za ukweli huu zinaweza kuwa janga ambalo tulitarajie tu litatokea.

Tunaambiwa kuwa moja ya masuluhisho dhidi ya tija ndogo katika kilimo ni matumizi ya mbegu bora ambazo zinaongeza uzalishaji kwenye eneo lile lile la ardhi inayotumika. 

Wataalamu wanaweka uzalishaji wa mbegu katika makundi matatu: mbegu asilia ambazo mababu zetu wamezitumia tangu enzi za adamu na hawa; mbegu mahuluti au mbegu zinazoboreshwa na wataalamu kwa kutumia aina mbili za mbegu kutoka kwa familia ya mbegu zinazofanana ili kuzalisha mbegu ambayo inabeba sifa bora za aina hizo mbili za mbegu; halafu kuna mbegu mvyauso, mbegu ambazo zinaundwa kwa mchakato unaounganisha aina mbili za spishi (wanyama au mimea) ambao kamwe isingewezakana kuwa na mchakato wa kupokezana mbegu kati yao. 

Kwa hiyo, kwa mfano, kwa mchakato wa kutoa mbegu mahuluti, wataalamu wanaweza kuunganisha aina mbili za ndizi ambazo zinatofautiana kwa kiasi fulani na kutoa mbegu bora zaidi. Kwa mbegu mvyauso, tunazungumzia mambo ya kutisha na ambayo hayawezekani kabisa katika mazingira ya kawaida ya viumbe na mimea. 

Hapa zinaweza kuunganishwa chembe hai za samaki na za mmea ili kutoa mbegu ambayo ina sifa mpya kabisa ambazo hazijawahi kuwapo. Natumia neno sifa siyo kwa kumaanisha ubora wa zao linalojitokeza lakini kwa kumaanisha hata ubaya ambao bado haujabainika wa hiyo mbegu mpya.

Labda tutaambiwa kuwa mbegu mvyauso mpya za mahindi zinaongeza uzalishaji kwa asilimia 1,000 kulinganisha na mbegu zilizopo bila kufahamu kwa uhakika iwapo mahindi yatokanayo na mbegu hizo yataathiri vipi afya zetu.

Kuna ubishi mkubwa wa kisayansi unaoendelea kuhusu iwapo mazao ya chakula yatokanayo na mbegu za aina hii yamethibitishwa kuleta athari yanapotumiwa na binadamu. Kwa bahati mbaya, mashirika yanayouza mbegu hizi yana uwezo mkubwa wa fedha na yametoa matokeo ya kitafiti yanayodai kuwa mazao yanayotokana na mbegu hizi hayana madhara yoyote kwa binadamu. Kwangu, matokeo kama haya ni ya kutiliwa shaka kutokana na kasoro za kimuundo za tafiti zenyewe, muundo ambao unachangia kutoa matokeo yenyewe.

Lakini inatosha kuwa na shaka juu ya matokeo haya hata kama tunakubali kuwa tafiti zenyewe ni thabiti kimuundo. Kama nimetembea porini kwa siku saba na sijakutana na simba mla watu, haina maana kuwa simba huyo hayupo ndani ya pori nitakalolifikia kesho. Wanasayansi wanapenda tuamini kuwa kama kitu hakionekani, basi hakipo.

Umri wa viumbe na mimea hii mipya inayoundwa kwenye maabara za sayansi ni mdogo sana, na haitupi sababu yoyote ya msingi ya kuamini kuwa hakuna athari ambazo tutakabiliana nazo kesho au kesho kutwa kwa sababu tunakubali kuvipokea.

Labda tutashiba leo kuepukana na njaa inayotukabili, lakini haraka yetu ya kukabiliana na njaa hii, bila sisi wenyewe kuwa na uwezo wa kutafiti kinachotufaa na kisichotufaa, inaweza kuwa chanzo cha balaa kubwa kwetu kwa siku zinazokuja.

 

<<TAMATI>>