Waandishi wa habari hutakiwa wazingatie miiko na maadili ya uandishi wanapofanya kazi zao.
Baadhi ya mambo wanayotakiwa kuyazingatia ni kuhakikisha wanatenda haki sawa kwa wanaowaandika.
Kwa maneno mengine ni kwamba wanatakiwa watoe fursa ya kusikiliza kila upande unaoguswa kwenye habari husika.
Jambo jingine, hutakiwa wasifanye kazi zao kwa upendeleo; na kwa kweli hutakiwa ‘wasiingie’ kwenye habari wanazoandika au kuzitangaza.
Mara zote mwandishi wa habari hutakiwa asiweke maoni yake binafsi kwenye habari; isipokuwa tu pale anapokuwa akiwasilisha maoni yake kupitia makala. Ndiyo maana kukawapo safu kama “Wazo Binafsi”, na kadhalika.
Maadili au miiko ya uandishi wa habari-kwamba inaanzia na kuishia wapi- bado ni mijadala mkubwa miongoni mwa wanahabari duniani kote.
Hivi karibuni, nikiwa na wanafunzi wenzangu wa Sahada ya Mawasiliano ya Umma, mjadala huu ulitawala. Nikaombwa nieleze uzoefu wangu kwenye suala hili.
Hapo nikalazimika kurejea tulichokifanya mwaka 2008. Mwaka huo nilikuwa sehemu ya wanahabari tuliokwenda Comoro kuripoti habari za vita iliyoongozwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) dhidi ya vikosi vya Kanali Mohamed Bacar, katika Kisiwa cha Anjouan.
Tulifika Moroni. Hapo tukapokewa na Kanali Methew Sukambi (sasa ni Brigedia Jenerali).
Alituita, akatueleza mambo haya: “Karibuni vitani. Hapa mmekuja kama Watanzania, na hii Operesheni inaongozwa na Watanzania. Kwa hiyo tunatarajia uzalendo wetu. Mkifanya kazi yenu vizuri tunaweza kushinda vita hii hata bila kurusha risasi.”
Maneno yale ya Afande Sukambi yalikuwa na maana kubwa kwetu. Yalitutaka tufanye kazi kama Watanzania kwa ajili ya Watanzania na Wacomoro.
Lugha aliyoitumia ilikuwa ni innuendo tu lakini angeweza kutumia maneno makavu akatuagiza hivi: “Wekeni miiko na maadili ya kazi yenu pembeni.”
Hapo ndiko uliko mjadala kwa wanahabari sehemu nyingi duniani. Wapo wanaoamini kuwa maadili au miiko ni kitu kinachoweza kubadilika kulingana na mahitaji ya wakati uliopo kwa sababu; tofauti na Maandiko Matakatifu, miiko au maadili ni vitu vinavyoweza kufungwa na kufunguliwa kadri inavyowezekana.
Hao wanapingana na wale wanaoamini kuwa miiko au maadili ya kitaaluma hayana budi yatekelezwe muda wote.
Wale wanafunzi wa shahada ya mawasiliano nikawaambia kuwa mimi ni kati ya wale wanaoamini kuwa maadili ya uandishi wa habari yanaweza kutekelezwa au kutotekelezwa na waandishi wa habari kulingana na tukio au mahitaji ya wakati na jamii.
Maadili yanamtaka mwandishi asipendelee wala kuuficha ukweli! Fikiria, nchi yake iko vitani. Majeshi ya nchi yake yanapigwa na hata kupoteza mamia ya askari. Je, ni busara mwandishi kuandika au kutangaza: “Majeshi yetu yamelemewa”? Habari ya aina hiyo inamshawishi mwananchi au askari gani zaidi wajitokeze kukabiliana na adui? Hapo unaona kuwa hiyo habari itaibua woga/hofu kwa askari na kwa wananchi.
Lakini habari hiyo hiyo, ikipindwa (kwa maslahi ya nchi) na kusomeka: “Majeshi yetu yasonga mbele”, nani ataingiwa hofu?
Tena basi, maadili yanasema mwandishi haruhusiwi ‘kuingia’ kwenye habari; lakini hapo juu kuna neno “majeshi yetu”. Mwandishi anaporipoti habari za nchi yake iliyo vitani, mara zote ametakiwa awe sehemu ya mapambano. Ingawa bado upo ubishi wa kitaaluma, walau wengi wanakubaliana na dhana ya mwandishi kuuvaa uzalendo pindi nchi yake inapokuwa katika vita.
Maudhui ya hoja yangu leo ni kujaribu kujadili maoni ya baadhi ya watu wanaowaona wanahabari wa Tanzania kama watu waliokengeuka wakati huu kwa kuamua kumshabikia wazi wazi Rais John Magufuli.
Tayari lawama zimeanza huku na kule. Kwenye mitandao ya kijamii kuna lawama na utetezi kutoka kwenye makundi yanayosigana juu. Mimi nawatetea wana habari walioamua kuweka kando miiko au maadili na kusimama katika kweli.
Kinachofanywa sasa na Rais Magufuli, ni kama kuongoza vita ya ukombozi ili kuipata Tanzania mpya.
Hiki anachokifanya hakina tofauti na vita. Rais Magufuli amegusa maslahi ya wezi na majahili. Ingawa hao majizi na majahili si wengi kuizidi idadi ya wananchi wanaomuunga mkono, bado uchache wao si kigezo cha kuwafanya wananchi wasiamini kuwa wapo kwenye mapambano.
Ukombozi wa nchi unafanywa na wananchi wote. Wasioshiriki ukombozi wa aina hii ni wasaliti. Mtanzania aliyejua Tanzania namna ilivyotafunwa kwa miongo kadhaa hawezi kusita kumuunga mkono jemedari anayeongoza mapambano haya ya ukombozi mpya wa Taifa letu.
Haya ni mapambano ya kuijenga Tanzania mpya. Anachofanya Rais Magufuli, na timu yake ni kuirejesha Tanzania mikononi mwa Watanzania. Kumuunga mkono kiongozi wa aina hii si jambo la kukiuka maadili, isipokuwa ni kutekeleza wajibu wa msingi wa kushiriki kuijenga Tanzania mpya.
Wapo wanaosema ni mapema mno kumsifu Rais Magufuli. Sawa, mwezi mmoja katika safari ya miaka mitano si kitu! Pamoja na hoja hiyo, walau basi asifiwe kwa haya aliyoyatenda ndani ya kipindi kifupi kabisa.
Tanzania imeanza kuangaziwa nuru mpya. Nchi inarejeshwa kwenye reli baada ya kuondolewa kwa muda mrefu. Yeyote anayeitakia mema nchi yetu hatakuwa na kazi nyingine, isipokuwa kumuunga mkono Rais Magufuli.
Walimwengu wanamzungumza Rais Magufuli. Wanahabari, sehemu mbalimbali duniani wanamsifu. Kama wao wanafanya hivyo, iweje sisi wenye tushindwe kuona kazi nzuri anayoifanya? Mfumo wa kitaasisi wanaotaka Rais Magufuli, aujenge, bila shaka ataujenga. Watanzania walichokitaka kwanza ilikuwa kuwa na kiongozi mwenye maono na dhamira ya kweli. Mambo mazuri kwa kawaida huanzishwa na mtu mmoja au watu wachache. Huyo mmoja na wenzake wachache tumeshawapata. Kinachofuata sasa ni kujenga mfumo imara kwa ustawi wa nchi yetu. Zama za kulaumu wageni zimepita. Wenye makosa ni sisi wenyewe. Hatuna Rais Mzungu, hatuna Waziri wa Fedha Mhindi, hatuna mkubwa yeyote serikalini asiyekuwa mwenzetu. Wizi wote unaotokea kwenye benki na kwenye rasilimali za nchi hii ni matokeo ya udhaifu wa Watanzania wenyewe.
Mwaka 1962 Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, aliandika kitu ambacho hakipo mbali na ukweli wa mambo tunaouona sasa.
Katika kitabu cha TUJISAHIHISHE, sehemu ya maandishi yake, Mwalimu alisema: “Siku hizi, tumeanza kutumia majibu mengine rahisi, mambo yakienda mrama, badala ya kutumia akili zetu na kutafuta sababu za kweli, tunalamu Wazungu, au Wahindi, au ukoloni, au ukoloni-mpya, au vibaraka n.k. Yawezekana kweli kwamba kosa ni la Wazungu, au Wahindi, au ukoloni, au ukoloni-mpya, au vibaraka n. k.-lakini yafaa akili ifikie jibu hilo baada ya uchaguzi wa kweli, siyo sababu ya uvivu wa kutumia akili! Uvivu wa kutumia akili unaweza kufanya tutumie dawa kuondoa matatizo ambayo si ya dawa hata kidogo. Nikienda kwa mganga anitibu maradhi yangu, namtazamia kuwa kazi yake ya kwanza ni kujua hasa, siyo kwa kubahatisha, naumwa nini; kazi yake ya pili ni kujua sababu ya ugonjwa wangu; kazi yake ya tatu ni kujua dawa ya ugonjwa wangu. Daktari asipojua ugonjwa wangu na sababu zake hawezi kujua dawa yake. Akinipa dawa nikapona, atakuwa kaniponya kwa bahati tu, kwa desturi daktari wa namna hiyo hawezi kumponya mgonjwa, na ni daktari wa hatari sana.
“Kadhalika, chama ambacho nia yake ni kuwa daktari wa matatizo ya jumuiya hakina budi kiwe na tabia ya kujua matatizo yenyewe, sababu za matatizo hayo, na dawa yake. Bila kujua matatizo na sababu za matatizo hayo hakiwezi kujua dawa yake.”
Rais Magufuli, ameingia madarakani akitambua ugonjwa unaoikabili Tanzania, anajua sababu za ugonjwa huo; na kwa kweli dawa yake ameijua.
Wakati huu anaoanza kugawa dozi ili kuiponya Tanzania, si busara miongoni mwetu kujitokeza kumkwaza, kumbeza au kutompa nafasi ya kufanya uponyaji aliokusudia.
Wana habari kama sehemu ya Watanzania, nao wana haki ya kumuunga mkono Rais Magufuli, hata kama kufanya hivyo kutaonekana ni kuvunja miiko au maadili ya kazi zao. Nchi inapokuwa vitani, kila raia mzalendo anakuwa sehemu ya jeshi la kuleta ushindi.