Kama tujuavyo, hivi sasa Taifa letu liko katika mchakato wa kutafuta Katiba mpya ya nchi.
Katiba tunayotafuta sasa itakuwa nafasi ya katiba ya kudumu iliyoanza kutumika mwaka 1977. Katiba ya nchi tunayotaka kuachana nayo imedumu kwa mbinde kwa sababu ina kasoro nyingi zilizoanza kupigiwa kelele tangu mwaka 1992, wakati Tanzania ilipoingia kwenye mfumo wa vyama vingi.
Katiba hii ya sasa iliyotungwa na wabunge wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) pekee yao, waliweka mbele maslahi yao ya chama chao, pengine kuliko maslahi ya Taifa.
Katiba hiyo haikushirikisha wananchi. Ni kweli Tume ya Jaji Mkuu Francis Nyalali ilifanya kazi nzuri hadi ilipopendekeza Tanzania iwe nchi ya vyama vingi katikati ya wanachama na viongozi wa CCM, waliotaka mfumo wa chama kimoja waendelee kulinda maslahi yao.
Kwa hiyo, wabunge wanachama wa CCM walipokutana bungeni, walivuruga nia njema ya Tume ya Nyalali iliyotaka Tanzania iwe na mfumo wa vyama vingi unaozingatia haki.
Wabunge wa CCM walitunga sheria ya vyama vingi iliyowapendelea kwa hiyo, kwa mfano, sheria ilikataza mtu kuhoji mahakamani matokeo ya uchaguzi wa rais au kuhoji mahakamani utendaji wa Tume ya Uchaguzi, yalikuwa matokeo ya kutambua kwamba walidhulumu haki.
Ukafika mwaka 2010 ambapo Rais Jakaya Kikwete alitangaza nia yake ya kuhakikisha kwamba Tanzania ina Katiba mpya.
Vyema, sasa wananchi tunataka Katiba halisi ya kudumu ambayo itatokana na Katiba hiyo kuzingatia haki na maslahi ya Taifa zima. Hatutaki tena Katiba inayolinda maslahi ya chama kimoja.
Lakini ipo hatari ya Katiba mpya kuvurugwa na baadhi ya wabunge wanachama wa CCM. Ikumbukwe kwamba Rais Kikwete hataki kukumbukwa kwa kuleta Katiba mpya, tu bali pia anataka akumbukwe kwa Katiba safi inayolinda maslahi ya watu katika Taifa hili na wala si inayolinda wanachama wa CCM na chama chao tu.
Dalili za mvua ni mawingu. Tulishuhudia ushabiki wa kisiasa zaidi kuliko ushabiki wa kitaifa na kizalendo mwaka 2011, wakati Bunge lilipotunga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Ushabiki huo wa kisiasa ulisababisha chama kikubwa cha upinzani kususia kikao cha Bunge.
Kwa ujumla, kila mtu na imani kwamba Tume ya Warioba itafanya kazi nzuri katika kuratibu maoni ya wananchi kama ilivyofanya Tume ya Nyalali mwaka 1991. Tatizo kubwa linaweza kutokea kwenye mkutano wa Bunge la Katiba ambako kama kawaida baadhi ya wabunge wa CCM kwa kutumia wingi wao, wataweza kuvuruga maoni safi yatakayotokana na kazi itakayokamilishwa na Tume ya Jaji Warioba.
Chonde! Chonde! Wabunge wa CCM. Taifa kwanza chama baadaye. Tuwaandalie watoto wetu Katiba halisi ya kudumu ambayo haitaleta migogoro.
Kama nilivyotangulia kudokeza; ili tuwe na Katiba halisi ya kudumu ambayo haitasababisha wananchi kudai nyingine haraka, ni lazima kila mtu atakayehusishwa na mchakato huu wa Katiba aweke mbele maslahi ya Taifa na wala si ushabiki wa kisiasa.
Tunataka mfumo wa vyama vingi unaoendeshwa kwa haki. Tusije tukasahau kwamba nchi zote zilizopata maendeleo makubwa duniani, ni zile zilizoheshimu kwa dhati mfumo wa vyama vingi. Kwa mfano, Uingereza na Marekani.
Tuzingatie pia kwamba hata hapa Tanzania mambo yamekuwa nafuu zaidi, baada ya kuingia mfumo wa vyama vingi pamoja na vikwazo vyote vyama vya upinzani vilivyoendelea kuwekewa na chama tawala na Serikali yake.
Katiba halisi ya kudumu tunayaotaka Tanzania lazima izingatie masaula yafautayo:
Kwanza Katiba ieleze waziwazi kwamba Kiswahili ni lugha ya Taifa ya Tanzania, pia kwamba Kiswahili na Kiingereza ni lugha rasmi Tanzania maana wakati Kenya haikusita kuonesha hivyo katika katiba yake, Tanzania imendelea kuionea aibu lugha ya Kiswahili wakati dunia inaamini kuwa Kiswahili kwao ni Tanzania.
Pili, Katiba isitaje Tanzania inafuata siasa gani. Tuondokane na madai ndani ya Katiba kwamba Tanzania inafuata Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea wakati tupo katikati ya siasa ya ubepari.
Tatu, Katiba ieleze waziwazi kwamba Tanzania ni nchi mbili – ikizingatiwa kuwa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010 inataja Zanzibar kuwa ni nchi. Tunataka Katiba halisi ya kudumu inayosema kweli tupu.
Nne, tunataka Katiba mpya itamke uhuru wa wananchi wa kuunda jumuiya zao za kitaifa. Kwa hivi sasa tuna jumuiya za kisiasa. Kwa mfano, Umoja wa Vijana, Jumuiya ya Wanawake na kadhalika.
Ukitaka kusema kweli, mambo mengi yameharibika Tanzania kwa kukosekana jumuiya halisi za wananchi. Tunahitaji umoja halisi wa vijana ambao hautafungamana na chama chochote cha siasa. Tunataka, kwa mfano, umoja wa wazazi wa kitaifa utakaojishughulisha na maadili ya vijana, pia na elimu ya watoto na kero wanazopata walimu.
Kwa sasa ikijishughulisha kwa wazazi masuala ya elimu yanaishia kwenye mikutano ya wazazi kishule. Basi Katiba itoe uhuru kwa wazazi, vijana na wanawake kuanzisha jumuiya za kitaifa.
Tano, Katiba ieleze kwamba ngazi ya kwanza ya Serikali za Mitaa ni shina (nyumba kumi kumi). Tufute mashina yanayojishughulisha na siasa wakati mashina yalianzishwa mwaka 1965 ili kulinda usalama wa raia na Taifa katika shina.
Mungu ibariki Tanzania ili ipate Katiba safi na halisi ya kudumu.