Alhamisi wiki iliyopita serikali kupitia kwa Waziri wa Fedha iliwasilisha mapendekezo ya bajeti kuu kwa ajili ya mwaka wa fedha 2019/2020.
Bajeti hiyo baada ya kuwasilishwa itajadiliwa na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambao kwa mujibu wa taratibu watakuwa na fursa ya kufanya marekebisho kwa kadiri watakavyoona inafaa kwa kuzingatia masilahi ya taifa.
Katika mapendekezo ya serikali kuhusu bajeti hiyo, jumla ya shilingi trilioni 33.11 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika katika uhai wa bajeti hiyo ya mwaka 2019/20.
Kwamba, mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa shilingi trilioni 23.05 ambayo ni asilimia 69.6 ya bajeti yote, na mapato yatakayotokana na kodi ni shilingi trilioni 19.10 sawa na asilimia 12 ya pato la taifa, na baadhi ya michanganuo ya bajeti 2019/2020 ni shilingi trilioni 7.56 kwa ajili ya mishahara, shilingi trilioni 1.44 kwa ajili ya miradi ya umeme vijijini, shilingi bilioni 788.8 za miradi kadhaa ambayo ni pamoja na reli, maji na shilingi bilioni 450 kwa ajili ya elimu ya juu, shilingi bilioni 288.5 kwa ajili ya kugharimia mpango wa elimu bure, na shilingi bilioni 600 kwa ajili ya wazabuni.
Vilevile katika bajeti hiyo waziri husika amependekeza kufutwa kwa misamaha ya kodi maeneo kadhaa, ikiwamo katika taulo za kike, kwa kuwa uamuzi wa awali haukuwezesha kupatikana kwa bei nafuu kwa bidhaa hiyo muhimu kwa walengwa kama ilivyokusudiwa, badala yake ni kuwanufaisha wafanyabiashara.
Pia kuna mapendekezo mengine ya ongezeko la ushuru kama vile utozaji wa ushuru wa asilimia 10 kwenye bidhaa za nywele za bandia zinazotengenezwa ndani ya nchi na asilimia 25 zinazoagizwa kutoka nje ya nchi, lengo likiwa ni kuongeza mapato ya serikali.
Mengineyo ni kuongeza muda wa leseni ya udereva kutoka miaka mitatu hadi mitano, sambamba na kuongeza tozo ya leseni kutoka shilingi 40,000 hadi 70,000, ada ya usajili wa magari kutoka 10,000/- hadi 50,000/-, bajaji kutoka 10,000/- hadi 30,000/- na pikipiki kutoka 10,000/- hadi 20,000/-.
Zaidi ya hapo, waziri amesisitiza kuwa tozo zote zilizokuwa zinatozwa kwa dola za Marekani zitatozwa kwa shilingi ya Tanzania, isipokuwa kwa shehena za kemikali zinazokwenda nje ya nchi. Kwa hiyo, JAMHURI tunaamini kuwa mjadala miongoni mwa wabunge utakuwa wenye tija zaidi ili hatimaye kupitisha bajeti bora zaidi. Tunawatakia kila la heri wabunge.