Wiki iliyopita Serikali imezindua Awamu ya Pili ya Mradi wa Mabasi ya Mwendo Kasi ( DART). Awamu hii sasa itakuwa ni ya upanuzi wa Barabara ya Kilwa kwenda Mbagala. Tanzania ni moja kati ya nchi tatu barani Afrika ambazo zina mradi wa aina hii. Nchi nyingine ni Nigeria na Afrika Kusini. Nchi ya Zimbabwe imetuma ujumbe wake kuja hapa kwetu kujifunza.

Sisi tunaipongeza Serikali kwa ufanisi huu wa hali ya juu. Ni kweli kuwa mradi wa Mabasi ya Mwendo Kasi, ukiacha sura ya jiji, umepunguza adha ya usafiri kwa baadhi ya watu. Kwa wanaotumia mabasi haya muda wa safari umepungua kwa kiasi kikubwa na usumbufu umeondoka. Hata maegesho ya magai mjini yameacha kuwa ya tabu kwani watu wengi sasa wanatumia mabasi haya.

Tunaamini kufunguliwa kwa njia ya Mbagala na baadaye Ali Hassan Mwinyi na Nyerere, itakuwa ukombozi. Wafanyakazi wengi watasafiri kwa starehe na msongamano wa magari utapungua. Hata hivyo, mradi huu unazo changamoto kadhaa. Tunaamini yapo mambo yanayostahili kuboreshwa kwa nia ya kuongeza ufanisi.

Tunaamini Barabara ya Morogoro ilikosewa katika ujenzi wake. Barabara hii ina kona nyingi na imekuwa nyembemba. Tunaamini kosa kama hili halitafanyika wakati wa kujenga Kilwa Road. Kona zinapokuwa nyingi zinachangia ajali kuongezeka. Pia Barabara ya mwendokasi imegeuka adhabu kwa watumiaji wengine wa barabara wenye magari.

Kwa sasa ukiwauliza polisi barabara hii imekuwa chanzo chao kikuu cha faini. Barabara hii imeziba njia nyingi za kutokea au kuingia katika barabara kwa anayetoka barabara za mchepuko. Tunaamini si haki kuwatesa wananchi kwenda umbali mrefu wakati tungeweza kutanzua tatizo hili kwa kujenga barabara za maghorofa kila yalipo makutano ya barabara badala ya ilivyo sasa.

Utaratibu wa kujenga flyover kila yalipo makutano utasaidia kupunguza upotevu wa muda kwa madereva wa magari mengine, utasaidia kuepusha ajali zisizo za lazima, lakini pia Mwendo Kasi zitakuwa Mwendo Kasi kweli badala ya sasa zinapofunga breki kila kituo chenye taa na kupoteza muda mwingine.

Mwisho, tunasema Serikali iruhusu ushindani kwa kuruhusu kampuni nyingine kadhaa kununua magari yenye viwango sawa na haya ya mwendokasi na kuyaingiza katika barabara hizo zinazojengwa kwa kodi zetu. Tayari baadhi ya watumishi wa kampuni inayoendesha sasa huduma hii wameanza kugeuka miungu watu. Wanawanyima wateja chenji za Sh 50, lugha zao baadhi si za kiungwana tumerejea kwenye zama za “mtakuja.”

Hata hivyo, tunasema upungufu huo mdogo ukiundolewa, Serikali imefanya jambo la maana kuleta mabasi haya ya Mwendo Kasi na ni suluhisho la kudumu kwa usafiri wa mjini yakichanganywa na treni za chini ya ardhi siku za usoni. Mungu ibariki Tanzania.