Kwa zaidi ya miezi miwili sasa kumekuwa na sintofahamu kwa wahasibu raia, wanaohudumu katika vyombo vya ulinzi na usalama. Rais John Magufuli aliagiza waondolewe, ili kuleta maboresho katika utendaji kazi.

Tunaamini Rais Magufuli alifikia maamuzi hayo baada ya kuambiwa kwamba kumekuwa na malipo kwa wafanyakazi hewa ndani ya Jeshi la Polisi, kama kiongozi ambaye amekuwa akipambana na kuondoa idadi ya wafanyakazi hewa katika mfumo wa malipo ilimlazimu kutoa maelekezo.

Ndiyo, maelekezo yalitolewa katika wakati sahihi. Lakini kuna kitu ambacho kimejificha nyuma ya askari hewa, ambao inaonesha kwa miaka miwili walau zaidi ya shilingi milioni 305, zimeyeyuka, huku zikionekana kuwalipa watu wasiostahili hata kidogo.

Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), imesema inaendelea na uchunguzi wa jambo husika. JAMHURI tunasema uchunguzi huo uje na majibu yanayosubiriwa kwa hamu na watanzania wote hasa kada ya wahasibu, ambao kwa kiwango fulani walionekana kurushiwa lawama.

DCI Diwani Athumani, ameliambia JAMHURI kwamba tayari ofisi yake inashirikiana na taasisi nyingine za kiuchunguzi hapa nchini kuchunguza na kutafuta ukweli wa jambo husika, huku akiahidi baada ya uchunguzi hatua nyingine za kisheria zitafuata.

Uchunguzi huo wa taasisi hiyo ndani ya Jeshi la Polisi, utathibitisha weledi katika masuala ya uchunguzi, na kuleta mwanga mzuri katika utendaji ndani ya jeshi.

JAMHURI tunaamini, wote wataokuwa wamehusika tangu kuandaa orodha ya majina feki, huku wakijua walioorodheshwa hawakuwa wanastahili posho za chakula, wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria na wapatiwe haki yao huko.

Ni kupitia uchunguzi huo pekee wingu lililotanda katika idara za uhasibu za majeshi, litaondoka. Maana wahusika halisi watabainika.

Uchunguzi huo utasaidia kubadili utaratibu ambao unaelekea kutekelezwa kwa kuwaondoa watumishi wa idara ya uhasibu wasiokuwa askari katika vyombo vya ulinzi na usalama. Maana wataalam wa fani za uhasibu wanasema kuwa na wahasibu raia kunaleta tija katika majeshi.

Hiyo ni kutokana na ukweli kwamba kama mhasibu ndani ya jeshi anakuwa ni askari, wakati mwingine atashindwa kutoa ushauri wa kihasibu hasa pale linapokuwa limetolewa agizo na bosi ambaye ana cheo zaidi ya huyu mhasibu ambaye ni askari.