Na Mwandishi Maalum,Tunduru
KILO milioni 19,375,896.00 za korosho zenye thamani ya Sh.bilioni 62,159,126,758.00 zimeuzwa na wakulima wanaohudumiwa na Chama kikuu cha Ushirika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma(Tamcu Ltd).
Korosho hizo zimeuzwa katika minada minne kupitia mfumo wa stakabidhi ghalani chini ya usimamizi wa mfumo soko la bidhaa(TMX) ulioonyesha mafanikio makubwa kwa wakulima kupata soko la uhakika na bei nzuri ya zao hilo.
Meneja Mkuu wa Chama kikuu cha Ushirika wilaya ya Tunduru(Tamcu Ltd) Marcelino Mrope alisema,mnada wa kwanza ulifanyika katika kijiji cha Nakapanya kilo 1,804,369.00 zenye thamani ya Sh.5,792,024,490.00 zimeuzwa kwa bei ya Sh. 3,210 kwa kilo moja.
Mrope alisema,katika mnada wa pili uliofanyika katika kijiji cha Mtina wakulima wameuza kilo 7,543,517.00 zenyethamani ya Sh.23,973,297,026.00 kwa bei ya Sh. 3,178.
Kwa mujibu wa Mrope,mnada wa tatu uliofanyika kijiji cha Airpot kata ya Mbesa, kilo 5,190,191.00 zimeuzwa kwa bei ya Sh.3,212 huku wakulima wakipata zaidi ya Sh. 16,670,893,492.00 na katika mnada wanne uliofanyika tarehe 12 Novemba kijiji cha Ligoma kilo 4,837,819.00 zenye thamani ya Sh.15,722,911,750.00 ziliuzwa kwa bei ya Sh.3,250.
Mrope amewataka wakulima wa korosho, kuhakikisha akaunti zao za benki zinakuwa hai ili kuepusha usumbufu wakati wamalipo kwani baadhi ya wakulima wamekuwa wakipata changamoto ya kutopata fedha kwa wakati.
Alieleza kuwa,katika mchakato wa mauzo ya korosho hadi sasa hakuna usumbufu wowote na wakulima wanapata fedha zao kwa wakati, na wanunuzi wanafanya malipo kupitia Chama kikuu cha Ushirika tofauti na hapo awali ambapo malipo yalipitia kwenye Amcos.
Mrope,amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo yake kutaka malipo ya wakulima yanafanyika kupitia chama kikuu kwani yamerahisisha sana ulipaji fedha za wakulima kutoka siku 14 hadi siku 4 tangu mnada unapofanyika.
“kwa mfano tumefanya mnada leo haizidi hata siku tano tangu mkulima alipouza mazao yake,kwa hiyo tunaona ni maendeleo makubwa sana,lakini tunaomba wasimamizi wetu waendelee kusimamia na kutoa maelekezo pale zinapojitokeza changamoto mbalimbali katika uuzaji na ununuzi wa mazao ya wakulima”alisisitiza Mrope.
Kwa upande wake meneja wa bodi ya Korosho Tanzania Tawi la Tunduru Shauri Makiwa alisema,katika msimu wa mwaka huumazao yote yanayouzwa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani bei yake imekuwa nzuri na kuwapongeza wakulima kwa jitihada wanazofanya mashambani.
Amewasisitiza waendelee kutumia pembejeo kwa wakati ili waweze kupata mavuno mengi na bora yatakayokuwa na bei nzuri, badala ya kutumia pembejeo feki zinazochangia kuwarudisha nyuma licha ya juhudi kubwa wanazofanya mashambani.
Mokiwa,amewashauri wakulima wa korosho kuepuka kuchuma korosho zikiwa juu ya miti badala yake kusubiri hadi zinapodondoka chini na kuhakikisha wanaanika angalau kwa siku tatu hadi nne kabla ya kufikisha ghalani ili kuepuka kuwa na unyevu.
Mkulima wa korosho wa kijiji cha Airpot kata ya Mbesa Ismail Mpepo,amefurahishwa na bei ya korosho mwaka huu kwanihaijawahi kutokea kwa miaka ya hivi karibuni.
Ameishukuru Serikali kwa kusimamia vizuri mfumo wa stakabadhi ghalani uliowezesha wakulima kupata soko la uhakika na bei nzuri, hali iliyohamasisha wakulima wengi kufufua mashamba waliyoyatelekeza kwa muda mrefu.