Mwaka 1953 nilikuwa mwanafunzi wa darasa la kumi, miaka hii ni kidato cha nne, nilikuwa nasoma Shule ya Sekondari ya Chidya, wilayani Masasi, Kusini Tanzania (Tanganyika enzi hizo).
Shule ya Chidya ilikuwa shule ya kwanza ya sekondari Kusini Tanganyika. Ilianzishwa mwaka 1923 na wamisheni wa Kanisa Anglikana, Mkuu wake wa kwanza alikuwa Padre Obedi Yusuf Kasembe, mtu wa jamii ya Wamakua aliyezoea kujiita ‘Mmakua wa Wamakua.’
Wakati tuliosoma sisi tulikuwa na Mkuu mpya wa shule, Louis Sparham, Mwingereza. Kukatokea shida kubwa ya chumvi shuleni petu. Japokuwa vijana wa Kimakua na Kiyao ambao ndiyo waliokuwa wengi shuleni hapo walikuwa wamezoea kulishwa mboga isiyo na chumvi jandoni, walitambua kwamba safari hii hawakuwa jandoni, walikuwa shuleni. Kwa hiyo, hawakuona sababu ya kuvumilia kulishwa mboga isiyo na chumvi.
Jioni ya Jumapili moja yakapangwa maandamano ya kwenda nyumbani kwa mkuu wa shule kudai chumvi. Hii ilikuwa baada ya viranja wa shule kufikisha tatizo hilo kwa uongozi wa shule na kutokuchukuliwa hatua yoyote.
Mwaka ule nilikuwa Bwana Saa wa shule, nafasi ambayo mwisho wa mwaka ule ilinipatia heshima ya kuteuliwa kuwa mwanafunzi bora wa mwaka, nikapewa zawadi ya Biblia ambayo ndiyo iliyokuwa zawadi kubwa aliyoweza kupewa mwanafunzi Mkristo.
Nilipokuwa Bwana Saa sikupiga kengele, nilipiga ngoma. Basi jioni ile ya Jumapili saa 12 jioni alikuja mwanafunzi mmoja eneo nililokuwa nimekaa. Akachukua ngoma bila kusema lolote, akaondoka nayo. Nilimuuliza alikuwa anapeleka wapi ngoma, akaniambia “kaa kimya, wewe hujui kitu.”
Kwa kuwa alisema nami kwa ukali sikutafuta utata, nilikaa kimya.
Ikatokea kwamba mwanafunzi yule aliyekuwa amechukua ngoma, alikwenda moja kwa moja eneo la uwanja wa shule wa kukutania. Akapiga ngoma ya kuashiria kuwa kulikuwa na mkutano wa dharura.
Kufumba na kufumbua, karibu wanafunzi wote walikuwa pale isipokuwa wanafunzi wa bweni la Vincent Lucas. Hawa walikuwa wamepata habari mapema kuwa kungekuwa na maandamano ya kudai chumvi. Wakaamua kutoshiriki maandamano hayo kwa kuwa mwalimu wa bweni lao, Yustino Mfaume, alikuwa mkali sana.
Wakahisi wangepata matata kama angesikia kuwa walikuwa wameshiriki maandamano yale.
Maandamano hayakuwa ya kimya kimya. Kila mshiriki wa maandamano yale alitakiwa kushika mkononi kitu chochote chenye kutoa sauti, wengine wakashika filimbi, wengine wakashika makopo, na wengine walishika madebe.
Maandamano yakaanza, mbele alitangulia mpiga ngoma kubwa (mdundo). Kila alipopiga mdundo “ndi! ndi! ndi!” waandamanaji waliitikia kwa umoja “hakuna chumvi.” Kelele za “hakuna chumvi” ziliendana na milio ya filimbi, makopo na madebe.
Ungedhani maandamano hayo yalikuwa yamefanyiwa mazoezi mwezi mzima. Maandamano yalisonga mbele. Mkuu wa shule akasikia kelele zinaelekea nyumbani kwake, kwa kuwa hakujua lugha ya Kiswahili alimuuliza mpishi wake kulikuwa na nini?
Mpishi akajibu kuwa wanafunzi walikuwa wanasema “Hakuna chumvi.” Mkuu wa shule akatambua kuwa mlengwa wa maandamano hayo alikuwa yeye, akatoka nyumbani akitokea mlango wa nyuma, akaenda kujificha kanisani.
Waandamanaji wakaingia eneo la nyumba ya mkuu wa shule. Kelele za hakuna chumvi zikazidi, ungedhani waandamanaji walikuwa vibarua ambao tayari walikuwa wanalipwa mishahara yao, kumbe walikuwa wanadai haki.
Mmoja wao akaenda kugonga mlango wa mbele uliokuwa umefungwa, badala ya kutoka mkuu wa shule alitokea mpishi aliyewaambia kwamba mkuu huyo wa shule hakuwako mle nyumbani.
Waandamanaji wakarejea mabwenini kimya kimya huku wakiwa na uhakika kwamba ujumbe wao umefika. Kesho yake na kwa juma zima mkuu wa shule alikuwa ameshikwa na mafua na hakuwa na furaha. Alishindwa hata kuzungumza.
Wakati huo huo, waliorodheshwa wanafunzi waliokuwa wameshiriki maandamano yale ya kihistoria. Hakuna aliyefukuzwa shule, ila wote walipewa adhabu ya kufyeka na kulima eneo la shule ambalo halikuwahi kulimwa tangu kujengwa kwa shule hiyo.
Hazikupita siku tatu, shule ikapata chumvi ya kutosha kutoka Machole, Lindi. Kumbe uongozi wa shule ulikuwa umesubiri machafuko ndipo unyooshe mambo!
Kimataifa, mwisho wa mwaka 1989 ulishuhudia machafuko makubwa nchi za Ulaya Mashariki. Wakati wanachama walipoamua kuandamana kupambana na mfumo wa chama kimoja uliokuwa ukiendelea kuwakandamiza. Kama tujuavyo, mfumo wa chama kimoja ulianzishwa na Warusi mwaka 1917.
Machafuko yalitokana na hatua ya wananchi wa Ulaya Mashariki kuukataa mfumo huo. Yalitokea maafa makubwa. Watu wengi waliuawa na polisi mpaka nguvu ya umma ilipowashinda polisi. Viongozi mbalimbali wa nchi, ama waliondolewa madarakani au waliuawa. Na baadhi ya nchi kama Urusi na Yugoslavia zilisambaratika.
Yalikuwa matokeo ya uongozi wa nchi hizo kusubiri machafuko ili wanyooshe mambo. Watu wenye busara hawasubiri machafuko ili wanyooshe mambo.
Kwa hiyo, Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye alikuwa mtu wa kuona mbali, aliona kwamba machafuko kama yale yaliyotokea Ulaya Mashariki yangeweza kutokea Tanzania kwa kuwa sote tulikuwa tumeogelea katika ziwa moja la mfumo wa chama kimoja.
Akapigania mfumo wa vyama vingi katikati ya watu ambao hawakutaka mabadiliko hadi tulipopata mfumo huo mwaka 1992.
Kwa jumla tukitaka kusema kweli, si juhudi za Mwalimu Nyerere zilizoleta mfumo wa vyama vingi Tanzania. CCM haikutaka mfumo wa vyama vingi, ilisubiri machafuko ili inyooshe mambo, mpaka wahisani walipohusisha misaada yao na mfumo wa vyama vingi.
Kwa kuwa CCM iliruhusu nchini mfumo wa vyama vingi kwa shingo upande, iliweka vikwazo vilivyoendeleza udikteta Tanzania mpaka leo. Kwa mfano, wameendelea kuzuia wagombea binafsi, hata pale Mahakama ilipoamua kuruhusu wameendelea kuzuia matokeo ya uchaguzi wa Rais yasihojiwe mahakamani.
Na wameendelea na Tume ya Uchaguzi ambayo inaonekana kutumika kupora ushindi wa wapinzani. Hizi si siasa za ushindani. Wameziba masikio, hawataki kunyoosha chochote mpaka yatokee machafuko makubwa.
Huko Kenya, wameendelea na maandamano ya kuitaka tume ya uchaguzi. Hapa Tanzania hapana shaka watatumiwa polisi wananchi wakiamua kuandamana kuikataa tume ya uchaguzi.
Polisi Tanzania wameendelea kutumiwa vibaya na CCM na Serikali yake kudhoofisha upinzani. Hapa hatuna ushindani wa vyama, tuna ushindani wa polisi na vyama vya upinzani, ni demokrasia staili ya Tanzania.
Tazama! watu wanakamatwa na kupigwa mabomu kwa kukutwa kwenye mkutano uliopata vibali na hawakuzuiwa. Mikutano ya hadhara ya wapinzani inapigwa marufuku nchi nzima wakati ni haki ya vyama vya siasa kufanya mikutano hiyo. Tunasubiri machafuko ili tunyooshe mambo! Ni demokrasia au ni udikteta?