MOROGORO
Na Everest Mnyele
Wiki iliyopita Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewafuta rasmi uanachama wabunge 19 wa Viti Maalumu.
Hebu kwanza tujifunze maana ya chama cha siasa. Kwa lugha rahisi, chama cha siasa ni muungano wa watu wenye itikadi moja wakiwa na nia ya kutafuta mamlaka katika dola au nchi (hasa ya kiserikali) kwa shabaha za kisiasa na kibinafsi, pamoja na kueneza falsafa fulani.
Maneno makuu ni ‘muungano’, ‘itikadi’, ‘dola’ na ‘falsafa’. Iwapo kutakuwapo itikadi na falsafa tofauti, hapo hakuna chama.
Kila chama huwa na utaratibu wa kuendesha shughuli zake kuendana na itikadi na falsafa yao, utaratibu ambao huundiwa ‘Katiba ya chama’ inayopaswa kufuatwa na viongozi na wanachama ili kuleta utulivu.
Uamuzi wowote unaofanywa na chama hufuata katiba, na si vinginevyo!
Tangu mwaka 1992, Tanzania iliridhia kufuata mfumo wa demokrasia ya vyama vingi.
Naasema ‘kuridhia’ kwa sababu haikuwa mara ya kwanza kuwa na mfumo huu.
Hapo ndipo vyama vya siasa viliundwa kutaka kuipoka dola kutoka CCM. Vilianzishwa vingi lakini vilivyowahi kutikisa ni NCCR-Mageuzi, CUF, Chadema na ACT-Wazalendo.
Hata hivyo, ukweli ni kwamba ni Chadema, chama kilichoasisiwa na Edwin Mtei, ndicho chenye mipango thabiti ya kuchukua ‘dola’ tofauti na vingine, hasa huku Tanzania Bara.
Bila shaka ni Chadema ndicho chama kikuu cha upinzani nchini.
Katiba inaelekeza kwa yeyote anayeutaka uongozi wa kisiasa nchini lazima adhaminiwe na chama cha siasa. Maana yake ili uwe rais, mbunge au diwani, lazima uwe mwanachama mwaminifu wa chama fulani cha siasa kitakachokudhamini.
Itambulike kwamba kila chama kina katiba yake na utaratibu wa kuwadhamini wanachama wake kuwa wabunge, madiwani na viongozi.
Ni hapa ndipo sakata la wabunge 19 wa Chadema linaanzia. Tujiulize, kulitokea nini hata wakafukuzwa uanachama na kikao cha juu kabisa, Baraza Kuu la Chadema?
Mapema nimefafanua maana ya chama na maelekezo ya kikatiba ya udhamini wa chama (vyama) kwa anayetaka urais, ubunge au udiwani.
Kwa ufupi uwepo wa wabunge wale 19 wa Chadema haukuwa na baraka za chama. Sasa ilikuwaje wakaapishwa na kuingia bungeni?
Lazima Watanzania tuache ubabaishaji. Tufuate taratibu na tuheshimiane kwani nchi hii ni yetu sote. Ubabe unaweza kusababisha mtafaruku na machafuko.
Tunafahamu Uchaguzi Mkuu uliopita ulivyoendeshwa kwa namna ambayo haijawahi kutokea.
Ninachompendea Rais Samia Suluhu Hassan ni utayari wake wa kukiri makosa juu ya kilichotokea. Kwa kweli wapinzaji walishughulikiwa na huenda hakufurahia hali ile ndiyo maana sasa anafanya kila awezalo kuirudisha demokrasia ya vyama vingi kwenye mstari.
Sijui kwa nini hili lilifanyika mwaka 2020! Kwa uelewa wangu wa demokrasia ya vyama vingi na maana ya uchaguzi huru na wa haki, nitakuwa mnafiki nikisema tulikuwa na uchaguzi huru na wa haki.
Hivyo kwa chama makini cha upinzani, ilikuwa vigumu kukubaliana na matokeo ya uchaguzi ule ndiyo maana Chadema waliugomea na kuuita haramu, na kuapishwa kwa wabunge 19 wa Viti Maalumu kulishitua Watanzania wengi.
Sitawalaumu hawa, kwa jinsi ninavyowafahamu, nadhani kuapishwa kwao bila baraka za chama kulikuwapo siri kubwa wanayoifahamu wachache.
Ndugu zangu, ni muhimu kama vyama vya siasa kuheshimu taratibu walizojiwekea, vinginevyo ni vurugu.
Hongera Chadema kwa uamuzi mgumu, hii inajenga nidhamu ndani ya chama na kukiimarisha.
Duniani kote, hata ndani ya CCM, ukikosa nidhamu unafukuzwa uanachama. Kinachofanywa na Chadema ni sahihi na ni vema waliofukuzwa wasilalamike ingawa inaonekana kulikuwapo shinikizo la kuapishwa bila ridhaa ya chama.
Wabunge hawa wakubali uamuzi wa chama ili kuimarisha demokrasia nchini. Wapo huru kuomba radhi na kujiunga upya Chadema, hivyo kuendelea kuimarisha upinzani na demokrasia.
Kuna wanaojiuliza itatokea nini bungeni? Hakuna haja ya kupoteza muda, katiba inasema mbunge akipoteza uanachama na ubunge unakoma mara baada ya Spika kupelekewa taarifa rasmi.
Spika ambaye kwa bahati nzuri ni mwanasheria aliyebobea, hatapoteza muda kwa jambo hili kwani lipo wazi. Nadhani Spika atajenga heshima yake na Bunge kwa kuridhia uamuzi wa Baraza Kuu.
Tusidanganyane, tunapaswa kujifunza mengi kwa tukio hili.
Kwanza, viongozi wa dola tusimamie na kuilinda katiba kwa masilahi mapana ya nchi yetu. Pili, viongozi wa dola wasiingilie uhuru wa wananchi katika kuwachagua viongozi wanaowapenda kwani kufanya hivyo kunasababisha kupata viongozi wasiokidhi matarajio.
Tatu, tuendeshe masuala ya kisiasa kwa kuheshimiana, hivyo kuepuka mifarakano isiyo ya lazima. Mwisho, wanasiasa heshimuni katiba zenu na mheshimu taratibu za vyama na muwe na nidhamu kwa vyama vyenu na itikadi mnayoiamini.
Kwa watawala na wenye mamlaka, simamieni kwa uadilifu demokrasia ya mfumo wa vyama vingi ili kupata viongozi wanaotokana na wananchi, hii ina manufaa makubwa kuliko madhara.
Ukweli ni mgumu kumeza, lakini ukweli utatuweka huru na haki huinua taifa. Nchi yetu ni tamu sana. Tushirikiane kuijenga. Hongereni Chadema kwa kufungua ukurasa mpya wa siasa.