Kwa muda wa wiki sasa nimekuwa hapa katika Mji wa Tunduma. Mji huu ni mji unaoongoza kwa kuwa na benki nyingi, idadi ya watu si haba na miundombinu yake baada ya kujengwa Barabara ya Tunduma Sumbawanga, si haba. Kwa sasa kuna upanuzi wa barabara unaendelea na maduka yaliyokuwa barabarani yamevunjwa na kusogezwa nyuma, kimsingi unakuwa na sura mpya.
Hata hivyo, kuna jambo kubwa limenishtua. Mji wa Tunduma ulisifika kwa ‘maraha’ ila kwa sasa hali ni tofauti. Mji huu ambao unahudumia mpaka wa Tanzania na Zambia, na kwa jirani unagusa mpaka wa Malawi, kipato chake kinashabihiana mno na cha mji wa Kahama, Shinyanga. Ulichangamka, na ulivutia wageni wengi.
Kuna raia wa Malawi, Zambia, DRC, Msumbiji na nchi kama Zimbabwe waliopiga kambi katika mji huu. Mji wa Tunduma ulichangamshwa kwa kiasi kikubwa na sekta ya usafirishaji. Ardhi zilizoko maeneo ya barabarani ziligeuka lulu. Viwanja vilipanda hadi milioni 80, kwa ajili ya kupata eneo la kuegesha malori. Baadhi ya vijana waliamua kufanya uwekezaji katika yadi za malori na hoteli.
Sitanii, kwa sasa ni kilio. Tunduma ilikuwa na foleni ya kutisha kabla ya kufika mpakani, ila sasa ikifika saa 12 jioni, huoni magari ya transit, malori yenye mzigo wala ndugu yake. Nimepiga baadhi ya picha katika lango la kuingilia mpakani, ni kilio. Saa 11:50 jioni mpakani hakuna lori hata moja linalosogelea lango la kuvuka.
Nimeingia kwenye baa, hoteli, maeneo ya stendi unaona kilio. Nimeingia kwenye eneo linaitwa Black Street, maduka yamejaa bidhaa ila wanunuzi hawapo. Mbao zimepangwa katika maeneo mengi, lakini hakuna wanunuzi. Wananchi waliozoea maisha ya kujirusha, kwa sasa wanalia na kusaga meno. Kuna hoteli, nyumba kadhaa zinauzwa kwa bei ya kutupwa Tunduma.
Wananchi wamejaa hofu. Bidhaa za magendo zimeanza kutamalaki kwa ‘wajanja’ wachache. Hili nitalizungumza zaidi katika makala zangu zijazo. Ukizungumza na watu wengi wanaona giza mbele ya safari. Hakuna mwenye jibu sahihi. Wenye malori walio wengi kwa sasa wanauza malori yao. Wenye ardhi waliogoma kuuza mwaka jana kwa sasa wanajuta kwa nini hawakufanya uamuzi sahihi.
Sitanii, hapa Tunduma mzunguko wa fedha umekatika. Nimetumia usafiri binafsi na usafiri wa umma mara kadhaa. Mazungumzo kwenye magari ni ugumu wa maisha. Mbeya inasifika kwa kuwa wafuasi wa dini. Ni mkoa wenye madhehebu mwengi kuliko mkoa wowote Tanzania. Sasa ukipanda magari ya abiria, wengi wanapiga nyimbo za kumtumainia Mungu. Ni dalili ya kukata tamaa? Tusubiri tuone.
Wakati wakimtumainia Mungu, viashiria vya uhalifu katika mikoa ya Songwe na Mbeya viko juu. Ukabaji umeongezeka. Biashara ya kupigana nondo imerejea Mbeya. Wenyeji wanapata hofu kuwa ugumu wa maisha ulivyo mchezo wa kuchuna ngozi uko hatarini kurejea. Soko la Mwanjelwa mjini Mbeya nao maduka mengi yamefungwa kutokana na ukosefu wa wateja.
Nilichokishuhudia Tunduma na taarifa ninazozipata kutoka sehemu mbalimbali za nchi, Serikali inapaswa kukaa ikawasiliana na wananchi na kupima maisha wanayoishi sasa. Hatari kubwa ninayoiona, ni kuwa kama biashara zinafungwa si muda Serikali itakuwa haina pa kukusanya kodi. Nafahamu kuwa zipo taarifa za uwekezaji katika viwanda na kwingineko, lakini tuwe makini.
Sitanii, tusipojipanga tutajikuta kama nchi tuna taarifa nzuri sana ya uchumi kama ilivyokuwa kwa Ghana mwaka 1962, lakini mapato ya mtu mmoja mmoja ni shida, itakuwa ni shida. Tukichukua utajiri wa wenye viwanda kama Bakharesa tukagawa takwimu kwa Watanzania na kujiridhisha kuwa uchumi umekua (GDP), watu wetu wataishia kilio cha kusaga meno na kupata utapia mlo.
Wakati tukijipanga kujenga uchumi mkuu (macro economics), Rais John Pombe Magufuli chonde chonde usisahau uchumi wa mtu mmoja mmoja (micro economics). Familia zetu zilizo nyingi hazina akiba. Uchumi wetu ni wa mkono kwenda mdomoni. Kama ni kukata mzunguko wa fedha unapaswa kuandaliwa utaratibu wa kufikia hatua hiyo. Nakubaliana na hatua ya kuzibana benki ziende kwa wananchi, ila kibano hiki kisipokuwa na njia ya kutokea, kufa hatufi ila cha moto tutakiona. Tunduma inasikitisha kwa sasa.