📌Asema majiko yanayotoa nishati safi ya kupikia ni salama

📌Ataja Wanawake kuathirika zaidi na matumizi ya nishati zisizo safi

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Khamis ametoa rai kwa jamii kuondokana na matumizi ya nishati zisizo safi ili kulinda afya zao.

Khamis ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akihamasisha wananchi kuachana na matumizi ya nishati isiyo safi na kuanza kupika kisasa kwa kutumia nishati iliyo safi.

“Jamii ihamie katika matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kulinda afya na magonjwa, lakini pia majiko haya ya kisasa tunayopikia ni salama.’ amesema Khamis.

Amesema wanawake ndio wamekuwa wahanga wakubwa wa athari zitokanazo na matumizi ya nishati zisizo safi ikiwemo magonjwa ya mapafu.

Ameongeza kuwa, mbali ya athari kwa binadamu, matumizi ya nishati isiyo safi pia husababisha uharibifu wa mazingira kutokana na ukataji wa kuni na mkaa.

Ametanabaisha kuwa, uharibifu wa mazingira unasababisha mabadiliko ya tabianchi ikiwemo upatikana wa mvua zisizo tabirika pamoja na kuathiri vyanzo vya maji ambayo pia yanatumika katika uzalishaji wa nishati ya umeme.