Mbunge wa Singida Mashariki wa Chadema, Tundu Lissu amesema dalili zinaonesha watu waliomshambulia kwa risasi mjini Dodoma mwaka jana walikuwa na uhusiano na serikali.

Lissu, akihutubia wanahabari kwa mara ya kwanza tangu kulazwa hospitalini, ameonekana kuilaumu serikali ya Rais John Magufuli kwa kuwakandamiza wapinzani.

Amesema anaamini shambulio dhidi yake lililenga kumnyamazisha kutokana na uokosoaji wake wa mara kwa mara wa serikali.

Lissu alikuwa akihutubu kutoka hospitali ya Nairobi jijini Nairobi ambapo amekuwa akipokea matibabu kwa miezi minne sasa.

Mbunge huyo wa Singida Mashariki ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuingilia kati akisema hali nchini Tanzania imebadilika sana.

Lissu amesema kufikia sasa anaamini hakuna uchunguzi wa maana kuhusu kushambuliwa kwake mnamo 7 Septemba unaendelea.

Aidha, amesema Rais John Magufuli, ingawa aliandika ujumbe kwenye Twitter na pia kumtuma makamu wake Samia Suluhu Hassan, hajawahi kuzungumzia hadharani kisa cha kushambuliwa kwake.

“Tanzania imebadilika na kuwa taifa ambalo hakuna aliye salama. Mawakili wanaweza kurushiwa mabomu kwa kuwawawkilisha wateja wao. Nchi ambayo afisi za mawakili zinaweza kuvamiwa, na mawakili kufungwa jela,” amesema Lissu.

Lissu amesema amepona na kwamba anashukuru Mungu na wote waliomtakia uponaji wa haraka.