Nachukua fursa hii kutoa pole kwa ndugu zetu waliowapoteza wapendwa wao, Jeshi la Polisi, nchini na Taifa kwa ujumla.
Nasikitika kuona nchi yangu Tanzania, nchi iliyosifika kwa kuwa na upendo, amani na utulivu, hivi sasa imeanza kuwa historia kutokana na matukio ya kuogofya na kukatisha tamaa.
Katika kipindi cha miaka zaidi ya 50 ya Uhuru, Watanzania sasa wameondokewa na utu na wanazidi kufichua makucha yao huku wakijifikiria wao wenyewe bila kujali ndugu zao.
Tumefikia hatua ya kutojali hata utu wetu na kuamua kusababisha taharuki huku wakiibuka na kukatisha uhai wa ndugu zetu. Wamekuwa watu wa mipango na mikakati ya kuichafua nchi yetu na kuipaka matope kutokana na kuunda magenge ya kihuni.
Tanzania nchi yangu imekumbwa na sintofahamu kutokana na kuibuka kwa vikundi vya kihuni, vilivyoamua kucheza na maisha ya watu na kuibua taharuki kwa vitendo vya kutekana na kuua raia.
Katika kipindi kifupi, tumeshuhudia viongozi katika Mkoa wa Pwani wakiuliwa na watu wasiofahamika. Mauaji haya yameendelea kutokea bila kukoma huku familia zikiachwa yatima.
Tumeshuhudia jinsi askari wetu walivyokuwa wakiuliwa na vikundi hivi kwa kihuni. Huu si utamaduni wa Mtanzania aliouzoea, utamaduni wa hovyo wa kuua walinda amani wetu! Hii ni laana na wala si jambo la kufurahia na kusherehekea kama baadhi ya watu wanavyofanya kupitia mitandao ya kijamii.
Haiwezekani askari wetu tunaowategemea katika ulinzi wauliwe nasi tuchekelee! Tumerogwa? Tumerogwa na nani kiasi cha kuanza kusherehekea mauaji ya walinda amani wetu?
Ni jukumu letu sote kuikataa laana hii na kupambana kuwafichua wale wote wanaohusika kwa njia moja ama nyingine. Tuwafichue kutokomeza mauaji ya ndugu zetu. Tuwafichue tutokomeze kuweweseka huku kulikoibuka nchini.
Naiomba Serikali iweze kulitumia Jeshi letu la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kukomesha uhuni huu, kwani bila kufanya hivyo tutajikuta ukiota mizizi na kufanya unavyotaka.
Kitendo cha kuuliwa kwa askari wetu si cha kupuuza hata kidogo. Si cha kubeza hata, bali ni cha kulaaniwa kwa nguvu zote na kukemewa ili kisitokee tena.
Kwa vyovyote wanavyoitwa wahalifu hawa wanapaswa kudhibitiwa kama inavyotakikana bila kuonewa huruma – kudhibitiwa kwa kuanzia na wahusika wote bila kujali mahala walipo – ili uwe mwisho wao kufanya vitendo viovu katika ardhi ya nchi yetu tuliyotunukiwa umoja na amani.
Ni jukumu la wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama kutafakari taharuki hii na uhuni huu unaofanyika, ili kuutokomeza na kurejesha amani iliyoanza kutoweka.
Sitarajii tena kuona ukimya wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba. Nataraji kuona akikemea aliyonyamazia uovu unaoendelea huku wananchi wakilalama.
Mwigulu Nchemba ninayemfahamu ni yule anayekemea uovu, asiye tayari kunyamazia uovu. Nataraji kumuona akikemea uovu na kupunguza ukimya katika haya yanayoendelea ili kujenga nguvu ya pamoja katika kulinda amani ya nchi yetu.
Ni wakati wa kusimama pamoja na kukataa udhalimu huu unaojipandikiza nchini kimya kimya. Tukatae kutekwa na kuuliwa na wahuni wachache watakavyo. Tuungane na kulinda umoja na amani yetu tuliyoizoea.
Mungu Ibariki Tanzania. Mungu vibariki vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama.