Wafanyakazi wa Tanzania leo wanaungana na wenzao duniani kote katika
maadhimisho ya Sherehe za Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi).
Siku ya leo ni muhimu kwa sababu inasaidia kutambua mchango mkubwa na wa
kipekee wa wafanyakazi katika ustawi wa jamii yote duniani.
Tunachukua fursa hii kuwapongeza wafanyakazi wote nchini ambao kwa juhudi
zao Taifa letu limeweza kupiga hatua kubwa katika maendeleo. Wakati tunapata
Uhuru mwaka 1961 nchi yetu ilikuwa taabani kimaendeleo, lakini kwa juhudi za
wafanyakazi na kada nyingine za uzalishaji, tumeweza kupiga hatua ya kujivunia.
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alisema “Kazi ni Kipimo cha
Utu”. Maneno haya yanaendelea kuwa ndiyo msingi wa maendeleo katika Taifa
letu na mataifa mengine yaliyodhamiria kujikwamua kiuchumi.
Tunatambua na kuheshimu msimamo wa serikali zilizopita, na sasa Serikali ya
Awamu ya Tano, wa kuwahimiza wananchi kuchapa kazi. Sote hatuna budi
kutambua kuwa bila kazi hatuwezi kupata maendeleo – iwe ni kwa ngazi ya
familia, jamii au Taifa. Kazi imehimizwa hata kwenye vitabu vitakatifu, kwa hiyo
hakuna namna yoyote ya kukwepa kufanya kazi, hasa kwa wale watu wenye
uwezo wa kufanya kazi.
Tunapaswa kuongeza ari na moyo wa kupenda kufanya kazi ili kuleta tija kwa
familia na kwa Taifa. Kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi, si tu kwamba
analazimika kufanya kazi, bali anapaswa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa.
Tunapotamani maisha bora kwa kila Mtanzania hatuna budi kukiri na kutambua
kuwa hali hiyo itawezekana tu endapo kila mmoja wetu atafanya kazi kwa juhudi
na maarifa.
Pia tunatoa mwito kwa waajiri, hasa Serikali kuyatazama maslahi ya wafanyakazi
wake ili yawe bora zaidi. Kuwalipa vizuri wafanyakazi kutaongeza uzalishaji na
tija.
Jambo lililo muhimu ni kuwa kila mfanyakazi ajione ana wajibu wa kufanya kazi ili
ujira atakaoupata ulingane na jasho au nguvu anazotumia kwenye uzalishaji.
Tuepuke kuwa Taifa la watu wanaotaka kulipwa vizuri, lakini wasiokuwa tayari
kuongeza tija katika maeneo yao ya kazi.
Tunawapongeza wafanyakazi wote nchini tukitambua kuwa mchango wao ni
muhimu mno kwenye maendeleo ya Taifa letu. Tunapoona maendeleo katika
mataifa yaliyoendelea tutambue kuwa siri ya mafanikio hayo ni uchapaji kazi wa
wananchi wake. Hongereni sana wafanyakazi.