Jana, Julai 18, ni Siku ya Mandela, inayoadhimishwa kila mwaka, kama ilivyotangazwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2009, kutambua mchango wake katika kuutokomeza ubaguzi wa rangi Afrika Kuisini.
Katika kuikumbuka Siku ya Mandela, Rais wa Kwanza wa Afrika Kusini huru, kuadhimisha kuzaliwa kwake mwaka 1918, hakuna kipya sana cha kuandika kwa vile yameandikwa mengi mno juu yake.
Umaarufu wa Mandela ni tangu wakati wa harakati zake za kuung’oa utawala wa kibaguzi wa Afrika kusini, kuanzia miaka ya 1950; kufungwa gerezani kwa miaka 27; kuachiwa huru, Februari 11, 1990; ushindi wake na kuwa Rais, 1994 hadi 1999; maisha yake ya kustaafu hadi kifo chake, Desemba 5, 2013.
Katika makala hii ya Siku ya Mandela nimedokoa tu yale ambayo labda pengine hayakuwa yameandikwa sana. Nimeyasisitiza machache mengine ili kumuelezea mwanamapinduzi huyo wa Kiafrika aliyeacha kumbukumbu isiyoweza kufutika duniani.
Mbele ya jaji wa kikaburu, Quartus de Wet, akiwa anakabiliwa na mashitaka ya uhaini na kufanya hujuma dhidi ya utawala wa makaburu yanayobeba adhabu ya kifo, Mandela alisema, kwa mujibu wa taarifa za kesi hiyo:
“Katika maisha yangu, nimejitoa kwa ajili ya mapambano haya ya Waafrika. Nimepigana dhidi ya ukandamizaji wa watu weupe. Nimepigana dhini ya ukandamizaji wa watu weusi. Nimetetea lengo la kuwepo kwa jamii ya kidemokrasia iliyo huru ambapo watu wote wataishi kwa amani na kuwa na fursa sawa. Nitaishi kutetea lengo hilo na kuhakikisha lifanikiwa. Lakini kama hapana budi, niko tayari nife kuhakikisha linatekelezeka”.
Hiyo sentensi ya mwisho kuhusu kifo, mawakili wa Mandela wanasemekana walimsihi asiitamke, ili kutowapa kisingizio kizuri majaji wa makaburu kumuhukumu kifo mpigania ukombozi huyo, kwa vile ametamka yuko tayari afe. Lakini Mandela aliisoma, bila ya hofu.
Katika kile kilichojulikana kuwa “Kesi ya Rivonia” kuchukua jina la kitongoji kimoja cha Johannesburg, kulikokokuwa na shamba la Liliesleaf, palikokuwa na maficho ya viongozi wa chama cha African National Congress – ANC, ilimchukua saa nne nzima Mandela kutoa maelezo yake hayo ya utetezi aliyoyasoma. Aliyatayarisha mwenyewe kwa wiki kadhaa akiwa mahabusu, kabla ya kufikishwa kizimbani.
“Sikanushi kuwa nilipanga njama za hujuma. Nimepanga njama hizo siyo kwamba ni mtu nisiye na hadhari au kwamba ni mtu wa kupenda kutumia nguvu, la hasha. Nimepanga njama hizo nikiwa na akili timamu na baada ya kutafakari kwa kina hali ya kisiasa iliyoibuka kutokana na miaka kadhaa ya utawala dhalimu, wa unyonyaji na ukandamazaji dhidi ya watu wangu ambao umekuwa ukiendeshwa na makaburu…” alisema Mandela katika chumba cha mahakama kilichokumbwa na ukimya mkubwa mjini Pretoria, makao makuu ya utawala wa makaburu.
Hakuna njia nyingine ila kutumia nguvu, kwa kuwa njia za amani zimezuiwa kwa sheria
Aliongeza: “Nakiri mara moja, tena bila ya kusita, kuwa mimi ni mmoja wa watu walioanzisha Umkhonto wa Sizwe (“Mkuki wa Taifa”, kitengo cha kijeshi cha chama cha ANC) na kwamba nilishiriki kikamilifu katika shughuli zake hadi nilipokamatwa Agosti mwaka 1962.
“Tulibaini kwamba bila ya kutumia nguvu, hapatakuwa na njia yoyote kwa Waafrika kufanikiwa katika harakati zao za kuutokomeza utawala wa makaburu unaowakandamiza. Njia za kufuata sheria na za amani za kuonyesha kuupinga utawala huo, zimefungwa kwa kutumia sheria, na tukafikishwa mahali ambapo ama tukubali muda wote kudhalilishwa au kwenda kinyume na serikali. Tukaamua kwenda kinyume na sheria…”.
Baada ya maelezo hayo ya utetezi ya Mandela, Jaji de Wet alimtaka wakili wa utetezi, Fischer Bram awaashirie washitakiwa waliobaki nao kutoa maelezo yao ya utetezi, mmoja baada ya mwingine. Wengine waliyatoa kwa maandishi na kuyasoma, wengine kwa kujieleza bila ya maandishi.
Ni dhahiri utetezi wa Mandela, ulithibitisha ujasiri wa mwanamapinduzi huyo, wakati huo akiwa na umri wa miaka 45. Aliibua vugu vugu kubwa la kutetea wapigania ukombozi hao waliokuwa kizimbani. Lawama dhidi ya utawala wa makaburu zilitolewa Afrika Kusini kwenyewe, kutoka nchi nyingine za Afrika na kutoka kwa wapenda amani duniani kote. Maazimio ya Umoja wa Mataifa, maandamano, mawasiliano ya kidiplomasia, vyote vilitawala kutetea ukombozi wa Afrika Kusini na kuwalaani makaburu kwa ushenzi wao wa ubaguzi wa rangi, ukandamizaji na kutowatendea haki Waafrika.
Ilimchukua wiki tatu kabla ya Jaji de Wet kutoa hukumu: “Nimeamua nisitoe hukumu ya juu kabisa,” akimaanisha ya kifo. Hata hivyo, wapigania ukombozi hao wote walikwishaamua kutojishughulisha kamwe na kukata rufaa endapo watahukumiwa kifo. Jaji aliongeza: “Hukumu kwa watuhumiwa wote ni kufungwa maisha”.
Waliokamatwa Julai 11, 1963 ni Mandela (ingawa yeye hakukamatwa Rivonia kwenye maficho ya viongozi wa ANC, kama walivyokamatwa wenzake, ila aliunganishwa baadaye, kwa kuwa alikuwa tayari gerezani mjini Pretoria tangu Oktoba, 1962 kwa kutoroka na kurudi nchini kwa siri na kuchochea maandamano); Walter Sisulu; Govan Mbeki; Raymond Mahlaba; Andrew Mlangeni; Elias Motsoaledi; Ahmed Kathrada; Denis Goldberg; Lionel ‘Rust’ Bernstein; Bob Hepple; Arthur Goldreich; Harold Wolpe na James ‘Jimmy’ Kantor.
Goldberg (mhandisi aliyekuwa anatoa michoro ya majengo na miundombinu mingine ya utawala wa makaburu kwa ajili ya kushambuliwa; Bernstein (msanifu majengo na mwanachama wa chama cha Kikomunisti cha Afrika Kusini); Hepple; Goldreich (ambaye alikuwa mmiliki wa shamba la Liliesleaf, Rivonia lililokuwa ni maficho); Wolpe na Kantor (shemeji yake Wolpe), walikuwa wenye asili ya Kiyahudi.
Waliohukumiwa kufungwa maisha ni Mandela; Sisulu; Mbeki; Mahlaba; Mlangeni na Goldberg, ambaye yeye alifungiwa gereza kuu la Pretoria, lililokuwa maalum kwa wafungwa wa kisiasa wazungu, badala ya gereza la Robben Island, walilofungiwa wenzake.
Mandela alijifanya mtunza bustani na mpishi, akiwa mafichoni Shamba la Liliesleaf, Rivonia kitongoji cha Johannesburg
Goldreich na Wolpe, waliotoroka walipokuwa rumande, baada ya kumhonga askari magereza. Baada ya kujificha kwenye kibanda kimoja mjini Johannesburg ili msako utulie, walivaa kama mapadre na kusafiri kwenda Swaziland na baadaye katika eneo la koloni la Bechuanaland (ambalo sasa ni sehemu ya Afrika Kusini) , ambako walisafiri hadi kwenye kiwanja cha ndege kidogo, walikopanda ndege ndogo hadi kwenye usalama jijini Dar es Salaam. Huko Bechuanaland, majasusi wa Afrika Kusini waliilipua ndege ambayo walidhani watoro hao wangeitumia kutorokea. Kumbe watoro hao walipangiwa ndege nyingine kwenye kiwanja hicho kingine kidogo. Bernstein aliachiwa huru .
Mandela alikuwa amehamia kwenye shamba la Liliesleaf katika kitongoji cha Rivonia, Oktoba 1961, baada ya chama chake hicho, kilichoanzishwa mwaka 1912, kupigwa marufuku na makaburu mwaka 1960. Hapo alipojificha, alijifanya mtunza bustani na mpishi, akiitwa David ‘Motsamayi’ (David Mtembezi). Polisi walivamia shamba hilo na kuwafurusha na kuwatia mbaroni viongozi hao wa ANC, baada ya kudokezwa na mtoa habari mmoja.
Alipotoroka Afrika Kuisini na kwenda nchi za Afrika, akianzia na Tanzania, ambayo wakati huo ni Tanganyika, Mandela alisema katika ksi hiyo kuwa alipokewa na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika, Julius Nyerere. Baadaye alikwenda Addis Ababa na kukutana na Mfalme Haille Sellasie wa Ethiopia na kupata nafasi ya kukutana na viongozi wengine waliokusanyika hapo kwa mkutano wa baadhi ya nchi za Afrika zilizokuwa huru wakati huo: kiongozi wa kijeshi wa Sudan, Jenereali Abboud; Rais Habib Bourguiba wa Tuninia; Rais Ben Bella wa Algeria; Rais Modibo Keita wa Mali; Rais Leopold Senghor wa Senegal; Rais Sekou Toure wa Guinea; Rais William Tubman wa Liberia na Waziri Mkuu wa Uganda, Militon Obote. Algeria, alikaribishwa Oudja, makao makuu ya jeshi la nchi hiyo na kupewa mafunzo ya kijeshi. Alisema mafunzo hayo yalikuwa muhimu na ni kwa ajili ya maandalizi ili ashiriki bega kwa bega na wapiganaji wa ANC, wakati mambo yatakapoiva.
Mandela alikaa gerezani Robben Island, kwenye pwani ya mji wa Capetown kwa miaka 18, akifanyishwa kazi ngumu, akiruhusiwa tu kupata barua moja na mgeni mmoja, kila baada ya miezi sita. Baadaye, 1982, Mandela na wenzake akina Sisulu; Mlangeni; Mahlaba na Kathrada walihamishiwa gereza la Pollsmoor, kwenye kitongoji cha Capetown.
“Anayestahili kufanya majadiliano ni mtu aliye huru. Mfungwa hawezi kuingia mkataba…”
Akiwa gerezani, kuna habari kuwa kuna watu walimshawishi atoroke, lakini akabaini kuwa zilikuwa ni njama za kutaka kumwua wakati anatoroka. Wakati wimbi la ukombozi linazidi, utawala wa makaburu ulifanya mpango kutaka Mandela aachiwe huru, kwa masharti kwamba aachane na harakati za kutumia nguvu, lakini Mandela alikataa katu katu kwa kusema: “anayestahili kufanya majadiliano ni mtu aliye huru. Mfungwa hawezi kuingia mkataba…”. Goldberg alikuwa mfungwa wa kwanza wa Kesi ya Rivonia, kuachiwa huru.
Februari 11, 1990, Mandela aliachiwa huru na Rais wa utawala wa makaburu wa wakati huo, F.W. de Klerk na mwaka uliofuata, akachaguliwa kuwa Rais wa ANC, baada ya chama hicho pia kuruhusiwa kufanya shughuli zake, katika mabadiliko ya kuleta suluhu Afrika Kusini.
Baada ya majadiliano ya kuleta mfumo wa Serikali isiyokuwa ya kibaguzi, yaliyomhusisha Mandela akiwa huru, utawala wa makaburu ukasalimu amri na kuitisha uchaguzi mkuu wa kwanza wa kushirikisha watu wa rangi zote, Aprili 1994. ANC ikapata asilimia 62 ya kura zote. Mei 10, 1964 Nelson Mandela, akatawazwa kuwa Rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini na kuuzika utawala wa kibaguzi wa makaburu, uliodumu kwa takriban karne tano.
Huo ndio ujasiri wa Mandela. Baada ya viongozi wa Kiafrika wa aina ya Mandela, Nkrumah na Nyerere, ambao wote sasa ni marehemu, kufanikiwa kuleta ukombozi wa kisiasa na kuutokomeza ukoloni mkongwe na ubaguzi katika bara hili, Afrika sasa inahitaji viongozi watakaoleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kuuzika ukoloni mambo leo unaolitafuna bara hili.
Kutoka kwa Mandela, tumepata somo la kutosha kuwa maendeleo makubwa ya kiuchumi katika Afrika yanawezekana na yataletwa na Waafrika wenyewe kwa kujiamini, kujituma, kujinyima na kufanya kazi kwa bidii na kutumia rasilimali lukuki za bara hili, tunazoziweka sisi wenyewe kwenye mikono ya waporaji kutoka nje. Kama ukombozi wa kisiasa uliwezekana, inatubidi tuwachague akina Mandela wengine watakaotuongoza kufanikisha maendeleo ya kiuchumi. Aina ya viongozi wengine, wanaojinufaisha wenyewe na kujilimbikizia mali, wakiwanyanyasa na kuwakandamiza wananchi wao wanyonge, huku wakiwaenzi na kuenziwa na wakoloni wetu wa zamani, hawatufai, wanatupotezea muda.
Saidi Nguba ni mwandishi wa habari mkongwe nchini aliyepata kuwa Mhariri wa Magazeti ya UHURU na MWANANCHI na amestaafu akiwa Msaidizi wa Waziri Mkuu – Masuala ya Habari. Simu: 0754-388418; Barua-pepe: [email protected]