Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan inatambua mchango mkubwa unaotolewa na wahandisi wanawake na kwamba inathamini kazi za kihandisi wanazozifanya katika kuchangia ukuaji wa uchumi nchini.

“Serikali inatambua umuhimu wa tasnia ya uhandisi kwa ustawi wa nchi nzima, hivyo inahitaji kuhamasishwa na kupewa kipaumbele ikiwa ni pamoja na kutengeneza viongozi wengi zaidi wanawake katika tasnia ya uhandisi. Mheshimiwa Rais amekuwa kielelezo cha ubora, maono, uthabiti na uthubutu kwa viongozi wanawake.”

“Kupitia uongozi wake tumeshuhudia namna anavyoifungua nchi yetu ikiwa ni pamoja na kufungua njia kwa wanawake wengi kuwa na uthubutu na kujiamini. Sasa njia iko wazi kwenu, kazaneni na wekeni bidii ili kazi yenu iendelee kuonekana na Taifa lisonge mbele.”

Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Ijumaa Julai 29, 2022) wakati akizindua Kongamano la Saba la Wahandisi Wanawake katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar Es Salaam.

Pia, Waziri Mkuu amesema amefurahishwa na shughuli mbalimbali ambazo Taasisi ya Wahandisi Tanzania kupitia Kitengo cha Wahandisi Wanawake inajihusisha nazo ambazo zimekuwa msaada mkubwa kwa Serikali katika kufanikisha azma yake ya kuwafikia Watanzania wote kuhusu kupata elimu ya masuala ya kihandisi.

“Ziara mnazofanya kwenye shule za sekondari na vyuo zimekuwa na mchango mkubwa katika kuandaa kizazi cha baadaye chenye ujuzi na uwezo wa kung’amua mambo mapema kwa maslahi mapana ya ustawi wa nchi. Kitendo hiki pia, ni ishara ya umoja uliopo baina yenu kwani mmeonesha uzalendo mkubwa na kwamba muda wote mnaitakia mema nchi yenu.”

Amesema Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuhamasisha wasichana katika shule za sekondari wapende na kusoma masomo ya sayansi na hisabati, kutembelea vyuo vikuu ili kuongea na wanafunzi wa kike wanaochukua kozi zinazohusiana na ujenzi na kuwajengea uwezo wanawake ili waweze kusajili kampuni na kufanya kazi za ukandarasi.

“Niwaase kutumia fursa hii kushirikiana na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ili kuongeza ushiriki wa wanawake katika tasnia ya ujenzi. Serikali inatambua mchango wa taaluma ya uhandisi kwa fani mbalimbali katika ukuaji wa uchumi wa Taifa kupitia ufanikishaji na ukuaji wa huduma mbalimbali.”

“Kwa takwimu za Machi, 2022 Tanzania ina wahandisi wapatao 30,921 ambapo kati yao wanawake ni 3,982 sawa na asilimia 12.88 tu. Hii ni idadi ndogo sana. Tunahitaji kuwa na wahandisi wanawake wengi zaidi, na hii ikiambatana na ongezeko la mafundi sanifu na mafundi mchundo. Serikali inaunga mkono juhudi hizi kwa kuanzisha shule za sayansi kwa wanawake katika kila mkoa.”

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi anayeshughulikia sekta ya Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya ametoa wito kwa wakandarasi na wahandisi washauri wanawake wafanye kazi kwa uadilifu na kuhakikisha miradi inakamilika kama ilivyopangwa na kwa viwango stahiki