Kwa mara nyingine wiki hii nchi imesisimka na hoja kubwa ya kumbukumbu ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Ni wiki ambayo taifa, Bara la Afrika na dunia wanakumbuka maisha ya kiongozi huyu wa kupigiwa mfano. Kumbukumbu hizi zinajikita katika kumbukizi ya kifo chake, kilichotokea jijini London miaka 20 iliyopita.
Mwalimu ametuachia masomo mengi makubwa kama taifa na kwa mtu mmoja mmoja. Ndiyo maana hata baada ya kupita miaka 20 baada ya kifo chake, inapofika wiki ya kumbukumbu yake nchi husisimka kwa sababu yanayojadiliwa yana akisi sehemu kubwa ya maisha ya Watanzania kama watu binafsi na hasa walio katika dhamana ya uongozi.
Mwalimu alikuwa kiongozi jabali kiasi kuwa katika maeneo mengi ya uongozi, yale aliyoyafanya au kuyasema, yamewekwa kama kipimo au kigezo pale wananchi wanapotaka kupima utendaji, uwajibikaji na weledi wa kiongozi fulani.
Si ajabu hata baadhi ya viongozi wanapotaka kuonyesha kuwa wanafanya vizuri katika kazi zao, hujifananisha na Mwalimu kwa kutaka kuonyesha kuwa yale wanayoyafanya yanarandana na yale ambayo Mwalimu aliyafanya au aliyasisitiza wakati wa uongozi wake.
Aghalabu katika wiki kama hii taasisi na watu binafsi hujitokeza na kutoa maelezo ya jinsi wanavyomfahamu Mwalimu Nyerere. Wapo wanaokwenda mbali zaidi na kujinasibisha na maisha ya Mwalimu Nyerere kiuongozi, wakijaribu kuuaminisha umma kwa kutoa mifano ya jinsi wanavyomuenzi Mwalimu kwa kuishi maisha yake kama viongozi.
Lakini kwa bahati mbaya sana wapo wanaofanya hivyo kwa kuchagua baadhi tu ya mambo ambayo Mwalimu aliyasimamia. Wanajinasibisha na mambo hayo huku wakikwepa mambo mengine ambayo Mwalimu aliyakemea. Yaani, wanataka kuuonyesha umma kuwa wanamuezi Mwalimu kwa kuchagua vipande ambavyo wanadhani vinaweza kuwapatia sifa nzuri katika jamii. Huu ni unafiki.
Ni kweli kuwa hakuna binadamu anayependa kutambulika kwa mabaya. Lakini katika ukamilifu wa maisha ya mtu, huwezi kukwepa kufanya makosa.
Kama kweli kukosa ni sehemu ya ubinadamu, basi wale wanaoficha makosa yao wanaficha sehemu ya ubinadamu wao. Haiwezekani kuwaamini watu wa aina hiyo.
Watu wastaarabu huwa wanakiri pale wanapofanya makosa na ikilazimu wanaomba radhi.
Lakini ukiona mtu, tena kwa makusudi, anakwepa kutaja makosa yake aliyofanya, na kujidai kwamba mambo mazuri anayofanya yanafanana na yale ambayo Mwalimu Nyerere aliyasimamia, mtu huyo ni wa kuchungwa sana.
Hata Mwalimu mwenyewe katika hotuba yake ya kuaga alipong’atuka kutoka katika uongozi wa umma, alikiri kuwa alifanya makosa, kwa sababu yeye hakuwa malaika na akaomba radhi kwa makosa hayo. Huo ndio uungwana. Kama kweli watu wanataka kumuenzi Mwalimu kwa haki, basi wanapaswa kujinasibisha na mambo yote ambayo Mwalimu aliyasema na kuyafanya, si kuchagua mazuri tu.
Kama Mwalimu aliweza kuonyesha upande wake mwingine kwa kukiri kuwa alifanya makosa, hawa wanaojinasibu kuwa wanamuenzi kwa kujikita upande mmoja tu, kweli wanamuenzi Mwalimu au wanatufanyia sanaa?
Lakini kwa upande mwingine, wanaochagua mambo ya kujinasibisha na Mwalimu wanamwonyesha Mwalimu kwa picha ambayo hailingani naye. Kwa kuwa Mwalimu amekwishatutoka na tumeamua kama taifa kumtumia kama kielelezo na somo la kitaifa, basi ni vema tukamtumia Mwalimu kwa ukamilifu wake kwa kuonyesha yote aliyoyafanya na kuyasema. Mwalimu hakuwa mwema pekee, alikuwa na ubaya wake. Kwa kuonyesha pande hizo mbili kwa ufasaha itakuwa ndiyo njia ya kumuenzi na kuonyesha ukamilifu wake.
Kimsingi, wale wanaojinasibisha na Mwalimu kwa kuchagua yale yanayofurahisha na kujenga tu, wanaonyesha jinsi ambavyo hawakumwelewa Mwalimu. Kwa waliomwelewa Mwalimu, wanajua kuwa ni vigumu sana kujinasibisha naye kwa vipande vipande, ukichagua baadhi ya mambo tu na kuyaacha mengine yanayomhusu.
Kama taifa, tunapaswa kuendelea kushukuru kuwa tulijaliwa mtu kama Mwalimu Nyerere ambaye alijua anachokitaka na si tu kuwa alikisema wazi hadharani, bali alikitenda pia na hayo yamesaidia kuijenga Tanzania kama moja ya mataifa yanayoheshimika duniani.
Kama Tanzania imeweza kusimama yenyewe kutokana na matendo ya Mwalimu, basi na viongozi ambao wanadhani kuwa wanafanana na Mwalimu, wajiachie wasimame wenyewe na Watanzania watawaona na kuwapima kama kweli wanafanana na Mwalimu na kumuenzi. Viongozi hawa wawe kitu chema ambacho kitajiuza.