Hivi karibuni naona mwelekeo usio na afya kwa taifa letu. Nimewaona polisi wakipiga marufuku mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, nimeona vyama vikitoa matamko ya nia ya kukabiliana, nimesikia baadhi ya vijana ndani ya vyama wakihamasishana kwenda Dodoma kuzuia mkutano wa wapinzani wao na nimeshuhudia Serikali ikizuia mikutano ya Bunge live.
Sitanii, naomba mniruhusu kusema ninachokiwaza. Napata tabu kidogo. Napata tabu kwa maana ya kwamba viongozi wengi wamejaa woga. Viongozi wengi huenda wanampa Rais John Pombe Magufuli taarifa wanazoamini zitamfurahisha. Kuna woga wa hali ya juu katika mfumo. Tusipojitokeza wachache kusema ukweli nchi itapotea njia.
Kwamba tusipojitokeza wachache tukasema mashirika ya umma yanakaribia kufa, na kifo chao kinachokana na ukweli kwamba bajeti zao wengi zimesimama, zimesimama si kwa sababu nyingine bali wameelekezwa wazipunguze na hawajui wapunguze nini na wapi, hii ni shida. Wataalam wengi wako kimya, hawamwelezi ukweli Mheshimiwa Rais, wanadhani ukimya utalinda ajira zao.
Tunajiandaa kuingia kwenye uchumi wa viwanda, ila maandalizi siyaoni. Siyaoni kwa maana kwamba hakuna mpango mahususi wa kubadili sheria 72 zinazohusiana na uanzishaji wa viwanda, ama kwa kuziunganisha au kuziuisha zikarahisisha mazingira ya nchi yetu kuwekeza katika viwanda.
Nimeangalia nchi kama Ethiopia, ambayo kwa sasa ni ya tano duniani kwa kuuza maua barani Ulaya. Nchi hii Waziri Mkuu wake aliyetangulia mbele ya haki, Meles Zenawi alifanya uamuzi wa makusudi mwaka 2,000. Alitangaza nia ya Ethiopia kuipita Kenya katika kilimo cha maua. Aliweka mpango wakatenga ekari hekta 1,000 kwa ajili ya kilimo cha maua.
Si hilo tu, alitenga muda wake kuwa kila mwezi lazima akutane na wakulima wa maua. Walijadiliana kwa saa 2 kila mwezi wamefanikiwa wapi, wamekwama wapi na nini kinawakwamisha. Hatimaye changamoto zilitanzuliwa mwezi hadi mwezi na baada ya miaka mitano tu, Ethiopia iliishakuwa namba tano duniani kwa kuuza maua nje ya nchi.
Sitanii, nchi kama Malaysia, Singapore na Korea Kusini zinazoitwa Asian Tigers, viongozi wao walifanya uamuzi wa msingi. Mfano waliweka utaratibu kuwa fedha za kigeni gharama ya kuzibadilisha itatajwa na Benki Kuu tu (controlled exchange rate). Kwa makusudi wakadhibiti kucheza kwa sarafu zao. Sisi leo kila mwenye duka la fedha (Bureau de Change) anaweza kuamka asubuhi akatangaza anabadili fedha kwa kiwango gani. Ni lazima sasa tuwe na controlled exchange rate inayodhibitiwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Nikiacha hilo la viwanda, nirejee katika ajenda ya uhuru wa kujieleza. Polisi kwa akili za pekee na nzuri walizojaliwa na Mwenyezi Mungu wameota kama marehemu Sheikh Yahya Hussein kuwa kuna watu wanafanya kazi ya kuhamisha wengine wasitii sheria. Sina uhakika iwapo wanayo mifano hai au wameelekezwa! Wakapiga marufuku mikutnao ya siasa.
Nafahamu dhana ya Rais Magufuli. Anataka watu wafanye kazi. Siasa anataka zihamie bungeni huko ndiko washikane mashati tujue mbivu na mbichi. Kwa bahati mbaya, bungeni nako kuna kisiki. Yupo mtu anaitwa Dk. Tulia Akson. Huyu amejipanga anasema liwe jua, iwe mvua yeye yupo kuhakikisha mwenye mawazo tofauti na hisia zake sauti yake haisikiki.
Ukimwacha Dk. Tulia matangazo live ya Bunge ambayo yangewapa wananchi fursa ya kuona wabunge wao wanawawakilishaje nayo yamesitishwa. Kwa kukosa mahala pa kusema, wanasiasa hawa wamedhani ngoja warudi majimboni wakazungumze na wapigakura wao wakiwamo hao polisi, lakini wanaambiwa hali ya hewa si nzuri mpaka itakapotulia.
Kwamba itatulia nini, ni fumbo la imani. Nimetangulia kusema hapo juu kwamba naomba mniruhusu kusema ambayo pengine hamtayapenda. Nchi yoyote duniani inapofika mahala ikadhibiti uhuru wa kutoa mawazo, huo ndiyo unakuwa mwanzo wa mgawanyiko. Ni vyema, na nasisiza, kuwa ni vyema nchi yetu na viongozi wetu tukawa na uvumilivu wa kusikia hata tusiyoyapenda.
Mheshimiwa Rais Magufuli. Hao wanaoitwa wapinzani ni chanzo kizuri mno cha taarifa kwako. Naweza kukuhakikishia kuwa hadi sasa wapinzani wengi wanaunga mkono Serikali yako. Wanaiunga mkono kwa sababu kila walichokuwa wakikisema ni kibovu umekifanyia kazi. Ni bahati mbaya, sijui kama ni wewe umeagiza au la, kwamba sasa huwapi fursa ya kuendelea kukupatia taarifa nyingi muhimu.
Wapinzani wanapofanya mikutano ya hadhara kwa mfano wakasoma taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali hadharani dhidi ya viongozi wa halmashauri walioiba fedha za umma wanakusaidia wawe kutawala raha mstarehe. Nakuhakikishia, ni kwa nadra sana utapata mwana-CCM kindakindaki atakayekuja kwako ‘kumchongea’ mwana CCM mwenzake.
Sitanii, Rais Magufuli jipe muda katika mazungumzo yako na wasaidizi au wana CCM usikilize ni wangapi mnafikia hatua ya kubishana katika suala fulani. Ikiwa unasikia kila unayekutana naye anakwamba: “Ndiyo mheshimiwa… sawa kabisa mheshimiwa… uko sahihi kabisa, kweli kweli mheshimiwa…” tena wakati mwingine wanaongeza na kakicheko ka kinafiki, fahamu wanakupoteza.
Ukiwa Rais wa Tanzania unahitaji kupata mawazo mbadala. Naamini umemwona Rais Barack Obama wiki iliyopita pale mwananchi alipoingilia hotuba yake vijana wa Usalama wakataka kumtia nguvuni, Obama akawazuia, akajibu hoja ya yule kijana, baada ya hapo hata yule kijana aliyekuwa na hasira gubigubi, akaishia kumpigia makofi Obama.
Inawezekana kabisa, watu kama Jenerali Ulimwengu alipowaza kwa sauti pale Chuo Kikuu siku ya Kigoda cha Mwalimu Nyerere, akitaka Rais mstaafu Jakaya Kikwete na wengine wafikishwe mahakamani, tayari umeishapata washauri wengi wanaokwambia Ulimwengu ni UKAWA. Nasikia siku hizi kila mwenye mawazo mbadala serikalini watendaji wako wanamwita UKAWA. Si ajabu hata mimi ninavyoandika hivi (ingawa si dhambi) tayari kati ya wanaosoma jumbe huu yupo anayeniona ni UKAWA!
Sitanii, taifa lenye maendeleo ya kweli linatokana na watu kuelezana ukweli. Linatokana na vyombo vya habari vyenye weledi wa kutosha, vinavyojadili mijadala na kutoa suluhisho. Kwa mfano, ukiniuliza mimi leo nitakwambia polisi walikosea kutoka tamko la kuzuia mikutano ya hadhara bila angalau kutoa mifano miwili ya nia ya uvunjifu wa amaani na hiyo baadaye ya hali kutengamaa itakuwa lini.
Walichofanya polisi ni njia sahihi ya kuijengea chuki Serikali yako kwa wananchi. Wananchi wanajiuliza, imekuwaje huyu Rais Magufuli anayejiamini, aliyeweza kupiga push up jukwaani leo Serikali yake inaogopa maneo? Ingekuwa katika mikutano ya hadhara, tena inayoanza saa 10 jioni, watu wanajiandaa kwenda na fimbo, visu, mapanga na kamba, ningewaelewa.
Kwa upande wa pili pia, nasema vijana wa Chadema (Bavicha) wanakosea. Si jukumu lao kwenda Dodoma kuisaidia polisi kuzuia mkutano wa CCM. Tukiruhusu matendo ya aina hii, ambapo kila mwananchi anaamua kufanya atakalo bila kufuata mkondo wa kisheria, basi tujue tunaipeleka nchi kwenye sintofahamu (anarchy).
Ikiwa vijana hawa wa BAVICHA wanayo hoja ya msingi, Ibara ya 107A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inasema bayana kuwa chombo pekee chenye mamlaka ya kutoa haki ni Mahakama. Muda upo na fursa hiyo ipo. Vijana hawa waende mahakamani kufungua kesi ya kuzuia mkutano wa CCM ikiwa wana hoja. Huo ndiyo utawala wa sheria, japo huko ‘saiti’ wanahoji kama Mahakama inayo nia ya kutoa haki kwa kila anayefika mbele yake kwa sasa?
Sitanii, naomba kuhitimisha makala hii kwa kushauri kuwa tuepuke dhana ya liwalo na liwe. Tujiepushe na dhana ya kumfukuza paka tukiwa tumefunga milango chumbani. Polisi wasiwafukuze vijana wa Bavicha na vijana wa Bavicha wasiwajaribu polisi. Tukiheshimiana kwa kiwango hicho, mikutano ya hadhara itarejea, na wanaoifanya watashiriki kwa kujadili ajenda na si uchochezi.
Heri na ole. Nasema tukifanya juhudi za makusudi kuminya uhuru wa mawazo, ama tutadanganywa na kupanda mtumbwi wa mabarafu au tutadumazwa na kujaza puto upepo bila kupima ukubwa wa ngozi yake. Likifumuka tuko hewa na chini kuna msitu wa simba na ziwa la mamba, historia itasomwa kwa mionzi ya kisayansi kujua kama Tanzania paliwahi kuishi watu. Mungu ibariki Tanzania, Mungu dumisha mani ya nchi yetu kwa kuongoza matendo ya Watanzania wadumishe amani, upendo na mshikamano.