Kufanya kazi ndiyo msingi wa maisha yetu ya kila siku, hususan jamii yetu ya Kitanzania ambayo wimbo mkubwa ni ukosefu wa ajira pamoja na ugumu wa maisha unaoongezeka kila kukicha.
Kila kazi huenda ikawa na changamoto zake, lakini kwa kuwa hatuna hiyana basi tunaweza kutumia mbinu mbadala kuhakikisha kazi inafanyika tena kwa kiwango kinachostahili.
Tatizo tulilonalo wengi ni kutopenda kutimiza wajibu wetu kwa wakati, hali inayochangia shughuli nyingi katika taasisi mbalimbali kudorora au kutofanyika kabisa.
Hapa huenda watu wanafanya kazi kwa mazoea ama bora liende, au labda wanatengeneza mazingira kama ilivyo kwa watumishi mbalimbali kupata saa za ziada (overtime). Huu ndiyo utendaji kazi wetu.
Ukiangalia katika kazi utakubaliana nami kuwa wengi wetu tunapenda sana starehe kuliko kazi, na ingekuwa kila mtu anapenda kufanya kazi basi uchumi wa nchi yetu usingekuwa chini, ungekuwa juu.
Namnukuu aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, katika maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi (Mei Mosi) 2001, iliyofanyika Dar es Salaam, kama ifuatavyo:
“Tanzania ni miongoni mwa nchi maskini sana duniani, na sasa tumeazimia kuondokana na aibu hiyo. Tumebuni Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 inayokusudia kutufanya tuwe Taifa ambalo watu wake walio wengi watakuwa na maisha bora.
“Taifa lenye amani, utulivu, na umoja; Taifa linaloongozwa kwa misingi ya utawala bora, utawala wa sheria; Taifa lenye watu walioelimika na wanaoendelea kujielimisha; na Taifa lenye uchumi unaohimili ushindani, uchumi unaokua na kutoa ajira na mapato, uchumi endelevu usioharibu mazingira yetu, na uchumi utakaonufaisha washikadau wote, na kuhimili matumaini yetu ya maisha ya kisasa.”
Nimejaribu kukumbusha maneno haya, ili tuweze kuwa pamoja katika kile ninachokusudia kukieleza juu ya utendaji kazi hapa Tanzania.
Mwaka mzima una jumla ya saa 8,760 lakini kati ya hizo unaweza kubaini saa 1,068 hatufanyi kazi na saa zinazobakia, yaani 7,692 ndiyo tunazofanya kazi zetu, au ndiyo tunasema tupo kazini.
Kwa mujibu wa sheria na taratibu za Shirikisho la Vyama vya
Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), mfanyakazi kwa siku anatakiwa afanye kazi saa zisizozidi nane na baada ya hapo ni ‘over time’.
Hapa ninamaanisha kwamba mfanyakazi akiingia kazini saa mbili asubuhi, anatakiwa atoke saa kumi jioni, na akiendelea hapa inahesabika kuwa amepitiliza muda wa kazi na anastahili malipo ya ziada.
Kwa mwaka mzima tuna sikukuu 17, yaani Januari Mosi ni Mwaka Mpya, Januari 12 ni Mapinduzi ya Zanzibar, Februari 6 ni Maulid (kutegemeana na kuandama kwa mwezi), Aprili kuna Ijumaa Kuu, Kumbukumbu ya Karume, Jumatatu ya Pasaka na Muungano.
Mwezi Mei kuna Mei Mosi, Julai 7 ni Sabasaba, Agosti 8 ni Nanenane, bado Idd el Fitr ambapo zipo mbili na Oktoba kuna Nyerere Day na Idd el Hajj, wakati Desemba zipo Sikukuu tatu – Uhuru na Jamhuri, Krismasi na Boxing.
Sikukuu zote hizi zina jumla ya saa 236 ambazo hatufanyi kazi, ambapo mapumziko ya mwisho wa juma ni siku 104 ambazo ni sawa na saa 832, na jumla kuu ni saa 1,068.
Nchi zilizoendelea kiuchumi duniani kama Marekani utakuta wana sikukuu saba kwa mwaka, huku nchi nyingine zikiwa na sikukuu chache zaidi. Hapa ina maana kuwa wapo kikazi zaidi kulikoni sisi Watanzania.
Mfano, mfanyakazi ambaye ni mwanamke kama ameolewa na ana watoto watano, ni kuwa katika utumishi wake mwaka mmoja na miezi mitatu tofauti na wikiendi na sikukuu hajawahi kwenda kazini. Kama kuna likizo ya uzazi, alifiwa, semina, ugonjwa na sababu nyinginezo. Hii ndiyo hali ya utendaji kazi kwa baadhi ya watumishi wengi tulio nao hapa nchini, hali inayochangia kurudisha uchumi wetu nyuma.
Takwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu zinaonesha kuwa katika mwaka 2011, pato halisi la Taifa lilikua kwa asilimia 6.4 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 7.0 mwaka 2010. Kiwango kidogo cha ukuaji kilitokana na hali mbaya ya ukame iliyojitokeza katika sehemu mbalimbali nchini, ambapo imeathiri sekta ya kilimo, pamoja na ukosefu wa nishati ya umeme ya uhakika, ambayo ilisababisha kupungua kwa uzalishaji wa bidhaa za viwandani na shughuli nyingine zinazohitaji nishati.
Kutokana na idadi ya watu Tanzania Bara kukadiriwa kuwa 43,169,305 pato la wastani la kila mtu lilikuwa Sh 869,436.3 mwaka 2011 ikilinganishwa na Sh 770,464.3 mwaka 2010, sawa na ongezeko la asilimia 12.8.
Kiwango cha ukuaji katika shughuli za kiuchumi za kilimo kilikuwa asilimia 3.6 mwaka 2011 ikilinganishwa na asilimia 4.2 mwaka 2010. Upungufu huu ulitokana na kuchelewa kwa mvua za msimu kwa mwaka 2009/10 ambazo ziliathiri uzalishaji wa mazao.
Kiwango cha ukuaji katika shughuli ndogo za uzalishaji mazao kilishuka hadi kufikia asilimia 3.5 mwaka 2011, kutoka asilimia 4.4 mwaka 2010 kutokana na kupungua kwa uzalishaji kufuatia kuwapo kwa hali mbaya ya hewa katika msimu wa 2009/10.
Kiwango cha ukuaji katika shughuli ndogo za mifugo kilikuwa asilimia 3.9 mwaka 2011 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 3.4 mwaka 2010. Ufanisi katika utekelezaji wa programu za kuboresha maeneo ya malisho na uimarishaji ubora wa mazao ya mifugo, ni miongoni mwa sababu zilizochangia kuongezeka kwa kiwango cha ukuaji katika sekta hii.
Shughuli ndogo za kiuchumi katika misitu na uwindaji zilikua kwa kiwango cha asilimia 3.5 mwaka 2011 ikilinganishwa na asilimia 4.1 mwaka 2010. Hii ilitokana na kupungua kwa mapato yatokanayo na uwindaji wa kitalii na hatua ya Serikali kudhibiti uvunaji holela wa mazao ya misitu, na hivyo kupunguza uvunaji na uuzaji wa mazao ya misitu.
Kama kuna uwezekano kila mtu ajikite katika kuzalisha na kutimiza wajibu wake zaidi kulikoni kufanya bora liende. Hii itatuwezesha kunusuru hali ya uchumi wetu unaoonekana kuzorota na maisha kuzidi kuwa magumu.
Vilevile ni muda mwafaka kwa Watanzania kufanya tathmini na kujionea kama hizi sikukuu zinaendana na uhalisia wa uchumi wa nchi yetu, ikilinganishwa na nchi nyingine tajiri duniani.
0712 229 829