Neno ‘mheshimiwa’ limekosa heshima inayokusudiwa. Ni tatizo linalotokana na ukarimu mkubwa uliopo Tanzania uliosababisha kuwapo kwa idadi kubwa ya ‘waheshimiwa’ wa kila aina.

Kwenye kamusi neno hilo lina maana ifuatayo: “neno la heshima linalotamkwa kabla ya kutaja jina la mtu maarufu…” Na mtu maarufu ni nani? Ni mtu anayejulikana kila mahala, au mwenye sifa za kujulikana sana.

Maana isiyo rasmi ambayo inaibuka linapotamkwa neno ‘mheshimiwa’ lakini ambayo hatuitafakari sana ni kuwa tunatarajia huyo anayetajwa kuwa ni mtu ambaye kwanza, anaheshimika mbele ya jamii, na kwa sababu hiyo tunatarajia kuwa atakuwa mtu ambaye anatambua heshima hiyo na anailinda. Kwa kifupi, yeye mwenyewe anajiheshimu. Uzoefu unadhihirisha kuwa siyo wote tunaowaita waheshimiwa wanajiheshimu.

Kwa mila na tamaduni zetu, upo utaratibu wa kupambanua miongoni mwetu umuhimu wa watu mbalimbali ndani ya jamii ambao tunatambua hadhi na heshima yao kabla ya kutajwa majina yao, au kutumia hiyo hadhi na heshima kama mbadala wa majina yao. 

Na mila hizi tunajifunza mapema sana kwenye familia. Baba na mama siyo majina tu yanayowatambulisha kama wanafamilia, lakini la muhimu zaidi, ni majina ambayo kila tunapoyatamka yanageuka pia kuwa kielelezo cha hadhi na heshima ambayo watoto tunawapa wazazi. Kwenye baadhi ya hizi mila na desturi hata kutaja tu majina ya wazazi ni marufuku kwa watoto.

Tukiingia kwenye jamii, yapo maeneo ambayo taratibu za kitaasisi zinashabihiana na zile za mila na desturi. Mojawapo ya maeneo haya ni taratibu za Mahakama.

Jaji au hakimu, au afisa wa Mahakama mwenye jukumu la kusimamia utekelezaji wa sheria anabeba wajibu mkubwa. Anapoingia mahakamani tunasimama. Akiwa mahakamani hatuongei mpaka atoe idhini. Tunafanya hivyo kutokana na wadhifa anaosimamia: usawa na haki kwa wale wanaofikisha shauri mahakamani. Wadhifa ule unahitaji jamii impe kiwango fulani cha heshima ndani na nje ya Mahakama.

Jamii pia ina wajibu wa kumpa kila nyenzo kumuwezesha kutunza na kulinda heshima yake ndani ya jamii. Wanaofahamu historia ya uanzishwaji wa klabu ya viongozi (Leaders’ Club) iliyopo Dar es Salaam wanaeleza ilikusudiwa kuwa ni sehemu ambapo viongozi wangeenda kufuata burudani mbalimbali, lakini wakiwa wamepewa kinga fulani na Taifa kulinda heshima na hadhi yao kwa jamii. Siyo rahisi kupigana vikumbo na mheshimiwa mitaani, halafu ukasimama mbele yake na kuipa taasisi anayoongoza heshima inayostahili.

Kwa hiyo, kwa namna fulani, kutambua uheshimiwa rasmi wa mtu ni njia mojawapo ya jinsi jamii inavyotambua na kulinda hadhi na heshima ya huyo mtu kwa manufaa ya wengi.

Kama binadamu, jaji au hakimu au kiongozi ambaye tunakubaliana anastahili hiyo heshima, ni mwenzetu, lakini kwa jukumu analobeba siyo mwenzetu.

Tukitoka kwa watumishi wa Mahakama tunaweza pia kutaja viongozi mbalimbali ndani ya jamii ambao nao wanabeba majukumu ambayo tunatarajia yatawasukuma wajiheshimu, na pia kustahili heshima ya jamii. Lakini kwenye kundi hili la pili si ajabu kutokea malumbano juu ya nani anastahili uheshimiwa na nani hastahili.

Na hata wakati tukiendelea kulumbana, tunashuhudia pia ni jinsi gani ule ukarimu niliogusia wa Watanzania unavyogeuza uheshimiwa kuwa stahili ya kila mtu, na kusababisha idadi kubwa ya waheshimiwa nchini. Kama ipo haja ya kuipa fasili rasmi ya neno lenyewe heshima inayostahili, basi ipo haja pia ya kupunguza mlolongo wa watu ambao tunawaita waheshimiwa. Iwapo ‘mheshimiwa’ ni utambulisho rasmi ambao tunawapa viongozi kama majaji na mahakimu, unaweza kutokea mkanganyiko tunapotumia neno hilo holela.

Kwangu mimi si neno lenye tofauti sana na neno ‘daktari.’ Madhumuni ni kupambanua kuwa ametajwa mtu ambaye ana nafasi ya pekee ndani ya jamii, nafasi ambayo inaweka mipaka na majukumu mahususi juu ya mahusiano yake na wanajamii wengine.

Nakiri kuwa wengi ya wanaoitana ‘mheshimiwa’ wanafanya hivyo siyo kwa kutaka kumpachika mtu cheo asichostahili, lakini ni mazowea tu yaliyojitokeza, kama vile watu wengine wanavyoitana ‘dokta’ au ‘profesa.’

Kwangu naona bado ipo hitilafu kwa matumizi ya lugha kwa mtindo huu. Unapozingatia wapo watu wawili, mmoja akiwa anahukumu kesi na mwingine akiwa mtuhumiwa katika kesi hiyo, halafu wote wawili uwataje kuwa waheshimiwa, inakuwa ni makosa makubwa ya matumizi ya lugha. Bila shaka inaweza kujengwa hoja pia kuwa itakuwa ni kitendo cha kudhalilisha Mahakama.

Tuseme: “Mheshimiwa Marwa kamhukumu Mheshimiwa Madaraka kifungo cha miaka mitano gerezani kwa kosa la kukutwa na bangi?” Halafu tuone ni sawa? Haipendezi hata kidogo.

Wakati mwingine matumizi yasiyo rasmi ya lugha yakianza kutumiwa na watu wengi yanakubalika na kuwa matumizi rasmi. Maana yake ni kuwa kama matumizi ya aina hii yakiendelea, basi katika enzi zijazo inawezekana kabisa kuwa hakimu na mhalifu wakatajwa kama waheshimiwa.

Naamini kuwa tumejenga desturi ya kuamini kuwa ilimradi tu jambo halijatajwa hadharani, basi jambo hilo halipo. Ni kama vile mtu hawezi kuheshimika bila kuitwa mheshimiwa. Na si ajabu basi kusikia baadhi ya watu kujitambulisha wao wenyewe kwa kujiita waheshimiwa.

Kwa maoni yangu iko haja ya kurudia tena kuitana ndugu, ingawa wengi wanaamini undugu unahusiana na siasa ya Ujamaa peke yake. Turejee maneno ya Rais Benjamin Mkapa alipozungumza kwenye semina ya Mwafaka ya Vyama vya Siasa, Zanzibar, tarehe 7 Machi 2005: “Ndugu siyo neno la kiitikadi tu, linahusu pia utamaduni wetu. Mtaniwia radhi nikiwaita “Ndugu wanasemina.”