Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema. Ni jambo la kushukuru sana. Wakati tulipopata uhuru mwaka 1961 nchi yetu iliitwa Tanganyika, lakini baada ya kuungana na Zanzibar Aprili 26, 1964 ikajulikana kama Tanzania.
Kabla ya utawala wa Waingereza eneo la Afrika Mashariki, zikiwamo Burundi, Rwanda, Tanzania Bara na Buganda; kuanzia mwaka 1885 hadi mwaka 1919 yalikuwa chini ya utawala wa Wajerumani na kujulikana kama “Deutsch-Ostafrica”.
Wakati wa Vita ya Kwanza ya Dunia, majeshi ya Waingereza –Royal Navy na wanajeshi wa ardhini kutoka Uingereza na India (British Indian infantry) yalipambana na Wajerumani na kuwazidi nguvu; hivyo mwaka 1916 Waingereza wakaanza kukalia ardhi yetu na waliendelea kuwapo hadi Vita ya Kwanza ya Dunia ilipomalizika mwaka 1918. Baada ya vita hiyo kukaundwa chombo kidunia kilichoitwa The League of Nations, ikiwa ni jitihada ya kutafuta amani duniani.
Kupitia chombo hicho Waingereza walikabidhiwa madaraka ya kusimamia Tanzania Bara. Ilipofika mwaka 1922 Waingereza wakaanza kusimamia rasmi, lakini wakifahamika kama waangalizi na ndipo jina la Tanganyika likaanzishwa. Kabla na baada ya Uhuru mwaka 1961, hali na afya ya misitu ya asili (forest health) ilikuwa nzuri sana.
Kwa upande mwingine hata tangu kuwa chini ya utawala wa wakoloni Wajerumani mwaka 1891 na Waingereza baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia hatujawahi kuwa na takwimu kamili zinazoonyesha eneo kamili la misitu ya asili nchini ni kiasi gani. Kwa mfano, kwa miaka ya nyuma imekisiwa kuwa eneo la misitu nchini ni kati ya asilimia 34 na 48 ya ardhi yote ya Tanzania Bara; asilimia 90 ikiwa ni misitu aina ya miombo.
Vilevile asilimia 37 ni eneo lenye misitu iliyohifadhiwa kisheria. Takwimu zilizotolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii mwaka 2015 zinaonyesha kuwa eneo lenye misitu ya asili na mashamba ya miti ni hekta milioni 48.1 (zaidi ya asilimia 50 ya eneo lote).
Pamoja na kuonekana kuwa Tanzania tunayo misitu ya kutosha, matumizi yake yamekuwa si endelevu. Miti mingi inakatwa sana hasa kwa kupata mbao, nguzo na mkaa. Wengi wetu tukiona msitu, kinachotujia akilini ni miti gani inafaa kwa mbao.
Hata wataalamu wa misitu mafunzo yetu yalielekea zaidi kusimamia misitu kwa minajili ya kuzalisha mbao (timber). Hivyo mkazo ulielekezwa zaidi kwenye mashamba ya miti na sana sana miti ya kigeni (pines, cyprus na mikaratusi). Wataalamu tukapikwa zaidi kushughulikia mashamba ya miti kwa kutupatia utaalamu wa kutosha tangu mbegu, kupanda miti, kuitunza hadi inapofikia umri wa kuvunwa.
Kutokana na hali hiyo, misitu ya asili ilionekana kutopewa umuhimu na hali imekuwa hivyo tangu ukoloni hadi leo. Mtazamo ni ule ule. Wakati wa ukoloni Wajerumani na Waingereza walihifadhi baadhi ya maeneo ya misitu kisheria. Lakini mkazo wao uliwekwa zaidi kuanzisha mashamba ya miti kwa misingi ya kupata miti inayofanana na rahisi kutunza ili kupata mbao nyingi kwa wakati mmoja na kuingiza fedha nyingi kupitia viwanda vya misitu.
Misitu ya hifadhi ilianzishwa, lakini haikupewa kipaumbele kwa matunzo kama ilivyokuwa kwa mashamba ya miti. Ndiyo tukawa na maeneo mengi ya misitu ya hifadhi kwa nadharia zaidi kuliko vitendo. Wakati tukikazania kuimarisha mashamba ya miti, uvunaji wa miti ya asili uliendelea kwa kasi sana na kwa vile hatukuwa makini kusimamia, hali imekuwa mbaya mno.
Aina za miti iliyokuwa maarufu kwa mbao hapa nchini na nchi za nje kama mivule, mininga, mipingo, mipangapanga na baadhi ya miombo ikavumwa sana. Sasa hali ni mbaya. Tangu Uhuru hatukuwa na mkakati wa kuanzisha mashamba ya miti ya asili.
Kiuhalisia ule mtazamo wa: “Ningefanya hivi au vile hili lisingetokea au lisingenipata” huwa inakuja wakati tatizo limejitokeza. Sasa aina za miti ya asili yenye manufaa kwa binadamu na utunzaji wa mazingira hapa nchini imo hatarini kutoweka.
Hata hivyo, hali haijawa mbaya kiasi cha kutukatisha tamaa. Bado tunayo nafasi ya kuirejesha miti ya asili kwenye uhalisia wake. Tutaweza kufanya kweli kupitia mbinu za kitaalamu na kisayansi kutokana na matokeo ya tafiti kwenye misitu ya asili na kutoa matokeo chanya.
Sasa wataalamu wa misitu “mpira umo miguuni mwetu” – sisi ndiyo timu shupavu inayotakiwa kuleta ushindi kwa Watanzania. Hivyo tujizatiti ipasavyo tuhakikishe aina za miti ya asili zilizo hatarini kutoweka tunazirejesha. Tufanye kila linalowezekana kuanzisha mashamba ya miti kama mivule (milicia excelsa), mininga (pterocurpus angolensis), mipingo (dalbergia melanoxylon), mkangazi (khaya anthotheca) na aina nyingine inaendelea kuwapo.
Wataalamu wetu kwa nyanja zote, hasa wenye elimu mimea na biolojia na “tree-breeders” tuhakikishe miti ya asili haipotei, bali iendelee kuwepo kwa manufaa ya vizazi vyote vya sasa na vijavyo.
Tuanze taratibu, lakini kasi iongezeke kadiri tunavyotekeleza dhima zetu. Nakumbuka miaka ya 1978 na 1979 nikiwa Ofisa Msimamizi wa Mradi wa Shamba la Miti Rondo mkoani Lindi tulianza kufanya majaribio ya kuotesha mivule na mininga. Pia tulianzisha bustani ya miche ya mipingo eneo la Kiwawa, wilayani Kilwa. Baadaye haikuendelezwa.
Sasa ni wakati wa kuweka nguvu kwenye miti asili. Hebu tuanze na aina zenye faida nyingi kiuchumi. Mfano, pamoja na ile ya mbao kuna miti kama misandali (sandalwood – oryris lanceolata) inatumika viwandani kutengeneza manukato na dawa; mikimbo (allanblakia stulmanii) ilikuwa inapatikana sana sehemu za Lushoto.
Kuna miti aina ya amarura (sclerocarya birrea) inafaa sana kibiashara na matunda yake ni chanzo kizuri cha vitamini C na dawa pia. Miti kama hiyo inaweza kuchangia uchumi wa viwanda Tanzania. Tuiwekee mkakati mzuri wa kuiendeleza kwa manufaa yetu sote.
Nawapongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), maana wameanza kulifanyia kazi suala hili muhimu kwa kuanzisha mashamba ya miti ya asili. Kinachotakiwa ni kuongeza nguvu na kuhakikisha utafiti wa makusudi unafanywa kwenye eneo hili ili uoteshaji miti asili uendane na mbinu za sasa za kisayansi.
Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) iwezeshwe na TFS na wadau wengine kwenye tasnia ya misitu na kwa kufanya hivyo tutaweza kufanikisha na kusonga mbele ipasavyo. Hakuna lisilowezeka. Penye nia pana njia.
Mwandishi wa makala hii, Dk. Felician Kilahama ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI). Anapatikana kwa simu: 0756 007 400.