Machi 31 na Aprili Mosi, mwaka huu ni Sikukuu ya Pasaka, ambapo Wakristo duniani wanakumbuka kifo na kufufuka kwa Yesu Kristo.
Kwa kawaida Wakristo hujipanga kwa namna tofauti kusherehekea Sikukuu hii, ikiwa ni pamoja na kuwanunulia watoto zawadi mbalimbali, kukaribishana kula chakula na kufurahi pamoja.
JAMHURI inachukua nafasi hii kuwatakia Watanzania heri na fanaka katika kusherehekea Sikukuu hii muhimu katika imani ya Kikristo.
Pamoja na kuwatakia Pasaka njema, pia tunaona umuhimu wa kuwakumbusha Watanzania wenzetu kuhakikisha wanasherehekea Sikukuu hii kwa amani na utulivu.
Katika sikukuu za hivi karibuni zikiwamo za Krismasi na Mwaka Mpya watu wamejitahidi kuzisherehekea kwa amani na utulivu katika maeneo mbalimbali nchini, ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Matukio ya vitendo viovu vikiwamo vya wizi, ukabaji, ngono haramu na zembe, ajali za barabarani na ulevi wa pombe kupindukia hayakutokea kwa kiasi cha kutisha ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Tungependa kuona hata kipindi hiki cha Sikukuu ya Pasaka hii Watanzania wanakuwa waadilifu katika matumizi ya fedha kuepuka vitendo visivyopendeza katika jamii.
Ingawa Jeshi la Polisi ndilo lenye dhamana ya kuimarisha ulinzi wa raia na mali zao, bado wananchi wana wajibu wa kuhakikisha wajiheshimu kipindi hiki cha Sikukuu na kuepuka kila aina ya vitendo visivyopendeza mbele za Mungu.
Wafanyabiashara mbalimbali nao wanahimizwa kuwa waungwana na kuepuka vitendo vya kuwakomoa wateja wao katika kuwauzia na kuwapatia huduma mbalimbali kuwezesha kila mmoja kufurahia Sikukuu hii ya Pasaka.
Sisi JAMHURI tunawatakia Wakristo na Watanzania kwa jumla heri ya Pasaka njema isiyo na bughudha, tukiamini kuwa kila mmoja atatekeleza wajibu wake katika kuimarisha amani na utulivu.