Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Leo zimesalia wiki tatu kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (TAMISEMI). Chama Cha Mapinduzi (CCM) wiki iliyopita wamepiga kura za maoni na kupata wagombea watakaowawakilisha katika uchaguzi huo unaofanyika Novemba 27, 2024. Yanaweza kuwapo malalamiko kati ya wagombea ndani ya CCM, lakini zamu hii sijasikia mengi.

Sitanii, kabla sijaendelea kuandika makala hii, naomba kurejea taarifa iliyotolewa na aliyekuwa Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Dk. Seleman Jafo, Novemba 27, 2019, iliyosema hivi:

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Selemani Jafo amesema kuwa Chama Cha Mapinduzi kimeshinda katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika Vijiji 12,260 sawa na asilimia 99.9, Mitaa 4,263 sawa na asilimi 100 huku kikijinyakulia vitongoji 63,970 sawa na Asilimia 99.4.

Ameyasema hayo leo wakati akitoa taarifa ya matokeo ya uchaguzi wa Viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ngazi ya Vijiji, Vitongoji na Mitaa uliofanyika tarehe 24/11/2019 kwa waandishi wa habari ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma.

Mhe. Jafo amesema katika mchakato wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019 jumla ya nafasi 332,160 zilihusika katika uchaguzi ambapo kulikuwa na Vijiji 12,262, Mitaa 4,263, Vitongoji, 63,992, wajumbe kundi la wanawake 106, 622, wajumbe kundi mchanganyiko 145,021.

Amefafanua kuwa jumla ya wananchi 555,036 kutoka vyama mbalimbali vya siasa walifanikiwa kuchukua fomu za kugombea ambapo wananchi waliorejesha fomu ni 539,993 sawa na asilimia 97.3.

Mhe. Jafo amesema kuwa Chama Cha Mapinduzi kilipita bila kupingwa kwa jumla ya nafasi za uongozi 316, 474 ambapo nafasi ya Mwenyekiti wa Kijiji waliopita ni 12,028, Wenyeviti wa Vitongoji 62,927, Wenyeviti wa Mitaa 4,207, Wajumbe kundi la Wanawake 105,953 na Wajumbe kundi mchanganyiko 131, 359.

Ameitaja mikoa ambayo wagombea wa nafasi zote za uongozi walipita bila kupingwa kupitia Chama Cha Mapinduzi ni Tanga, Katavi, Ruvuma na Njombe. Ameendelea kusema kuwa Chama cha CUF kimepata nafasi moja katika ngazi ya wenyeviti wa vijiji, wajumbe kundi la wanawake wamepata nafasi tatu na wajumbe kundi mchanganyiko wamepata nafasi 14.

Mhe. Jafo amesema kwa upande wa Chadema, wenyeviti wa vijiji imeshinda nafasi moja, haikufanikiwa kupata Wenyeviti wa Mitaa, Wenyeviti wa vitongoji imepata nafasi 19, wajumbe kundi la wananawake imepata nafasi 39 na wajumbe kundi mchanganyiko nafasi 71.

Amesema Chama cha ACT Wazalendo kilipata uongozi ngazi ya Wenyeviti wa Vitongoji nafasi moja, wajumbe kundi la wanawake nafasi moja na wajumbe mchangayiko 11, wakati Chama cha UDP kilipata nafasi moja kwa upande wa wajumbe kundi la wanawake na Chama cha DP kikipata nafasi moja.

Amevishukuru vyama vya siasa ambavyo vimeonyesha ukomavu wa kisiasa na kudumisha demokrasia nchini kwa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Aidha, amewashukuru wananchi, viongozi wa serikali katika ngazi ya wizara, taasisi, idara za serikali, mikoa, wilaya, halmashauri, tarafa, kata, vijiji na mtaa kwa kushiriki kikamilifu kusimamia na kukamilisha uchaguzi kwa amani.

Sitanii, haijapata kutokea. Nimeirudia taarifa hiyo, kuonyesha maajabu yaliyopata kutokea Tanzania pekee. Mikoa minne CCM wagombea wake walishinda asilimia 100 bila kupingwa. Maeneo mengi ya nchi, CCM ilishinda ama bila kupingwa au kwa kura asilimia 100. Zipo nyakati au maeneo ambayo wagombea walijipigia kura, lakini wakati wa kuhesabu ikabainika hata wao hawakupata hata kura moja.

Mbaya zaidi katika uchaguzi huo, zilitumika mbinu za kujaza vibaya fomu. Asilimia kubwa ya fomu za wapinzani zilikataliwa kwa maelezo kuwa zimejazwa vibaya, hawajui kusoma na kuandika. Baadhi ya ofisi, watendaji walizikimbia hadi muda wa kurudisha fomu wa saa 10 ukapita. Kimsingi, wachambuzi mbalimbali uchaguzi wa mwaka 2019 na baadaye 2020 walisema haukuwa UCHAGUZI, bali ulikuwa UCHAFUZI.

Rais Samia Suluhu Hassan hakuyapenda haya. Mwaka 2022 aliunda Kikosi Kazi cha Hali ya Siasa Nchini. Kwa hakika kikosi kazi hiki kiliwasilisha taarifa iliyokuwa na sura 11. Taarifa hii imekuwa mwanga wa kurejesha demokrasia nchini. Mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni. Ni baada ya taarifa ya Kikosi Kazi, mikutano ya hadhara imerejeshwa, masuala ya wagombea kupita bila kupingwa sheria imeyazuia na kwa hakika, siasa sasa zinafanyika.

Tunawasikia viongozi wa kisiasa wakifanya mikutano nchi nzima. Nafahamu hapa katikati maandamano ya wapinzani yalizuiwa na polisi. Maandamano hayo yaliitishwa baada ya vuguvugu la kisiasa nchini Kenya ambalo lilivunja Baraza la Mawaziri na sasa wimbi lake limemchukua Makamu wa Rais, Rigathi Gachagua.

Sitanii, najua wapo wanaosema wangeachwa waandamane, ili kama mwisho wa siku ingeonekana wanavunja amani ndipo wazuiwe. Kamanda wa Polisi mmoja aliniambia: “Hivi sisi tuliopewa dhamana ya kuimarisha ulinzi wa nchi yetu, watu wametwambia kuwa wanataka kufanya kama Kenya, huko Kenya wameuliwa watu 52…

“Kwa hiyo na sisi tuache waue watu 52 kama Kenya, kweli? Si unaona tumezuia wasiandamane hakuna aliyekufa, na hata hao tuliowaweka chini ya ulinzi, maana hatukuwakamata tuliwapa hifadhi ya muda, ndiyo maana hawakulala ndani tukawaruhusu usiku wakaenda kulala nyumbani kwao… sisi Tanzania ni nchi ya amani, hatutaki vurugu. Kama wanaandamana kwa amani, hata maji ya kunywa tunawanunulia.”

Ukiacha hayo maandamano, kwa kiasi kikubwa uandikishaji wa wapigakura umekwenda vizuri, japo nasikia mabishano ya takwimu. Kwamba watu zaidi ya milioni 30 walioandikishwa wametoka wapi katika nchi yenye watu milioni 63. Yote yanaweza kutokea, ila nashauri jambo moja kubwa. Vyombo vya dola vilinde amani, na visitumike kuminya demokrasia kama ilivyofanyika mwaka 2019.

Sitanii, haiingii akilini na wala haitakaa ikubalike, kuwa mikoa minne, mitaa na vitongoji hadi wajumbe wote wanapita bila kupingwa. Hii ni Tanzania ya Watanzania wote. Vyama vya siasa vifanye ushawishi, badala ya kutumia mabavu. Niliamini na napenda kuamini kuwa CCM ikishinda kihalali, kama ilivyotokea mwaka 2005 Rais Jakaya Kikwete alipopata zaidi ya asilimia 80 hata Freeman Mbowe akampongeza, hakutakuwapo malalamiko.

Lakini pia kama vyama vya upinzani vikishinda katika maeneo mbalimbali, CCM iwe tayari kuvipongeza na kuacha vikabidhiwe viti vilivyoshinda bila mizengwe, vionyeshe uwezo wao wa kuongoza. Viongozi wa vyama vya upinzani na chama tawala wote ni Watanzania. Katika uchaguzi huu ambao ni wa ngazi ya chini kabisa, vyama na wagombea washindanishe sera si matusi na kejeli.

Katika ngazi ya mtaa na vitongoji ndiko vinakopimwa viwanja. Ndiko miradi ya kujenga barabara, maji, hospitali, shule, ulinzi na usalama wetu iliko. Ni bahati mbaya Watanzania wengi wanataka kukimbilia udiwani, ubunge na urais. Hakika ngazi hizo tatu bila viongozi imara katika serikali za mitaa, inakuwa ngumu kufanikisha maendeleo.

Sitanii, natumaini kuwaona wastaafu wengi wakichukua fomu kugombea nafasi hizi. Wakifanya hivyo, watakuwa wanaendeleza utumishi wa umma.

Katika ngazi ya serikali za mitaa ni sawa na utume wa kanisani au msikitini. Huko ni kutoa huduma, usitarajie mafao. Ni bahati mbaya baadhi ya viongozi wa ngazi hizi wamekuwa chanzo cha migogoro hasa eneo la kuuza viwanja.

Yote kwa yote, naomba Watanzania tujitokeze kwa wingi kupiga kura na kuchagua viongozi tunaowapenda. Tushiriki mikutano ya hadhara, kuhakikisha tunawasikiliza wagombea, tunawauliza maswali na mwisho wa siku tuwapigie kura tukifahamu wameahidi kututendea lipi tukiwachagua. Tunataka Novemba 27, 2024 Tanzania ifanye uchaguzi, si uchafuzi. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404827