Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo -CHADEMA – Bara, Tundu Lissu ametangaza rasmi nia ya kuwania nafasi ya Uenyekiti wa chama hicho Taifa.

Akitangaza nia hiyo jijini Dar es Salaam leo Novemba 12, Lissu amesema amefikia uamzi huo baada ya kubadili msimamo wake wa kuwa makamu mwenyekiti nafasi aliyohudumu tangu mwaka 2019.


“Napenda kuwajulisha rasmi kwamba nimeshawasilisha taarifa rasmi kwa Katibu wa Chama chetu ya kuondoa kusudio langu la kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti na badala yake nimewasilisha rasmi kusudio langu la kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Chama chetu”, amesema Lissu.

Aidha Lissu amesisitiza kuwa upingaji wa nia yake hiyo ya kuwa mwenyekiti wa CHADEMA taifa kwa mtu yeyote ni ukwiukwaji wa katiba ya Chama na kushindwa kuenzi utaratibu uliochwa na waasisi wa chama hicho.

“Kwasababu hiyo mwanachama wa CHADEMA au mtu mwingine yeyote anaeyona ajabu, au anayechukizwa au kukwazwa na uamzi wangu wakutangaza nia ya kugombea uongozi ndani ya chama chetu atakua ama amesahau, au hajui au hataki kuenzi na kue ndeleza urithi tulioachiwa wazee wetu Edwin Mtei na Bob Makani wakuachiana madaraka ya uongozi ndani ya chama kwa njia ya uchaguzi huru na wahaki.”

Ameongeza “Mtu wa aina hiyo anatakiwa kuelimishwa au kukumbushwa juu ya urithi wetu huu, na kwa vyovyote vile asiruhusiwe kutuletea utamadani tofauti katika kubadilishana madaraka na uongozi katika chama chetu.”

Lissu amesema kubadili kwake msimamo wa kuwa makamu mwenyekiti tangu alipoanza kushawishiwa kugombea nafasi hiyo mwaka 2015 kunatokana na mazingira ya siasa ya sasa ambayo amesema yanamuhitaji kiongozi mwenye historia ya uadilifu na kukubalika na jamii.

“Ndugu zangu na wanachama tupo katika mazingira mapya katika siasa za nchi yetu…. Hatua hii ya sasa inahitaji kiongozi mwenye historia ya uadilifu na kukubalika na jamii. Ninapenda kuamaini kwamba historia ya kukubalika kwangu kwa watanzania inajulikana wazi na watanzania wengi,” amesema.

Ameongeza:“Aidha hatua hii ya mapambano ya kidemkorasia inahitji kipngozi aliyeonesha kwa maneno ya katiba yetu kwa tabia na mwenendo wa uzalendo wa kupenda na kutetea nchi yetu”.

Lissu amesema kutokana na utumishi wake wa miaka 20 katika chama hicho na katika umma ni imani yake kwamba ana nafasi ya kukiongoza chama katika mapambano ya kidemokrasia.

Amesema kutokana na chama hicho kukua kwasasa hakuna budi kurudisha tena, utaratibu wa kikatiba wa ukomo wa madaraka katika chama hicho uliokuwepo mwanzo.