Bunge hili la kitaifa linajulikana kama Bunge la 11 (eti mimi nalihesabu kama Bunge la 12, kadiri ya kumbukumbu zangu, nilivyoonesha kwa miaka). Ni Bunge la wasomi na ni Bunge la mkato (cross-cutting Parliament) kwa kuwa limejumuisha wabunge wa rika mbalimbali hapa nchini. Hebu ona wabunge wenye umri mdogo kuanzia miaka 21-35 vijana wapo jumla 47, wabunge watu wazima kuanzia miaka 36-50 wako 112, na wabunge wale wanaoelekea uzee kuanzia miaka 51 na kuendelea wako 91. Hapo tumepata wabunge wetu 250 wanaotuwakilisha majimboni yaani wa kuchaguliwa katika majimbo. Hao ndiyo hasa sauti za wanyonge kutoka wananchi waliopiga kura tarehe 25 Oktoba 2015. Inajulikana wapo wajumbe wa Viti Maalumu, na wapo wateule wa Rais pia katika Bunge hili la 11.

Mimi nataka kuonesha tu kuwa sauti zetu tuliopiga kura ndio hao 250. Bunge lina damu changa ya kutosha na lina watu wazima lakini wazee acha tulie tu hatumo! (hapa wazee ni kuanzia miaka 60 na kuendelea).

Tumaini la Taifa hili kwa Bunge hili lenye wasomi lukuki, lenye Baraza la Mawaziri maprofesa, madaktari na wengineo wenye shahada za kwanza, stashahada na vyeti vya elimu ya juu, litaleta sura ya faida za elimu. Hapo wasomi wetu waoneshe uwezo wao wa kutoa hoja na kuuliza maswali yenye akili. Wasipoteze muda wa vikao vya Bunge hili kwa vijambo visivyosaidia maendeleo ya nchi (trifle questions). 

Aidha wasomi wetu hawa wasijitafutie umaarufu kwa kuomba miongozo ya Spika au kutega Serikali hali wakijua muda ni thamani sana (time is money). Basi ieleweke tu kuwa umaarufu wa mtu unatokana na hoja zenye nguvu na wala umaarufu huo haupatikani kwa uchochezi na vurugu, migomo na zomeazomea ndani ya Bunge. Huko ni kupoteza muda. Siyo dalili nzuri ya msomi mzalendo. ‘Surplus energy’ zetu zinufaishe Taifa nilivyoelezea hapo juu na wala zisilete majanga humo bungeni. Ni Bunge la hadhi ya juu sana hili.

Huko nyuma, miaka lie ya 1970-1980 katika radio kulikuwa na kipindi kilichoitwa “Mazungumzo Baada ya Habari’. Haya ama yalisomwa na David Wakati au na Paul Sozigwa na baadaye yakaja somwa na Abdul (Barker). Kuna hili jambo la ukosoaji wa siasa ile ya Ujamaa na Kujitegemea na maisha ya Vijiji vya Ujamaa. Basi simulizi moja ilienda hivi (kwa kadiri ninavyokumbuka leo hii). Bwana Juma alikuwa mbunge, na alikuwa mstari wa mbele kukosoa mipango ya Serikali. Lakini alikuwa mcheza mpira katika timu ya viongozi wa Bunge. Ni mlalamishi na mkosoaji au mzomeaji sana pale wachezaji wenzake wawapo kiwanjani. Siku ya siku, palikuwa na mchezo kati ya Wabunge na Mabalozi, Uwanja wa Taifa. Mgeni rasmi alitokea kuwa Mkuu wa nchi. Basi mchezo ulipoanza yule mheshimiwa alikuwa benchi hakupangwa kuanza kucheza.

Tujuavyo mchezo wa wazito hawa huwa una vioja, vichekesho vingi na kosa kosa nyingi. Mbunge Juma alisikika sana akikosoa kila wenzake walipokosa kuupiga mpira. Mara akebehi, “tazama lile hata kukimbia haliwezi”. Funga hapo wewe, vipi bwege sana wewe. 

Kocha akaamua kumwingiza uwanjani Bwana Juma na kupumzisha mmoja wa wabunge wenzake aliyechoka. Kule kuingia tu, kwa vile alikamia kuonesha uhodari wake hadharani, basi mpira ulipomjia akaurukia kwa nguvu na kupiga teke la kudhamiria hasa. Masikini, akaukosa mpira ule, kwa kuwa alitumia nguvu sana akaanguka vibaya na akaumia.

Ilibidi abebwe kwa machela kutolewa pale uwanjani. Wote watazamaji, wachezaji wenzake na hata mgeni rasmi, wakabaki kuduwaa na kushangaa. Chepi, mheshimiwa, akiwasakama wenzake mbona hakuchukua hata raundi kiwanjani? Huo mpira wenyewe hakuugusa! Jamani, kweii kwa mwenzako unaona rahisi ikiwa kwako nongwa. Aliaibika na kuzibwa domo lake. Funzo hapa ni kwamba tusiwe wepesi kuona upungufu wa wengine. Sisi wenyewe katika nafasi namna ile tungefanikiwa kweli? Tupime na kufikiri kabla ya kukosoa ya wenzetu”.

Mazungumzo mengine yalihusu kada wa TANU ambaye hakubahatika kuteuliwa katika ngazi ya utawala serikalini. Kila penye vikao vya chama yeye alikosoa watendaji wa Serikali wasivyojali wananchi. Ikaja habari upepo ukamwangukia, akateuliwa Mkuu wa Wilaya fulani hapa nchini. Bwana yule kwa furaha na kiherehere alichokuwa nacho akaenda na mawazo lukuki. Atafanya hivi, atabuni miradi hii, atatembelea kata zote kuhimiza maendeleo na kadhalika.

Siku chache tu baada ya kuwasili wilayani, kijiji fulani kikakumbwa na njaa. Akaenda huko kuona namna ya kuwahudumia waathirika. Kabla hajarejea makaoni pake akaletewa ujumbe, kijiji kingine upande mwingine kumezuka gonjwa la kipundupindu na anatakiwa aende na waganga na madawa. Maskini DC mpya mweye mipango kibao akachanganyikiwa akasema, “kama U-DC wenyewe ni huo wa kusumbukia majanga tupu mimi siutaki”. Akabwaga manyanga akaachilia mbali kazi yenyewe, alifikiri utawala ni lele mama.

Nimekumbusha mazungumzo haya ya baada ya habari enzi zile za utawala wa chama kimoja. Maelezo yote yalilenga kuelimisha wananchi wasikilizaji kuwa kukosoa ni rahisi, kila mmoja anaweza. Lakini kujenga hali ya utulivu kuleta maendeleo katika nchi ni kazi ngumu sana. Wale wabunge niliowasema walikuwa wakosoaji mashuhuri bungeni nyakati zao, baadhi yao leo hii wako hoi lakini sijui hali za maisha yao zikoje.

Baadhi ya viongozi wa upinzani mahodari wakiwa bungeni kukosoa mipango ya sera za Serikali leo hii wako benchi wanaugulia majeraha ya kukosa ubunge au fursa walizotarajia na hivyo hawana tena ile nafasi ya kutoa mipasho yao, wanabaki kulaumu chini chini tu, na tumekandamizwa kwa kukosekana demokrasia halisi katika nchi hii. Wanadiriki hata kulaumu chama chao cha siasa eti hakuna demokrasia ndani ya vikao vyao. Kuna vitisho na ubabe. Tuwaulize hayo unayaona leo ulipokosa kuteuliwa?

Upinzani mzuri ni ule unaokosoa huku ukiwa na mpango kamili ya sera mbadala ya maendeleo ya Taifa. Kwa maana hiyo bungeni panakuwa na mawaziri wa Serikali kivuli (shadow government with its shadow Cabinet). Endapo Serikali iliyoko madarakani itaondolewa kwa kile kinachojulikana kuwa wabunge hawana IMANI nayo (by vote of NO CONFIDENCE) mara moja upinzani wanachomoza na kutekeleza sera zao. Mpango namna huo ndiyo unaojulikana kama Serikali mngojea – (government in waiting). Mambo hayaanzi upya kwa kufumua kila kilichojengwa na ile Serikali iliyoondolewa (voted out government). Wao wanajenga pale wenzao walipoboronga ilimradi kufanikisha maendeleo ya nchi yao.

 

>>ITAENDELEA