Mbwana Samatta ndiye staa wa Tanzania kwenye soka. Ndiye mchezaji bora zaidi kuwahi kutokea Tanzania. Hili halina ubishi. Kama unataka kupinga hili, unaruhusiwa.

Hakuna ubishi kwamba kwenye kikosi cha Taifa Stars, Samatta ndiye mchezaji aliyepiga hatua zaidi. Ndiye mchezaji aliyefanikiwa zaidi. Ndiye mchezaji mwenye kipaji zaidi. Kuna mtu anayebisha? Basi atakuwa na chuki binafsi.  

Siku zote tumekuwa tukimtazama Samatta kama kioo cha soka letu. Tumekuwa tukimtazama kama mkombozi wetu. Hata hivyo bado kuna maswali mengi juu ya namna Samatta anavyowajibika kwenye timu ya taifa.

Kuna ambao wanasema Samatta hana msaada na timu kwa sababu hajitumi ipasavyo. Kuna ambao wanasema Samatta ni muhimu. Mjadala ni wa moto kweli kweli. Uzuri ni kwamba mjadala huu hata Samatta mwenyewe ameuona na ametoa majibu. Amekiri kuwa mjadala huu unampa chachu ya kupambana zaidi.

Hata hivyo, naomba tulitazame hili kwa makini. Mjadala huu uanze kwenye takwimu, kisha tutarejea uwanjani. Kama tunataka kumsema Samatta, lazima tujenge hoja thabiti. Ni lazima tumwonyeshe kwamba ameteleza wapi.

Katika michezo minane ya mwisho ya Taifa Stars ambayo Samatta amecheza, amefunga mabao matano na kuchangia upatikanaji wa mabao mengine mawili. Mechi nyingine moja aliangushwa ikazaliwa penalti, ilikuwa dhidi ya Uganda. Kwa kifupi amehusika katika mabao manane.

Mgawanyo wa mabao yake kuanzia Oktoba mwaka jana uko hivi: Aliwafunga Cape Verde bao moja na kutoa pasi ya bao la pili wakati Tanzania ikishinda 2-0 jijini Dar. Alifanyiwa faulo iliyozaa penalti kwenye ushindi wa 3-0 dhidi ya Uganda mapema mwaka huu.

Samatta akafunga bao jingine na kuchangia upatikanaji wa bao jingine baada ya shuti lake kuokolewa na golikipa wa Kenya na kisha Simon Msuva kufunga kwenye mechi ya AFCON dhidi ya Kenya pale Misri.

Baada ya AFCON, Samatta ameichezea Taifa Stars mechi nne na kufunga mabao mawili. Alifunga kwenye mechi ya kuwania kufuzu hatua ya makundi ya kusaka tiketi ya Kombe la Dunia dhidi ya Burundi. Amefunga tena wiki iliyopita dhidi ya Libya, kwa mkwaju wa penalti. Kama ni kufunga, Samatta amefunga sana tu katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, hadi ndoa amefunga.

Ni Simon Msuva pekee aliyeweza kufunga idadi hiyo ya mabao. Msuva amefunga mara tano kama Samatta, lakini mawili kati ya hayo yametokana na kazi nzuri ya Samatta. Kwa kifupi, Msuva ameng’ara kwenye michezo hiyo kutokana na msaada mkubwa anaopewa na Samatta. Pia mfumo wa sasa unampa uhuru zaidi Msuva kuliko Samatta.

Mechi ambazo Msuva amefunga kwenye kipindi cha mwaka mmoja uliopita ni dhidi ya Cape Verde, Uganda, Kenya, Burundi na Equatorial Guinea. Inavutia sana. Je, Samatta anang’ara kwa msaada wa nani?

Turejee uwanjani sasa. Ni kweli kwamba kwa siku za karibuni, Samatta amepungua nguvu kidogo katika timu ya Taifa. Wengi tunatamani kuona akifanya kile alichokifanya dhidi ya Liverpool pale Anfield. Wengi tunatamani kuona akifanya zaidi na zaidi, lakini tumewahi kujiuliza, nani anamsaidia Samatta kufanya hayo?

Kwenye kikosi cha Stars, washambuliaji wengine wote wanamtegemea Samatta. Wanasubiri yeye apige chenga kisha awape pasi za kufunga. Angalau Msuva amekuwa akitegemea kufunga pia kwenye mashambulizi ya kushtukiza. Mara nyingi viungo na mabeki pia wamekuwa wakitegemea mbio zake, hivyo kumpigia pasi ndefu ili aweze kufunga.

Ni nani ambaye anacheza kwa ajili ya Samatta? Nani amewahi kupiga chenga na kumtengenezea Samatta nafasi za wazi katika mechi za Stars? Ni wazi kuwa hakuna.

Bao la Samatta dhidi ya Cape Verde alipokea pasi ya Mudathir Yahya nje ya eneo la hatari, akapiga shuti kali na kufunga. Bao alilofunga dhidi ya Kenya pale Misri zilikuwa jitihada binafsi. Bao alilofunga dhidi ya Burundi ilikuwa ni mpira wa kona, akafunga kwa kichwa. Angalau bao la juzi dhidi ya Libya lilikuwa la penalti.

Kabla hatujamlaumu Samatta, tujiulize ni kwa kiasi gani timu inacheza kwa ajili yake? Ni lazima tujiulize ni mchezaji gani anajituma ili Samatta aweze kung’ara katika kikosi cha Stars? Bila shaka hakuna.

Tunamtaka Samatta awe mungu mtu. Tunataka akabe, apige chenga, atoe pasi za mabao na akafunge mwenyewe. Duniani kote hii haipo. Inatokea mara chache sana. Lazima timu ifanye kitu kwa ajili ya Samatta ili aweze kung’ara na kuisaidia timu.

Nadhani wakati huu ambao tuna mechi muhimu za kuwania kufuzu AFCON na Kombe la Dunia, tunamhitaji Samatta akiwa bora zaidi. Tunahitaji kumtia moyo zaidi. Wachezaji wenzake wanahitaji kufahamu kuwa ipo haja ya kucheza kwa ajili ya Samatta. Nadhani hapa tutakuwa tunajenga.

Nyakati za sasa si za kunyoosheana vidole, ni nyakati za kushikamana. Tukianza kumlaumu Samatta kwa kutocheza kwenye ubora wa juu hatutakuwa salama. Kama Samatta anacheza vibaya, tumtaje aliyecheza vizuri. Wengine wamefanya kitu gani cha ajabu?